Mtoto anusurika kuliwa na fisi

MTOTO Agnes Mtani (6), mkazi wa Kijiji cha Namarebe, Tarafa ya Nansimo, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara amenusurika kuliwa na fisi ba... thumbnail 1 summary
MTOTO Agnes Mtani (6), mkazi wa Kijiji cha Namarebe, Tarafa ya Nansimo, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara amenusurika kuliwa na fisi baada ya kuvamiwa na mnyama huyo kisha kuokolewa na wasamaria wema.
Akizungumza na Tanzania Daima jana akiwa njiani kumpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, babu wa mtoto huyo, Mnubhi Chiremeji, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12,30 jioni katika kijiji hicho.
Kwa mjibu wa Mnubhi, mtoto huyo aliondoka nyumbani kwao akiwa na dada yake aitwaye Mariamu Mtani kwa ajili ya kwenda kuzoa udaga ulioanikwa mwambani, mbali kidogo na nyumba yao.
Alisema wakiwa wanatembea kuelekea eneo walikokuwa wameanika udaga huo, ghafla alitokea fisi ambaye alimnyakua mtoto huyo na kukimbia naye.
“Baada ya dada yake kuona hivyo alipiga kelele za kuomba msaada na kwa bahati nzuri kulikuwa na mwananchi mmoja wa kijiji hicho alikuwa  jirani, ndipo alipoanza kumfukuza fisi huyo huku pia  akipiga kelele na hatimaye alimdondosha chini, hapo ikawa pona yake,” alisema babu huyo.
Alifafanua kuwa baada ya fisi kumdondosha mtoto huyo chini, wananchi wengine walifika na kumkuta akiwa na majeraha usoni, kichwani hadi begani.
Aliongeza kuwa walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika Kituo cha Afya Kibara na kupatiwa matibabu ya awali na baadaye kuhamishiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi.
Katika siku za hivi karibuni kumezuka wanyama aina ya fisi katika baadhi ya vijiji vya tarafa hiyo ambao wamekuwa tishio kwa maisha ya wananchi na mifugo.
 
Chanzo: Tanzania Daima