Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
kimesema, Bara la Afrika lisipochukua hatua za makusudi za kupambana na
Mabadiliko ya Tabianchi, linaweza kuangamia kwa ugumu wa maisha.
Pia, chuo hicho kimeitahadharisha Serikali ya
Tanzania, kupambana na mabadiliko hayo hususan kutenga maeneo ya wakulima na
wafugaji kuepuka migogoro inayoweza kusababisha vurugu na kugharimu maisha ya
watu.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Kituo cha
Mabadiliko ya Tabianchi wa chuo hicho, Profesa Pius Yanda wakati akielezea
kuhusu mkutano wa kimataifa wa kujadili tatizo hilo utakaofanyika Oktoba 15,
mwaka huu jijini Arusha.
Profesa Yanda alisema, tatizo la mabadiliko ya
tabianchi barani Afrika linatokana na kutokuwapo kwa jitihada za makusudi za
kupambana na janga hilo.
Alisema katika mkutano huo utakaoandaliwa na
chuo hicho, utashirikisha wanasayansi na watunga sera kutoka Barani Afrika,
America na Asia ambapo Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo.
“Bara la Afrika limekuwa likifanya tafiti kidogo
katika mambo ya Tabianchi lakini hata hivyo, bado hazifanyiwi kazi hivyo
kupitia mkutano huo tutakuwa na wataalamu kutoka nje ya bara hili ambao
watatupa ujuzi wa kupambana na mabadiliko hayo,” alisema Profesa Yanda na
kuongeza:
“Ili kuelewa kwa kina jinsi ya kupambana na
mabadiliko haya, ni lazima kufanya tafiti nyingi zitakazobainisha ni maeneo
gani kunahitajika kufanyiwa kazi.”
Profesa huyo alisema, migogoro ya wafugaji na
wakulima inatakiwa kutengewa maeneo mapema kwa ajili ya shughuli zao ili
kuepuka pindi eneo fulani linapoathiriwa na mabadiliko hayo kuhamia katika eneo
jingine na kusababisha kutokea vurugu.
Chanzo: Mwananchi