ASKARI WA HIFADHI WAINGIA KASHFA NYINGINE YA MAUAJI

NA DANIEL LIMBE Askari wa Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo wilayani Geita mkoani hapa, wamekumbwa na kashfa nyingine baada ya kudaiwa ku... thumbnail 1 summary
6_29584.jpg
NA DANIEL LIMBE
Askari wa Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo wilayani Geita mkoani hapa, wamekumbwa na kashfa nyingine baada ya kudaiwa kumuua raia mmoja kwa kipigo mbele ya kituo kidogo cha polisi Chato.
Aliyeuawa ametambulika kuwa ni Moshi Nkola (39), mkazi wa kijiji cha Mkuyuni kata ya Chato wilayani hapa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Pudensiana Protas, alidai kutokuwa na taarifa ya tukio hilo na kuahidi kufuatilia ukweli wa jambo hilo kutoka kwa wasaidizi wake.
Akielezea tukio hilo, kaka wa marehemu, Paulo Nkola (42), aliliambia NIPASHE Jumapili kuwa nduguye alipigwa na askari wawili wa hifadhi ya kisiwa cha Rubondo (hakuwataja majina) Oktoba 17, majira ya saa 4 usiku wakati akitoka kwenye duka la kuuza pombe.(P.T)
Alisema kabla ya kipigo hicho, Nkola alikuwa akiendesha pikipiki yake wakati akirejea nyumbani kwake na baadaye alikutana na askari hao wakamtaka awabebe kwenye pikipiki hiyo kwa nguvu kwa lengo la kuwapeleka kwenye mwalo wa kasenda ambapo kuna ghati la kuvukia ili kuingia ndani ya hifadhi hiyo.
Baada ya kukaidi amri ya askari hao, mmoja wao alipanda kwa makusudi wakati Nkola akitaka kuondoka eneo hilo, hali iliyosababisha kuyumba na kuanguka. Kitendo hicho kilichowaudhi askari hao na kuanza kumshambulia kwa kipigo.
Paulo alisema baada ya mdogo wake kuzidiwa nguvu, alilazimika kukimbilia kituo kidogo cha polisi cha Muganza ili kunusuru maisha yake, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida watu hao walimfuata mpaka kituoni hapo na kuendelea kumpiga mbele ya askari wa polisi waliokuwa zamu.
Kutokana na kipigo hicho, Nkola alijeruhiwa vibaya na baadaye kuomba PF3 kwa ajili ya matibabu kwenye zahanati ya Nyabugera iliyopo kata ya Muganza.
Hata hivyo, baada ya hali ya Nkola kuonekana kuzidi kuwa mbaya, alilazimika kwenda hospitali ya wilaya ya Chato ili kupata huduma zaidi kabla ya kukumbwa na mauti hayo usiku wa kuamkia jana.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mashaka Majige, maarufu kwa jina la Kishimba, alisema askari hao pia walikuwa wamelewa pombe ambapo walimtaka Moshi awabebe kwenye pikipiki kwa nguvu ambapo alikaidi amri hiyo.
Alisema hata baada ya merehemu kukimbilia kituo cha polisi na kuingia ndani, askari hao walimfuata na kumshambulia mbele ya askari waliokuwepo bila kuwazuia.
Diwani wa kata ya Muganza, Marco Maduka, amekiri kutokea tukio hilo na kudai kuwa askari hao walikuwa wametoka kwenye hifadhi ya kisiwa cha Rubondo na kwamba walionekana wakinywa pombe kabla ya kufanya ukatili huo.
Alidai kuwa askari hao ambao majina yao hayajafahamika mara moja, walimpiga mtu huyo ndani ya kituo cha polisi kabla ya kukumbwa na mauti.
Jeshi la polisi wilayani hapa limekiri kuwapo kwa madai hayo na uchunguzi unafanyika. Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.
NIPASHE Jumapili lilipomtafuta Ofisa doria mkuu wa hifadhi ya kisiwa cha Rubondo, aliyefahamika kwa jina moja la Chuwa ili kuzungumzia tuhuma hizo simu yake haikupatikana.
Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Pius Buchukundi, alikiri kupokelewa kwa Nkola akiwa mgonjwa lakini wakati akipatiwa matibabu alipoteza maisha.
Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa Nkola aliumia kichwa kutokana na kitu kisichojulikana kumgonga na kusababisha kupasuka baadhi ya mishipa iliyosababisha damu nyingi kuvuja eneo la jicho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI