Tido: Sekta ya habari inaweza kukuza utalii

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Limited,Tido Mhando akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo mkoa wa Arusha jana,kulia n... thumbnail 1 summary
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Limited,Tido Mhando akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo mkoa wa Arusha jana,kulia ni Meneja Mkuu wa Usambazaji,Emmanuel Kanagisa.Picha na Filbert Rweyemamu 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Tido Mhando amesema tasnia ya habari ikitumika vyema inaweza kutoa mchango mkubwa kuinua sekta ya utalii kutokana na kuaminiwa na kufikia watu wengi kwa wakati mmoja.
Mhando alisema hayo jana akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari katika kuinua sekta ya utalii Afrika wakati wa mkutano wa Umoja wa Vyombo vya Utangazaji Kusini mwa Afrika (SABA).
Kwa mujibu wa Mhando , umuhimu wa vyombo vya habari unachagizwa na maendeleo na matumizi ya sayansi na teknolojia inayorahisisha utengenezaji na urushaji wa matangazo yenye ubora.
Naye Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungi aliwataka watengenezaji wa vipindi na filamu kutoka nchi za Kusini mwa Afrika kuandaa, kutengeneza na kurusha vipindi vinavyoonyesha na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo, ili kukuza sekta ya utalii.
Alisema muda umefika kwa filamu na matangazo yote yanayoelezea vivutio vya utalii Afrika kuandaliwa, kurekodiwa na kurushwa na Waafrika wenyewe.
Awali akifungua Mkutano Mkuu wa 21 wa SABA, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal alivitaka vyombo vya SADC kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi zao, badala ya kuacha kazi hiyo kufanywa na vyombo vya habari vya nje.
Dk Bilal alivitaka vyombo ya utangazaji kutumia kuaminika kwao kwa jamii kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na ulinzi wa maliasili.
 Chanzo: Mwananchi