Waziri Mkuu ainadi Tanzania ughaivuni, Azialika kampuni za Kichina kuja kuwekeza Tanzania

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaeleza washiriki wa Maonesho 14 ya Kimataifa ya China Magharibi kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani na ya k... thumbnail 1 summary

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaeleza washiriki wa Maonesho 14 ya Kimataifa ya China Magharibi kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na vituo vingi vya utalii na akawataka waanze kumininika kwa wingi kuja nchini kutalii.

Ametoa mwaliko huo leo asubuhi (Jumatano, Oktoba 23, 2013) wakati akihutubia kwenye maonesho hayo ya kimataifa yanayojulikana kama 14th Western China International Fair yaliyoanza leo jijini Chengdu kwenye jimbo la Sichuan, China na kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa mataifa 11 waliopata fursa ya kuhutubia maonesho hayo makubwa ya kimataifa, aliziomba kampuni za China kuja nchini kuwekeza kwa kujenga viwanda vingi vya nguo zinazotokana na zao la pamba.

Alitumia fursa hiyo pia kuinadi Tanzania kuwa ni nchi yenye ardhi kubwa tena yenye rutuba ambayo inafaa kwa kilimo, na kuzisihi kampuni za Kichina ambazo zinataka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo zije nchini kwa ajili ya kulima kilimo cha mashamba makubwa ya biashara.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Pinda aliwaambia wawakilishi wa kampuni mbalimbali za kimataifa zinazoshiriki kwenye maonyesho hayo kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima pamba kwa wingi wakati China ni taifa ambalo limebobea kwa viwanda.

“Sisi tuna pamba na ninyi mna viwanda, nawaomba mje nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nguo kwani malighafi ipo ya kutosha,” alisema. Maonesho hayo yanashirikisha kampuni 4,000 kutoka nchi 72 mbalimbali ulimwenguni na majimbo mengine ya hapa China.

Ufunguzi wa maonesho hayo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi saba, mawaziri wakuu wanne mbalimbali akiwemo Pinda, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 25, wakuu wa mashirika ya kimataifa wapatao tisa na mabalozi wanane wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini China.

Gazeti la Serikali la China Daily limeyaelezea maonesho hayo kuwa ni makubwa kufanyika katika jimbo hilo na inatarajiwa kuwa mikataba yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 82 itasainiwa na kampuni mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu utalii, Waziri mkuu pia alitumia fursa hiyo ya kuhutubia maonesho hayo makubwa ya kimataifa kuinadi Tanzania katika sekta ya utalii na kuwaeleza wafanyabiashara hao Tanzania ni nchi ya pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki yenye vivutio vingi vya utalii vikiwemo vitatu vilivyoko kwenye maajabu saba ya Afrika.

“Kati ya maajabu saba mapya ya asili barani Afrika, yaliyotangazwa Februari, mwaka huu, maajabu matatu yako nchini mwetu ambayo ni mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti na Bonde la Ngorongoro,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na vivutio hivyo lukuki lakini bado idadi ya watalii wanaofika nchini kutoka China haijawa ya kuridhisha.

Alisema licha ya maajabu hayo matatu, lakini pia kuna hifadhi nyingine za wanyama, hifadhi za mambo ya kale na kisiwa maarufu cha Zanzibar. Alisema hata takwimu za kimataifa zinaitaja Tanzania kama nchi ya pili duniani yenye vivutio vingi kuliko nchi zingine ikiifuatia Brazil ambayo inaongoza kwa vivutioa duniani.

“Pamoja na vivutio hivi lakini idadi ya watalii kutoka China bado ni ndogo, sasa nawaambieni njooni kwetu mjionee maajabu ya dunia,” alisema. Mkutano huo ulihutubiwa na viongozi saba kutoka mataifa mbalimbali ambao wote walieleza kunufaika na uhusiano wa kibiashara na China.

Viongozi hao ni magavana wakuu ambao ni Quentin Bryce wa Australia na David Johnston wa Canada. Wengine ni Rais wa Macedonia, Gjorge Ivanov, Waziri Mkuu wa Mongolia, N. Altanhhuyag, Naibu Waziri Mkuu wa Berarus, Analy Tozik, Waziri Mkuu wa zamani wa Ufaransa, Jean-Pierre Raffarin na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Jan Mattassons.

Kwa upande wa Ardhi, Waziri Mkuu alisema Tanzania bado ina ardhi kubwa ambayo haijaguswa kwa kilimo, hivyo kampuni za China na zingine za mataifa mengine yanayoshiriki kwenye maonesho hayo kuja kuwekeza nchini hasa katika sekta ya kilimo.

Waziri Mkuu alisema, anatoa ukaribisho kwa kampuni hizo kwa vile Tanzania sera yake ya kibiashara ni ya kushirikiana na mataifa mengine na kukaribisha wawekezaji wa nje na wa ndani kuja kuwekeza nchini katika maeneo ambayo wanaona inafaa kufanya hivyo.

“Maonesho haya ni ishara kwamba China inatoa fursa mbalimbali kwa watu wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara pamoja, na sisi tuna sera ya namna hii hivyo tunawakaribisheni kuja nchini kuwekeza kwa wingi,” alisema Pinda.

Alisisitiza pia kuwa wawekezaji hao wanaweza kuja kuwekeza katika sekta kama ya gesi ambayo imegundulika hivi karibuni au kwenye makaa ya mawe na hata kwenye madini ya chuma. “Ndiyo maana nasema kampuni za China njooni muwekeze kwetu hasa katika sekta hizi.”

Waziri mkuu ambaye alistaajabishwa na maonesho hayo ya kijimbo ambayo ni makubwa na yenye mvuto kwa kampuni kubwa duniani, alitoa mwito kwa kampuni za China kuja kushiriki kwenye maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya mwakani ambayo yatafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 8, 2014.

Waziri mkuu jana ameondoka Chengdu na kueleka katika jimbo la Guangzhou ambako atamalizia ziara yake ya sikua tisa ya kikazi.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim.

Pia amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega), Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, Bibi Julieth Kairuki na viongozi wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfrey Simbeye.