Taarifa toka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ina utaratibu wa kushirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi, ikiwa ni pamoja na asasi za... thumbnail 1 summary


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ina utaratibu wa kushirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi, ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia, taasisi za serikali, mahospitali, mashule, na vijiji kote nchini kwa kuchangia katika shughuli zao za maendeleo.  Michango inayotolewa na Mamlaka inalenga kuwawezesha wananchi kupitia vijiji, asasi, ama taasisi husika kwa kusaidia miradi mahususi iliyoainishwa kupitia maombi yao kwa Mamlaka na kupitishwa ofisi ya Mhifadhi Mkuu.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatoa misaada hiyo kama sehemu ya majukumu yake ya kushirikiana na wanajamii (corporate social responsibility). Aidha, Mamlaka imeendelea kutoa misaada hii kwa kutegemea uwezo wa kifedha, mkazo mkubwa ukiwa kwenye miradi ya Jamii zinazozunguka hifadhi, na vilevile, kusaidia miradi, majanga, na shughuli zingine kote nchini.  Kulingana na maombi na uwezo wa fedha wa Mamlaka.

Hivi karibuni kumetokea taarifa potofu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kjamii kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatoa msaada hiyo kwa baadhi ya Taasisi kwa mashinikizo ya kisiasa, taarifa ambazo hazina ukweli wowote na zina lengo la kufarakanisha Mamlaka na Wananchi ambao wamekuwa wakipokea misaada ya kibinadamu na kimaendeleo kwa kupitia utaratibu wa ujirani mwema wa Mamlaka. 

Habari hizi zinasikitisha, na si sahihi.

Tunapenda kutoa rai kwa umma kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea na jukumu lake la kusaidia jamii mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo, na kuwanusuru wananchi pale ambapo majanga yanatokea kama ilivyokuwa katika milipuko ya mabomu iliyotokea katika Jiji la Arusha hivi karibuni.
  
KAULI MBIU YETU
“UTALII UANZE NA MTANZANIA KWANZA”
Imetolewa na Kaimu Mhifadhi