Sendeka awa mbogo operesheni ujangili, Aonya isitumike kupora ardhi ya vijiji

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), amekuja juu na kutaka operesheni maa... thumbnail 1 summary
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), amekuja juu na kutaka operesheni maalum ya kupambana na ujangili na watu waliovamia maeneo ya hifadhi isitumike kama kichaka cha kupora ardhi ya wakazi wa Kijiji cha Kimotorok na kuifanya kuwa sehemu ya Hifadhi ya Pori la Hifadhi la Mkungunero.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chake na viongozi wa kijiji hicho, wazee pamoja na malaigwanani waliomwangukia ili atafute suluhu ya mgogoro huo.

“Naunga mkono operesheni hii iliyoanzishwa na serikali kupambana na majangili na watu waliovamia maeneo ya hifadhi, lakini operesheni hii isitumike kupora ardhi halali ya vijiji.

“Natambua Rais anao uwezo wa kisheria wa kutwaa eneo lolote la ardhi nchini kwa manufaa ya umma, lakini hadi sasa serikali ya awamu ya tatu na hii ya awamu ya nne hazijatwaa ardhi yoyote ya Kijiji cha Kimotorok na kuifanya kuwa sehemu ya Pori la Hifadhi la Mkungunero.

“Naomba na ni vema kila upande ukaacha kuiingilia upande mwingine,” alisema na kuongeza, “Jumapili nitafanya mkutano mkubwa na wanakijiji kutoa ufafanuzi wa mgogoro huo.”

Alisema Pori la Hifadhi la Mkungunero lilianzishwa mwaka 1996 na Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma wakati Kijiji cha Kimotorok kilichopo wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara na vitongoji vyake kilianzishwa na kupewa hati halali na Wizara ya Ardhi mwaka 1992.

Hata hivyo, alisema kumekuwapo na mwingiliano wa mipaka kati ya Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara katika eneo la Kijiji cha Kimotorok, hali ambayo imezusha vurugu kwa wakazi wa eneo hilo wa jamii ya wafugaji ya Wamasai na Wabarbaig baada ya askari wa wanyamapori kuingia maeneo ya makazi ya watu na kuchoma maboma yao.

“Tayari tumewasilisha serikalini malalamiko yetu kwamba kila upande (Mkungunero na Kimotorok) ubaki kama ulivyo bila kubughudhiwa wala kusumbuliwa mpaka tatizo hilo la mpaka litakapotatuliwa.”

Mamia ya wakazi wa Kijiji cha Kimotorok wameanza kuchomewa moto makazi yao na askari wa wanyamapori katika operesheni maalum wanayodai ya kuwaondoa katika eneo la Pori la Hifadhi la Mkungunero.

Askari wa hifadhi hiyo walithibitisha kuanza kwa zoezi hilo linalotekelezwa maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba mosi hadi 18, hatua ambayo imemfanya meneja wa ofisi hiyo, Johnson Msellah, kuungana na askari wenzake kuifanikisha.

Licha ya kuanza kwa operesheni hiyo, vitendo vya uchomaji moto wa maboma ya wafugaji yakiwa na chakula na mifugo yao kwa madai ya kuvamia pori hilo vilikuwa vikiendelea, huku waathirika wakiachwa bila msaada wowote wa chakula, mavazi au malazi.
Hadi sasa zaidi ya maboma 250 yamekwishachomwa kuanzia mapema Septemba kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, huku wakazi wengine wakidai kupigwa na kuumizwa sehemu mbalimbali za mwili.

Mama mmoja mkazi wa Kitongoji cha Kisandoko, ambaye jina lake limehifadhiwa alilalamika mbele ya kikao cha wakazi wa eneo hilo kuwa alibakwa Septemba 30 mwaka huu na watu wawili waliokuja pamoja na wenzao kuchoma moto maboma yao.

Mwenyekiti wa Wafugaji wa Kitongoji cha Kisondoko, Bura Araji Faraja alidai kumekuwa na vitendo vingi vya ubakaji kwa wasichana katika eneo hilo linalodaiwa kuhusishwa kufanywa na watu wanaokwenda kuchoma moto maboma yao.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Daniel ole Melau, aliwaambia wakazi wake kwamba hawapo tayari kuhama katika eneo lao na kwamba wapo tayari kufa katika eneo lao.

“Sasa hivi manyanyaso yamezidi, hatupo tayari kutoka na hata wale waliochomewa moto maboma yao bado wapo kwenye maeneo yao,” alisema na kudai sheria haina sababu ya kuwaondoa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI