DC alia wilaya kukosa uwanja wa ndege

MKUU wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, Mary Tesha, amesema watalii wengi wanashindwa kwenda wilayani humo kujionea jiwe la maajabu lin... thumbnail 1 summary
MKUU wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, Mary Tesha, amesema watalii wengi wanashindwa kwenda wilayani humo kujionea jiwe la maajabu linalocheza kutokana na ukosefu wa uwanja wa ndege.

Mkuu huyo wa wilaya (DC), alibainisha hayo hivi karibuni jijini Mwanza alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hizi katika maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini hapa.

Alisema kuharibika na kushindwa kutumika kwa muda mrefu uwanja wa ndege wilayani humo, unachangia kwa asilimia kubwa watalii wengi kushindwa kutembelea vivutio vilivyoko Ukerewe.

Kutokana na hali hiyo, Tesha ameiomba serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya kuujenga upya uwanja wa ndege Ukerewe.
Katika swali lake, mwandishi wa habari hizi alimuomba DC aeleze iwapo kukosekana kwa uwanja wa ndege Nansio Ukerewe ni chanzo cha watalii wengi kutokwenda kutembelea na kujionea vivutio vingi, likiwemo jiwe linalocheza.

Katika maelezo yake, Tesha alikiri kukosekana kwa uwanja wa ndege wilayani humo kunachangia taifa kukosa fedha nyingi za kigeni kwa kuwa watalii wengi kutoka nje ya nchi wanashindwa kutembelea vivutio hivyo.

Mkuu huyo wa wilaya alitaja baadhi ya maajabu ya utalii yaliyoko wilayani Ukerewe kuwa ni ghorofa la kwanza kujengwa wakati wa ukoloni katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, jiwe linalocheza na mapango mengine yaliyotumiwa na wakoloni.

Chanzo: Tanzania Daima