WATU watatu wakiwemo waliokuwa maaskari wa Jeshi la Polisi wilayani
Serengeti katika mkoa wa Mara jana walifikishwa katika mahakama ya
wilaya ya Bunda kujibu mashtaka ya kukutwa na jino moja la tembo, lenye
thamani ya sh milioni 3, kinyume cha sheria.
Waliofikishwa katika mahakama hiyo iliyokuwa chini ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa wilaya hiyo, Safina Semfukwe, ni John Sigita Masese (25)
ambaye ni mkulima na mkazi wa eneo la Bomani mjini Mugumu, Sixberth
Amos (35) na Isaac John Ackley (43) ambao wote walikuwa ni maaskari wa jeshi la polisi.
Awali ilidaiwa na mwanasheria wa hifadhi za taifa Serengeti (SENAPA),
Emmanuel Zomba, kuwa Oktoba 25 mwaka huu, huko katika eneo la maktaba
mjini Mugumu washtakiwa wote kwa pamoja walikamatwa na askari wa idara
ya wanyamapori wakiwa na jino moja la tembo lenye thamani tajwa na
walikuwa wakilitafutia mteja.
Mwanasheria huyo aliiambia mahakama kuwa baada ya kukamatwa washtakiwa kwa pamoja walifikishwa katika
kituo kikuu cha polisi cha mjini Mugumu ambapo maofisa hao wa polisi
walishtakiwa kijeshi na kukutwa na hatia iliyosababisha wafukuzwe kazi
mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo kushtakiwa katika mahakama za kiserikali.
Mbali na shtaka hilo, pia mshtakiwa Isaac John Ackley
alikutwa na risasi moja ya bunduki ya SMG na nyingine tano
zinazotumika kuwindia wanyama pamoja na nyama ya aina ya nyumbu, yenye thamani ya sh 1,040,000.
Washtakiwa kwa pamoja wamekana mashtaka na wako nje kwa dhamana hadi
Novemba 18 mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.