Pinda aonya Watanzania wanaouza ‘passport’ zao China

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Watanzania waishio Guanzhou nchini China, baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ... thumbnail 1 summary
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Watanzania waishio Guanzhou nchini China, baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara ya kikazi nchini humo juzi. Picha na PMO  
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda amewaonya baadhi ya Watanzania wanaokuja katika Jiji la Guangzhou nchini China kwa ajili ya kununua bidhaa mbalimbali,waache kuuza hati zao za kusafiria kwa raia wa nchi nyingine kama njia ya kujiongeza kipato. Alitoa onyo hilo jana usiku wakati akizungumza na Watanzania wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika Jiji la Guangzhou, jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China.
Alisema wengi wa wafanyabiashara hao wanapouza pasipoti zao wanasingizia kuwa zimepotea ndio maana kuna malalamiko mengi kutoka kwa Watanzania wanaofika katika jimbo hilo kudai wanaibiwa hati zao za kusafiria wakati sio kweli.
Wakati wa mazungumzo hayo, mmoja wa Watanzania aliyejitambulisha kwa jina la Ambrose Lugai alisema changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania waishio katika jimbo hilo na moja ya tatizo hilo ni kuibiwa kwa hati za kusafiria za Watanzania.
Lugai alisema tatizo la wafanyabiashara wengi kupoteza pasipoti limekuwa sugu na kila siku linaongezeka na cha ajabu linawatokea wafanyabiashara wa kutoka Tanzania tu.
Alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kuzungumza na Serikali ya jimbo hilo ili Watanzania wawe wanaacha pasipoti hotelini wakati wanapoenda mitaani, badala yake wapewe karatasi nyingine ya kuwatambulisha mitaani.
Akijibu hoja hiyo ya Lugai, Waziri Mkuu alisema suala hilo linamshangaza kwamba inakuwaje hati za wafanyabiashara wa Tanzania tu ndio zinaibiwa wakati wafanyabiashara wanaofika kwenye jimbo hilo ni wengi
Chanzo: Mwananchi