Sheria, sera ya utalii kufanyiwa marekebisho

SERIKALI imesema iko mbioni kuzifanyia marekebisho sheria, sera na kanuni zinazohusu sekta ya utalii ili ziendane na wakati. Waziri wa ... thumbnail 1 summary
SERIKALI imesema iko mbioni kuzifanyia marekebisho sheria, sera na kanuni zinazohusu sekta ya utalii ili ziendane na wakati.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge pamoja na wawakilishi wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato) kwenye semina ya kujadili changamoto na faida ya sekta ya utalii.

Alisema sheria, sera na kanuni zinazoongoza sekta ya utalii zilizopo zimepitwa na wakati na zimekuwa zikichangia kudorora kwa sekta hiyo ikiwemo kuwavutia wawekezaji.

Alisema wawekezaji wanapofika nchini hukatishwa tamaa na milolongo ya kupata vibali husika, hivyo huamua kukimbilia nchi jirani ambazo sasa zinapiga hatua nzuri katika utalii.

“Wenzetu wa Rwanda mwekezaji anapotaka kuwekeza katika sekta hiyo hupewa vibali kwa siku zisizopungua saba, sisi hapa kwetu huchukua zaidi ya mwaka mmoja, urasimu huu ndiyo unaotumaliza,” alisema.

Katika semina hiyo, Tato wameiomba serikali iweke ajenda ya utalii kuanzia kwenye serikali za mitaa ili kukuza sekta hiyo, mapato ya taifa na ajira.


Mwenyekiti wa Tato, Wilbard Chambulo, alisema sekta ya utalii ina uwezo wa kuliingizia taifa fedha nyingi iwapo serikali itashirikiana na sekta binafsi inayojishughuli na utalii.

Chanzo: Tanzania Daima