Mzee wa Upako afanya maombi kulinda wanyama

MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC), Ubungo-Kibangu, Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’, amelazimika kufanya maombezi kwa ajili ya kulinda ... thumbnail 1 summary
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC), Ubungo-Kibangu, Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’, amelazimika kufanya maombezi kwa ajili ya kulinda wanyama  kutokana na kukithiri kwa ujangili wa kuuawa kwa tembo.
Akizungumza katika ibada mojawapo ya Jumapili, Mchungaji Lusekelo alikemea vitendo hivyo  kushamiri miongoni mwa jamii.
Alisema ni muhimu wanyama wakalindwa kwa kuwa  ni rasilimali inayokuza uchumi wa nchi na kutaka waumini wake kufanya maombi mafupi ya kuombea suala hilo.
“Hatuwezi kukubali kuona wanyama kama tembo wanatokomea ni lazima tuliombee jambo hili, la sivyo hata vizazi vyetu vitashindwa kujua aina ya wanyama kwa sababu ya watu wachache kuwa na uroho wa fedha,” alisema.
Mchungaji huyo alisimama kwa muda akiombea suala hilo pamoja na waumini wake na kumuomba Mungu afanye ulinzi juu ya rasilimali hiyo.
Lusekelo alisema suala la ujangili lisipodhibitiwa kuna uwezekano wa wanyama kwisha na hata kuwa historia ya taifa kuwa na wanyama kama tembo.
“Hili suala si dogo kama tunavyofikiri, ni muhimu kuomba ulinzi wa Kimungu ili yeye aliyetubariki juu ya suala hilo aendelee kuwapa ulinzi wanyama hao,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima