Raia wanne wa Pakistan wapandishwa kizimbani kwa kuua tembo na nyati

RAIA wa nne  Raia  wa nchini Pakistani jana walifikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,  wakikabiliwa na mashtaka... thumbnail 1 summary
RAIA wa nne  Raia  wa nchini Pakistani jana walifikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,  wakikabiliwa na mashtaka  ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha  nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 52.6 kwenda  jiji la Guangzhou China, kuwinda wanyama na kuwaua bila kibali.
Mbele ya Hakimu Mkazi  Sundi Fimbo, wakili wa serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa hao kuwa mfanyabiashara na mkazi wa Mount Meru View Arusha,   Kamran Ahmed (32), Wafanyabiashara na wakazi wa Mtaa wa Mkunguni Kariakoo, Usman Afzal(32), Shekh Mohammad (30) pamoja na  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Paktan Company Limited, Mohammad Sufian (27).
Wakili Nchimbi alidai washitakiwa hao  walitenda makosa hayo  kati ya Januari Mosi, mwaka 2005 na Septemba 14, mwaka 2013. Na kuwa  washtakiwa wote kwa pamoja hao walisafirisha meno ya Tembo yenye mng’ao mweupe 50 yenye thamani  ya Sh 6,480,000  kwenda jiji la Guangzhou nchini China.
Wakili Nchimbi alidai kuwa shitaka jingine ni la  washitakiwa waliwinda na kuua wanyama akiwamo Tembo mmoja mwenye thamani ya dola za Kimarekani 15,000, Chui mwenye thamani ya dola za Kimarekani 3,500 na Duma mmoja mwenye  thamani ya dola za Kimarekani 4,900.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kuwawinda na   kumuua Nyati mmoja mwenye thamani ya dola za Kimarekani 1,400, Pundamilia mwenye thamani ya dola za Kimarekani  1,200, Swala mwenye thamani ya dola za Kimarekani 320 pamoja na Eland mmoja mwenye thamani ya dola za Kimarekani 1,700 wote wakiwa na jumla ya Sh 46,202,400  mali ya Serikali na akadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Baada ya  wakili Nchimbi kumaliza kuwasomea mashitaka hayo, hakimu Fimbo aliwataka washitakiwa hao wasijibu chochote  kwasababu mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na akaiarisha kesi hiyo hadi Septemba 30 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa wapelekwe gerezani.

Jukwaa Huru