HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. KHAMIS KAGASHEKI (MB) KATIKA UZINDUZI VYOMBO VINAVYOUNDWA CHINI YA SHERIA YA UTALII (2008), OKTOBA 8, 2013

Mwenyekiti na Wajumbe wateule Mamlaka ya wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Suedi Kagashek... thumbnail 1 summary
Mwenyekiti na Wajumbe wateule Mamlaka ya wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Suedi Kagasheki (MB) (wapili kutoka kulia kwa waliosimama msitari wa mbele) mara baada ya kuzinduliwa rasmi katika Ukumbi wa Ngorongoro ulioko Maqkao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es salaam

• Naibu Waziri;
• Katibu Mkuu;
• Naibu Katibu Mkuu;
• Wenyeviti na Wajumbe Wateule:
Bodi ya Leseni za Biashara za Utalii Tanzania
Mamlaka ya Rufaa
Kamati ya Ushauri ya utalii
• Viongozi wa Wizara;
• Wageni Waalikwa;
• Mabibi na Mabwana

Mabibi na Mabwana,
kabla zijasema mengi zaidi, naomba binafsi nichukue fursa hii kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe walioteuliwa na kuwashukuru kwa kukubali uteuzi huu. Natumaini kwa njia moja au nyingine mnafahamu jinsi Wizara yetu ilivyo na changamoto nyingi ambazo kusema ukweli zinahitaji busara, umakini na ujasiri katika kufanya maamuzi. Hivyo ndugu zangu naelewa kazi kubwa iliyopo mbele yenu, lakini kukubali kwenu kunaonyesha jinsi gani mko tayari kushirikiana na sisi katika juhudi za kukuza uchumi wa Tanzania kupitia sekta hii muhimu ya utalii.

Kama mnavyofahamu, pamoja na usimamizi wa rasilimali za asili, jukumu kubwa lingine la Wizara ya Maliasili na Utalii ni kusimamia maendeleo ya sekta ya utalii kwa:
• Kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya utalii nchini,
• Kusajili, kutoa leseni na kudhibiti ubora wa biashara mbalimbali za utalii nchini,
• Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kamambe wa uendelezaji utalii nchini,
• Kukusanya, kutunza na kutoa taarifa na takwimu za utalii nchini,
• Kuratibu na kusimamia ubora wa mafunzo katika fani ya utalii,
• Kuhakiki, kukagua na kuweka hoteli katika daraja za ubora, na
• Kukuza utalii wa ndani.

Ndugu Wenyeviti na Wajumbe wateule,
Kama ilivyo katika uendeshaji wa vyombo mbalimbali vya Serikali, dhumuni kuu katika uwepo wa vyombo hivi vitatu yaani Bodi ya Leseni za Biashara za Utalii Tanzania, Mamlaka ya Rufaa na Kamati ya Ushauri wa Kitaalam katika Wizara hii ni kusaidia katika usimamizi, kutoa miongozo na ushauri wa kitaalam kulingana na sera na sheria. Hivyo hili ndugu zangu kama nilivyosema mwanzoni, ni hitaji muhimu katika kuimarisha utendaji na usimamizi bora wa shughuli mbalimbali ambazo tunategemea zilete faida kwa nchi nzima.

Mabibi na Mabwana,
Kwa kifupi Sekta ya Utalii ni miongoni mwa sekta zenye uwezo mkubwa wa kukuza uchumi. Mafanikio katika sekta ya utalii nchini yanaonekana wazi ambapo, takwimu zinaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la watalii walioingia nchini kutoka 770,376, mwaka 2008 hadi kufikia watalii 1, 013,317 mwaka 2012, ambalo ni ongezo la asilimia 23.98.

Aidha mapato yatokanayo na watalii hao yameongezeka kutoka dola za kimarekani Bilioni 1.2 mwaka 2008 hadi kufikia dola 1.5 mwaka 2012 na kufanya sekta hii kuongoza katika kuliingizia taifa fedha za kigeni. Mchango wa sekta katika pato la Taifa ni asilimia 17.2 na ni chanzo kikubwa cha ajira hapa nchini. Ni imani yangu kuwa, sekta hii ikipewa nafasi zaidi itasaidia kukuza uchumi wa taifa letu.

Ndugu Wenyeviti na Wajumbe wateule,
Pamoja na ukuaji huu bado tunazo changamoto mbalimbali ambazo nyingi ni mtambuka nikimaanisha kuwa zinatokana na sekta nyingine ambazo zinashamirisha sekta ya utalii. Baadhi ya changamoto hizi ni ukosefu wa maeneo maalum ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za utalii, na idadi ndogo ya huduma za malazi zenye viwango wa Kimataifa.

Ni imani yangu kuwa mtatoa suluhisho katika kukabiliana na changamoto hizi ili kuiwezesha sekta ya utalii kukua kwa kasi na juhudi za serikali kupunguza umaskini nchini. Kwa upande wetu tupo tayari na milango iko wazi wakati wote kupokea ushauri na miongozo yenu. Wizara itajitahidi kadiri iwezavyo kutimiza mahitaji mbalimbali kuwasaidia kutimiza majukumu yenu bila vikwazo. Naomba niongezee tu kuwa, tunategemea kuufanya ushirikiano huu baina na Wizara na nyinyi kuwa wa mafanikio na kukumbukwa.

Mabibi na Mabwana,
Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi hizi na Kamati,
Baada ya kusema hayo sasa naomba kutamka rasmi kuwa Bodi ya Leseni za Biashara za Utalii, Mamlaka ya Rufaa na Kamati ya Ushauri wa Kitaalam zimezinduliwa rasmi.

Nawashukuru, nawatakia kazi njema na natumaini ushirikiano mzuri kutoka kwenu.