Watanzania waunga mkono Uganda kukuza Kiswahili

KUTOKANA na nchi ya Uganda kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kwenye  shule za msingi hadi vyuoni, baadhi ya wataalamu wa  lugha hiyo wamese... thumbnail 1 summary
KUTOKANA na nchi ya Uganda kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kwenye  shule za msingi hadi vyuoni, baadhi ya wataalamu wa  lugha hiyo wamesema ni ushindi kwa Tanzania.
Akizungumza  na Tanzania Daima jana, mtaalamu wa Kiswahili aliyewahi kuwa Ofisa Uhusiano wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Mohammed  Mwinyi, alisema anaunga mkono jitihada za  Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika kuhakikisha Kiswahili kinakua na kutumika katika nchi mbalimbali duniani.
Alisema awali Watanzania walikuwa wanatembea wakati wenzetu wanakimbia,  ndiyo maana Uganda ilikipa kipaumbele Kiswahili tangu wakati wa Iddi Amini.
Alieleza kutokana na Museveni kuwa miongoni mwa viongozi waliosoma hapa nchini, ndiyo sababau iliyomfanya atambue nafasi ya Kiswahili hadi kuidhinisha kutumika  nchini kwake ingawa baadhi ya  Waganda wamekuwa wakihofia lugha hiyo.
"Ninaunga mkono jithada za Rais Museveni, kwani kutokana na hili inaonyesha jinsi Kiswahili kinavyoanza kutawala, lakini pia inafaa tutambue kwamba kuna utaratibu katika kufundisha lugha ya asili na ya kigeni hivyo ieleweke lugha ya Kiswahili katika nchi ya Uganda  itaanza kufundishwa kama lugha ya kigeni,” alieleza.
Naye Eva Joseph, mkazi wa Ukonga, alisema kutokana na serikali ya Uganda kufikia uamuzi wa kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia ni dhahiri harakati za kukuza Kiswahili zimefanikiwa na kinachotakiwa ni uhamisishaji zaidi, ili lugha hiyo iweze kutumika duniani kote  kama zilivyo lugha nyingine.

Chanzo: Tanzania Daima