MSIGWA AMSHINIKIZA KIKWETE KUWATAJA MAJANGILI.

Na Denis Mlowe,Iringa. MBUNGE wa Iringa Mjini na Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa amemtaka Rais w... thumbnail 1 summary
Na Denis Mlowe,Iringa.

MBUNGE wa Iringa Mjini na Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa amemtaka Rais wa Jakaya Mrisho Kikwete kuwataja wahusika wote wa ujangili wanaojulikana na kuendeleza Ujangiri katika Ardhi ya Tanzania.
Msigwa amesema Tanzania ni moja ya nchi 8 duniani ambazo ziko katika kiwango cha juu sana katika biashara haramu ya ujangili na kati ya kilo 800 zinazokamatwa duniani asilimia 37 za meno ya Tembo zinatokea Tanzania na hali ya ujangili kwa sasa ni ongezeko la asilimia 57 ikiwa kwa siku wanauwa tembo 63.
Hayo amezungumza Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa wakati wa maandamano ya siku ya Ujangili yaliyodhaminiwa na shirika la Wild life Connection na kufanyika katika viwanja vya Mwembetogwa jana Msigwa ambaye alikuwa alisema serikali ya Kikwete inawatambua majangili wote wa meno ya Tembo na kushangaa inakuwaje inakuwa vigumu kuweza kuwataja ingawa majina yao wameyakalia tu na kuitaka Serikali kutimiza wajibu wake kwa kuwafikisha majangili na wafanyabiashara haramu wa wanyamapori katika vyombo vya dola na watendewe ipasavyo kwa mujibu wa Sheria
“Namshinikiza Rais awataje majangili wote lakini nashangaa hakuna kauli hata moja ya kuwataja majangili hao na wanaoendelea kuwateketeza tembo kila mwaka hivyo ni shinikizo kwake aweze kuwataja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria” alisema Msigwa
Alisema suala la biashara haramu ya wanyamapori nchini limeendelea kukua kwa kasi ya ajabu huku Serikali ikionesha wazi kushindwa kudhibiti suala hili na hivyo kutoa mwanya kwa majangili kuendelea kuteketeza wanyamapori huku baadhi ya viumbe hai vikiwa hatarini kutoweka kabisa katika ramani ya Taifa letu hasa Tembo ambao kila siku wanauwa 63.
Msigwa alisema mkutano mkuu ulifanyika Bangkok ulikuwa kwa lengo la kuziwekea vikwazo vya biashara nchi za Kenya na Tanzania swali la kujiuliza kwa nini kama taifa lifikie kuwekewa vikwazo vya biashara kwa kushindwa kutekeleza wajibu wetu na kulinda maslahi ya watu wachache?
“Ukiangalia takwimu Tanzania na Kenya ni nchi 8 duniani katika biashara ya tembo, Taifa letu limeendelea kuwa katika ramani ya dunia kwa kuwa moja ya nchi vinara zinazotia doa hasa kwa biashara haramu ya wanyamapori, hali inayohatarisha maisha ya baadhi ya viumbe hai je kwa nini serikali ya Kikwete isiwataje majangili hao? Alisema Msigwa kwa kuhoji
Aidha Msigwa alisema jambo moja la msingi wananchi wote tuungane katika kuweza kupambana na majangili walioko katika maeneo yetu na kuwafichua bila kuogopa kwa lengo la kuwanusuru tembo ambao wanateketea kila siku duniani hasa katika mbuga zetu.
“Ningependa kulizungumza na kusisitiza hapa leo ni juu ya wajibu wa kila Mtanzania katika kuhakikisha kuwa tunaungana kwa pamoja katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori na watajeni wanahusika na biashara ya ujangili ambao tunaishi nao kila siku huwezi kukuta mchina anakamatwa katika mbuga zetu hivyo kuna mnyoror mkubwa wa ujangili tuukate kwa kuwafichua” alisema Msigwa
Mara kadhaa pia Serikali imeendelea kukiri kuwa mtandao huu unawahusisha Wafanyabiashara wakubwa, Wanausalama, Wabunge, Wanasiasa na watu wenye dhamana ya uongozi katika taifa letu. Serikali imeendelea kutoa matamko kuwa itawataja wahusika wa biashara haramu dhidi ya wanyamapori na kuwachukulia hatua lakini cha kushangaza, mara zote hakuna hatua yoyote inayochukuliwa hadi sasa kwa kuwataja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Chanzo: Michuzi