ASKARI wa kikosi cha wanyamapori kwa kushirikiana
na wananchi wamelazimika kutumia nguvu ya ziada kuwaangamiza viboko wawili ambao walikuwa hatari kwa
usalama wa watu pamoja na uharibifu mkubwa wa mazao yanayolimwa pembezoni mwa
ziwa Victoria.
Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa wananchi
limetokea katika Kata ya Nyakato, Mtaa wa Baruti ndani ya Manispaa ya Musoma
ambako walikusanyika kushuudia viboko hao ambao wamekuwa wakiwataabisha kwa
muda mrefu.
Wakizungumza na Tanzania Daima, baadhi ya wananchi
ambao ni wakulima katika eneo hilo wamesema wanyama hao walikuwa wakiwasumbua
kwa muda mrefu kwani wamekuwa wakitoka ndani ya ziwa na kuvuka mita 60 kwenda
kuharibu mashamba.
Walisema hali hiyo iliwalazimu watoe taarifa katika
ofisi za maliasili na utalii na kuanzisha msako wa kuwaangamiza.
Aidha, wananchi hao wameeleza kuwa kuna baadhi ya
wakulima ambao walikwisha amua kutojihusisha na kilimo katika maeneo hayo,
lakini wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha wanyamapori
kuwaangamiza wanyama hao ambao wamekuwa kikwazo kikubwa katika shughuli za
maendeleo.
Chanzo: Tanzania Daima