Pinda kushuhudia kuhama kwa nyumbu

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sherehe za Siku ya Mara, maarufu kama (Mara Day), zinazofan... thumbnail 1 summary
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sherehe za Siku ya Mara, maarufu kama (Mara Day), zinazofanyika wilayani Serengeti, mkoani Mara kuanzia jana hadi Septemba 15, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tupa, alisema madhumuni ya maadhimisho hayo ni kushuhudia tukio kuu la kuhama kwa makundi makubwa ya nyumbu kutoka Hifadhi ya Masai Mara kwenda Serengeti.
Alisema lengo jingine ni kuuenzi Mto Mara, ambao asili yake ni kutoka milima ya Mau nchini Kenya na ambao hupitia katika mapori ya akiba na wanyama walioko katika hifadhi hiyo hutegemea maji ya mto huu.
“Kwa kutambua umuhimu wa bonde hilo, kikao kilichofanyika mwaka juzi mjini Kigali, Rwanda kiliamua kila mwaka yafanyike maadhimisho ya Siku ya Mara na mwaka jana wenzetu wa Kenya walifanya sherehe hizi katika sehemu moja iitwayo Muroti na mwaka huu ni zamu yetu,’’ alisema Tupa.
Alifafanua kuwa katika maadhimisho hayo wamealika wageni 110 na kati ya hao wageni 200 watatoka nchi jirani ya Kenya wakiwamo mawaziri wa maji, Tamisemi, Maliasili, Mazingira - Ofisi ya Makamu wa Rais na wadau mbalimbali wa mazingira nchini.
Mkuu huyo alibainisha kuwa faida za maadhimisho hayo ni kuimarisha ushirikiano, uhifadhi wa bonde la Mto Mara, kuleta mwamko kwa Watanzania ili waweze kufahamu uhifadhi na utalii hasa wa ndani.
Alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kuhudhuria sherehe hizo ili waweze kushuhudia namna mkoa huo ulivyojiandaa, pia watapata fursa ya kutembelea mabanda na kujionea mambo mbalimbali.
Kwa mjibu wa Tupa, kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni: “Mara Mali Yetu, Urithi Wetu Tuutunze."