WANANCHI HUPUUZIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA, HUISHI KIMAZOEA

WANANCHI wametahadharishwa kuacha tabia ya kuishi kwa mazoea hasa katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na badala yake waishi kuling... thumbnail 1 summary
WANANCHI wametahadharishwa kuacha tabia ya kuishi kwa mazoea hasa katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na badala yake waishi kulingana na mazingira ya hali ya hewa wanayotangaziwa na Mamlaka husika kwani kwa kuzitumia taarifa hizo vizuri kutasaidia kuongeza uzalishaji katika maeneo mengi ya sekta za uchumi na kupunguza vifo vitokanavyo na machafuko ya baharini na ziwani.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza ametoa tahadhari hiyo jana wakati akifungua warsha ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu huduma za hali ya hewa na nafasi ya vyombo hivyo katika sekta ya hali ya hewa mkutano ambao ulifanyika mjini Kibaha.

Mahiza amesema Watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kukurupuka tu kwa imani ya Mungu ndiye ajuaye na kujiendea katika shughuli zao ikiwemo za uvuvi,usafiri wa baharini na ziwani,kilimo hasa aina ya mazao yanayostahili kuyapanda wakati huo bila ya kufatilia hali ya hewa ya wakati huo inaelekeza nini,na kwa wakati gani.

Amesema ukurupukaji wa aina hiyo imekuwa ikichangia kushuka uchumi na pia kuleta madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya majini na kisha jamii kuilaumu Serikali wakati makosa wanayo wenyewe kwa utamaduni wao wa kutokuwa na tabia ya kufatilia matangazo ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayotolewa kila siku na Idara husika katika vyombo vya habari.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa mkoa ameitaka Mamlaka ya hali ya hewa nchini wakae na Waziri wa Uchukuzi watengeneze muswada mdogo wapeleke Bungeni waangalie namna ya kuwabana watu ambao hupuuzia matangazo ya mabadiliko ya hali ya hewa na kusababisha madhara.

Awali Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka wa hali ya hewa nchini(TMA) Dkt Agnes Kijazi amesema pamoja na ushirikiano uliopo na vyombo vya habari pia imekuwepo changamoto ya lugha inayotumika kutoeleweka vizuri pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kutoa taarifa ambazo hazijatolewa na Mamlaka hiyo.

Dkt Kijazi amesema hali hiyo imekuwa ikiwasababishia Mamlaka hiyo kupokea maswali mengi toka kwa wananchi pale ambapo utabiri huo unapokuwa si sahihi na kutofautiana sana na utabiri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.


Amesema kutokana na changamoto hiyo ndiyo maana Mamlaka ya hali ya hewa imeandaa warsha hiyo kwa Wahariri hao ili kwa pamoja wapate fursa ya kujadiliana na kukubaliana njia bora zaidi itakayowezesha taarifa sahihi zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa zinawafikia walengwa kwa wakati.