Serikali ya Tanzania yakana madai ya kuizuia Kenya kutumia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere (JNIA)

Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene  akizungumza  na waandishi wa habari leo jijini Dar es Sa... thumbnail 1 summary

Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene akizungumza  na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam  kuhusu  mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ulioituhumu  Serikali ya Tanzania.
 --------------
Na Fatma Salum-MAELEZO
 
SERIKALI  ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi yake zilizotolewa na mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ujulikanao kama  www.standardmedia.co.ke unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya gazeti la The Standard la nchini humo.
 
Akizungumza  na waandishi wa habari leo  jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene , alisema mtandao huo umeripoti kuwa  Serikali ya Tanzania imekataa kuiuzia Kenya gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina ukweli  kwa kuwa  gesi inayozalishwa hivi sasa bado haijafikia kiasi cha kuweza kuuzwa nje ya nchi.
 
Mtandao huo pia umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania ilikataa viwanja vyake vya ndege vya kimataifa kutumiwa na ndege zilizopaswa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata wakati wa ajali ya moto iliyotokea kwenye uwanja huo hivi karibuni.
 
Mwambene alifafanua kuwa tuhuma hizo ni za uongo kwani mara baada ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata kuwaka moto, ndege zilizotakiwa kutua uwanjani hapo ziliruhusiwa kutua kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania vya Julius Nyerere   International   Airport (JNIA) na Kilimanjaro International Airport (KIA).
 
“Sio kweli hata kidogo kwamba Tanzania ilikataa ndege za Kenya zisitue kwenye viwanja vyake kwa sababu uwanja wa Jomo Kenyata ulipoungua ndege nyingi zilizopaswa kutua katika uwanja ule zilitua kwenye viwanja vyetu na hii pia ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na Kenya zinachangia ndege nyingi za nje ya nchi.” Alisema Mwambene.