JELA MIAKA 70 KWA KUKAMATWA NA MENO YA TEMBO

Na Walter Mguluchuma Mpanda Katavi Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imewahukumu watu w... thumbnail 1 summary
Na Walter Mguluchuma
Mpanda Katavi
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imewahukumu watu watatu kutumikia kifungo cha  jumla ya miaka sabini jela bada ya kupatikana na hatia  ya kukamatwa na meno ya tembo manne yenye thamani ya shilingi milioni 45

Hukumu hiyo ilitolewa hapo jana na Hakimu Mkazi  mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa baada ya kulidhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka na upande wa utetezi 

Waliohukumiwa kifungo hicho ni Gwabi Mayala  (39)  mkazi wa kijiji cha Majimoto  Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi  ambae alikuwa mshitakiwa wa kwanza amehukumiwa kifungo cha miaka 30 na kulipa fidia ya shilingi milioni 45 

Washitakiwa wengine waliohukumiwa ni Mashaka Mabanga (33)  Mkazi wa Sumbawanga  Mkoa wa Rukwa  na Adamu Kalinzi (30) Mkazi wa Kijiji cha majimoto Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi  wamehukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka ishirini jela 

Awali katika kesi hiyo ilidaiwa na mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi  Fadhili Mwandoloma kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo hapo Oktoba 10  mwaka huu  majira ya saa nne usiku katika Kijiji cha Majimoto Wilayani Mlele 

Wanadaiwa siku hiyo ya tukio  washitakiwa walikamatwa wakiwa na meno manne ya Temboyenye uzito wa kilo kumi na sita yenye thamani ya shilingi milioni 45 wakiwa katika harakati ya kuyauz

Mwanasheria huyo wa Serikali aliiambia mahakama kuwa Mshitakiwa wa kwanza  Gwabi  Mayala  ndiye aliyekuwa mwenye meno hayo ya Tembo  na aliwashirikisha wenzake hao wawili kwa ajiri ya kumtafutia wateja ambao wangeyanunua  meno hayo ya Tembo 

Aliiambia mahakama baada ya washitakiwa hao kukamatwa na Askari wa Hifadhi ya wanyama pori ya Katavi walioshirikiana na polisi  washitakiwa walipofikishwa polisi mshitakiwa wa pili na watatu walikiri kuhusika na meno hayo ya tembo na kudai kuwa  meno hayo ni ya mshitakiwa wa kwanza Gwabi  Mayala 

Hakimu mkazi mfawidhi Chiganga  baada ya kusikiliza mwenendo mzima wa kesi hiyo  aliiambi mahakama kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo wa pande mbili za mashitaka na utetezi mahakama imewaona washitakiwa wote watatu wanahatia hivyo kabla ya mahakama haija towa adhabu inatowa nafasi kwa washitakiwa kujitete

Katika utetezi  washitakiwa Mashaka na Adamu walikiri kukamatwa na meno hayo ya Tembo lakini walidaikuwa meno hayo ya Tembo yalikuwa ni ya mshitakiwa wa kwanza  Gwabi Mayala ambae alikuwa amewaomba wamtafutie wateja wa kuyanunua  kwa upande wake mshitakiwa Gwabi aliiomba mahakama isikubaliane na maelezo ya washitakiwa wenzake kuwa meno hayo yalikuwa sio ya kwake 

Hakimu Chiganga  alieleza mahakama kuwa washitakiwa wamevunja sheria ya kifungu namba 86 (1) (2) cha sheria ya huifadhi  ya mwaka 2009 na kifungu namba 57 na 60 ya sheria ya kuhujumu uchumi  sura ya 200 ya mwaka 2002 hivyo mahakama imetowa adhabu kwa mshitakiwa wa kwanza Gwabi Mayala kutumikia kifungo cha miaka 30 jela la kulipa fidia ya shilingi milioni 45 ambayo ni thamani ya meno hayo ya Tembo 

Pia washitakiwa  Mashaka Mabanga  na Adamu  Kalinzi  wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja  baada ya kupatikana na hatia ya kushirikiana na mshitakiwa wa kwanza katika biashara ya kumtafutia wateja wa kununua meno ya Tembo