Kwa undani: Kontena lenye magunia 95 yaliyosheheni meno ya tembo lakamatwa Zanzibar

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa (kushoto), akieleza kwa Waziri wa Utalii na Maliasili, Khamis Kagasheki na Waziri w... thumbnail 1 summary
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa (kushoto), akieleza kwa Waziri wa Utalii na Maliasili, Khamis Kagasheki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Omar Kheir juu ya meno ya

Magunia 95 ya meno ya ndovu ambayo thamani wala idadi yake haijajulikana, yamekamatwa katika bandari ya Zanzibar yakiwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.
Magunia hayo yalikuwamo ndani ya kontena lenye namba PCIU 8576190  lililofikishwa jana bandarini hapo majira ya saa 9:00 alasiri.

Akizungumza na waandishi wa habari bandarini mjini Unguja jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema inasikitisha kuona rasilimali za taifa zinateketezwa hivyo serikali haitovumilia mtu yeyote atakayehujumu rasilimali hizo. 

Alisema ana imani kuwa magunia hayo yanatokea Tanzania Bara kwa kuwa Zanzibar haina msitu wa hifadhi yenye wanyama wakubwa kama ndovu.  Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Zanzibar hawawezi kulikwepa tatizo hilo kwa kuwa wao ndiyo wanaopokea ushuru wa mizigo inayoingia visiwani humo.

 Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema jeshi hilo linawashikilia watu wawili ambao hakuwataja majina lakini mmoja kati ya hao ni wakala wa mizigo bandarini hapo.  Alisema haijajulikana mmiliki halali wa mzigo huo wala sehemu unapotoka na ulikokuwa usafirishwe.

Aliwataka wananchi hususan wafanyabiashara kufuata sheria na taratibu za nchi bila ya kushurutishwa huku akisema kuwa thamani ya mzigo huo haijajulikana. Alisema bado wanaendelea na uchunguzi ili kujua wahusika wa tukio hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Omar Kheir, alisema uhujumu wa uchumi kupitia maliasili ni kitendo kibaya hivyo serikali haitovumilia vitendo hivyo.
CHANZO: NIPASHE