KAMPUNI ya Ndege ya Hainan ya
China imekubali kufanya safari za ndege za moja kwa moja kutoka China hadi
Tanzania ili kukuza sekta ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.
Ahadi hiyo imetolewa leo mchana (Alhamisi,
Oktoba 24, 2013) na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la Hainan (Hainan Airlines),
Bw. Chen Feng baada ya kuombwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika
mazungumzo yao alimwomba akubali ndege za shirika lake ziwe zinatua Tanzania. Ndege
za shirika hilo zinafanya safari kati ya China na Angola kupitia anga la
Tanzania.
Waziri Mkuu ambaye yuko ziara ya
kikazi nchini hapa, moja ya eneo ambalo amekuwa anaziomba kampuni za ndege za
China ni kufikiria kufanya safari ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili
kukuza biashara pamoja na utalii pamoja na kuja kuweza katika ujenzi wa hoteli
za kitalii. Pia alisema kuna Watanzania wengi ambao wanakuja China kuchukua
bidhaa hapa China lakini wanalazimika kuunganisha safari mara tatu hadi nne
kabla hawajafika China jambo ambalo alisema linawaongezea gharama mno.
Akijibu maombi hayo ya Waziri Mkuu,
Bw. Chen alisema kutokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili, maombi
yake watayafanyia kazi na mojawapo ni hilo la kufungua safari za moja kwa moja
za ndege kutoka China kwenda Tanzania.
Lakini alishauri kuwa ili njia hiyo
iendelezwe ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuhakikisha njia hiyo inakuwa ya
kudumu kwa kuwa na abiria wengi na ikiwezekana Tanzania kiwe kitovu cha usafiri
wa anga kwa abiria wanaotoka nchi jirani wanaokwenda na kutoka China.
Alisema ili kuweza kuwa kitovu cha
usafiri wa China, ni lazima abiria kutoka nchi jirani wapate usafiri wa uhakika wa kuwafikisha katika uwanja wa
ndege wa Dar es Salaam ambako wataunganisha safari yao wakitokea katika nchi
zao.
Alisema dawa pekee ya kufanikisha
hilo ni kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la taifa ambalo litashirikiana na
Hainan kuhakikisha safari hizo zinakuwa zenye tija na faida kwa kuwafikisha
abiria hao kwenye kitovu cha usafiri wa kuunganisha kwenda China.
Pia alisema ili Dar es Salaam iwe
kitovu cha usafiri wa anga ni lazima kuwe na uwanja wa ndege mkubwa na wa
kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa wenye kukidhi mahitaji ya kimataifa
(international standards). Alisema kampuni yake iko tayari kuja nchini
kushiriki katika kupanua uwanja wa ndege utakaotumiwa na shirika hilo ili uwe
wa kisasa.
“Tuna wataaalam waliobobea
katika eneo hilo, maana sisi wenyewe tu tunamiliki viwanja vya ndege vipatavyo
16, hivyo mkitushirikisha mtakuwa na uwanja ambao kila aina ya ndege inaweza
kutua,” alisema mwenyekiti huyo wa Hainan Airlines.
Bw. Chen pia alisema suala la
utalii ni la muhimu zaidi kwani anatambua kuwa Tanzania kuna vivutio vingi kama
fukwe za bahari, mbuga za wanyama na vingine vingi na akaongeza kuwa shirika
lake lina uzoefu wa biashara ya utalii kwani lina kampuni zinazofanya kazi
ndani ya China na Hong Kong. “Tunaweza kusaidia kuwaleta Wachina waje kutalii
Tanzania,” alisema Bw. Chen na kusisitiza kuwa wataangalia katika kuwekeza
kwenye hoteli karibu na hifadhi za taifa.
Hainan ni moja ya mashirika makubwa
ya ndege duniani. Ina ndege 470 na imeajiri wafanyakazi wapatao 1,000. Shirika
hilo pia lina hoteli 500 za kitalii duniani na lina viwanja vya ndege vipatavyo
16 vikiwemo vitatu vya kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimweleza
mwenyekiti huyo kuwa Tanzania inafanya juhudi za kujikomboa kiuchumi; lakini
bado inahitaji msaada wa China hasa katika masuala ya usafiri wa anga ili iweze
kupiga hatua kutoka hapo ilipo.
Alisema Tanzania kuna shirika la
ndege lakini liko taabani licha ya kuwa lina njia nyingi na akatumia muda huo
kumwomba mwenyekiti huyo wa Hainan kufikiria pia namna ya kuweza kufufua ATC
ili iweze kufanya kazi pamoja na Hainan.
“Ndio maana tunawakaribisha nyinyi
Hainan ni shirika kubwa ambalo naamini linaweza kuisaidia Tanzania katika eneo
hilo la usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanya
safari za moja kwa moja hadi Tanzania; lakini pia na kuangalia namna ya
kulifufua shirika la ndege la Tanzania (ATC),” alisema Waziri Mkuu.
Alimwomba Bw. Chen aangalie
uwezekano kuja kujenga hoteli za kitalii karibu na viwanja vya ndege. “Iweje
hoteli za utalii katika nchi yetu zijengwe na wafanyabiashara wa nchi za
magharibi tu wakati na nyinyi mna uwezo wa kufanya vizuri zaidi hata kuliko
wao? Alihoji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 24, 2013