Kama hadi sasa hujaamini kuwa ujangili
ni janga la dunia naamini hatua ya Mtoto wa Mfalme Prince William kumwomba mchezaji
David Beckham kuungana naye katika kupambana na ujangili na biashara ya
wanyamapori itakufanya upate picha kamili.
Beckham alipoombwa kushirika katika
kampeni hiyo ambayo imepewa jina la United for Wildlife hakuwa na kipingamizi
na hivyo kuwekwa kwenye list ya watu mashuhuri watakaoshirika kampeni hiyo
ambayo inafanyika chini ya usimamaizi wa foundesheni ya ufamle (Rayal
Foundation) ambayo mbali na mambo mengine kazi yake ni kupinga ujangili na
biashara ya nayara za wanyamapori.
Siku
moja tu baada ya kutangaza kuacha kutumikia jeshi Prince Williams ameweka wazi
kampeni yake ya kupinga ujangili aliyoipa jina la United for Wildlife ambayo
itashirikisha pia taasisi kubwa na zenye ushawishi mkubwa ulimwenguni kwenye
masuala ya vita dhidi ya ujangili
Taasisi hiyo itajikita zaidi katika kukomesha biashara haramu ya
wanyamapori na zana zake, na itampa muda mwingi Prince William kuitumikia baada
ya kumaliza miaka saba katika jeshi.
Prince William ambaye ndiye rais wa taasisi hiyo mpya wiki hii aliungana
na Beckham na Mchezaji wa zamani wa basket kutoka China Yao Ming kurekodi video
mbili za kupinga biashara haramu ya wanyamapori ikiwa ni msaada kwa taasisi ya
kupambana na ujangli na biashara ya ujangili ya WildAid.
Video hizo ambazo zitaonyeshwa hivi karibuni zinalenga kufikisha ujumbe
kwenye nchi za mashariki ya mbali na China ambako kuna soko kubwa la bidhha
zinazotokana na wanyamapori zilizozuiliwa hasa za tembo na faru.
Inakadiriwa kuwa tembo 25,000 huuawa kila mwaka na majangili wakati faru
618 wameshauawa kwa mwaka huu pekee na kuweka hali ya hatari ya kupotea kwa
viumbe hao katika miaka michache ijayo.
Beckham anasema: “Nilipoambiwa kiwango cha ujangili barani Afrika,
nilikubali moja kwa moja ombi la Prince William la kufikisha ujumbe huu wa kupinga
ujangili, inasikitisha na kushangaza kutambua kuwa kumbe tunaweza kuwakosa
wanyama hawa katika kipindi cha uhai wetu”
Lakini kwake Yao Ming, mmoja wa wanamichezo wakubwa kutoka China anasema:
"Ni lazima tupunguze (China) mahitaji kama tunataka kuwanusuru wanyamapori
hawa, tulifanikiwa kuzuia biashara ya nyangumi ambapo sasa biashara hiyo
imepungua na kufikia asilimia 50 hivyo naamini Serikali ya China inaweza
kufanya hivyo hata kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru”
Prince William akizungumzia uanzishwaji wa umoja huo United for Wildlife
anasema: “Tishio la kupotea kwa urithi wetu wa asili ni kubwa lakini naamini
ushirikiano huu tuliouanzisha utachochea harakati njema za kulinda viumbe hai
na wanyama waliokatika athari kwa ajili ya kizazi kijacho”
"Mzizi wa ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ni soko, hasa pale
unapoona soko linahitaji malighafi ambayo ili ipatikane lazima maelfu ya
wanyama hao wauawe, jambo linalowaangamiza na kufanya wapotea ulimwenguni
katika kipindi kifupi kijacho”
Anasema kuwa ni lazima kutumia muda huu kufanya kazi pamoja kulinda
rasilimali hizo ili kutoa fursa kwa watoto wanaozaliwa leo kuwaona wanyama hao na
kufurahia urithi huo ambao kila mtu mwenye mapenzi mema angependa kuendela kuuona.
Taasisi saba zilizoungana na taasisi ya Royal Foundation katika
kutekeleza program ya United for Wildlife ni pamoja na Conservation
International, Fauna & Flora International, International Union for
Conservation of Nature, The Nature Conservancy, Wildlife Conservation Society,
WWF-UK na taasisi ya Zoological Society ya London.