TANAPA YATENGA MAENEO 34 YA UWEKEZAJI KWA AJILI YA KUINUA UTALII HIFADHI ZA KUSINI NA MAGHARIBI

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetenga maeneo 34 kwa ajili ya uwekezaji katika huduma za malazi kwa wageni wanaotembelea Hifadhi ... thumbnail 1 summary
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetenga maeneo 34 kwa ajili ya uwekezaji katika huduma za malazi kwa wageni wanaotembelea Hifadhi za Kusini na Magharibi mwa nchi kwa ajili ya utalii.

Maeneo haya ya uwekezaji ambayo yatahusisha ujenzi wa loji na kambi za kudumu za wageni yatawezesha kuongezeka kwa vitanda 1,790 vitakavyowezesha kuongezeka kwa uwezo wa shirika kuhudumia watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Maeneo haya 34 yaliyotengwa mahsusi kwa ajili ya kupanua wigo wa huduma za malazi katika hifadhi, yanapatikana katika Hifadhi za Kilimanjaro; Katavi; Mikumi; Mkomazi; Ruaha; Saadani; Tarangire; Rubondo na Kitulo. Kipaumbele kwenye uwekezaji huu umewekwa kwenye Hifadhi za Kusini na Magharibi ya nchi, ambazo zina uhaba mkubwa wa malazi na kusababisha idadi ndogo ya watalii. 

Uamuzi huu wa TANAPA wa kutenga maeneo mapya ya uwekezaji umezingatia ukuaji wa sekta ya utalii nchini ambapo karibu asilimia 75 ya wageni wanaofika nchini kwa ajili ya 
utalii hutembelea Hifadhi za Taifa. Hata hivyo, pamoja na idadi ya watalii kuongezeka, idadi ya watalii wengi hutembelea Hifadhi za Kaskazini tu, wakati Hifadhi za Kusini na Magharibi zina vivutio vya kipekee na vya ubora wa aina yake.

Hivi sasa idadi ya vitanda katika maeneo ya hifadhi kwa ujumla inafikia vitanda 6,681 na kwa ongezeko hili katika kipindi cha miaka mitano ijayo idadi hii itafikia vitanda 8,421.

Katika kuhakikisha kuwa maeneo haya yaliyotengwa yanapata wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, jitihada mbalimbali zitafanywa ili kuyatangaza maeneo haya ikiwa ni pamoja na kuandaa Kongamano Maalum litakalotangaza fursa za uwekezaji katika hifadhi linalotarajiwa kufanyika mwezi Februari mwakani. Kongamano hilo linatarajiwa kushirikisha wawekezaji mbalimbali wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi ambapo watapata fursa ya kuyafahamu kwa undani maeneo hayo na namna gani uwekezaji wao utakavyoleta faida kwa sekta ya utalii na uchumi wa nchi yetu.

Aidha, shirika limejipanga kwa maana ya kuandaa miundombinu bora kama vile barabara, madaraja na viwanja vya ndege ambavyo vitarahisisha zoezi la uwekezaji kwenye maeneo hayo.

Uamuzi wa TANAPA wa kutenga maeneo haya ya uwekezaji unafuatia jitihada nzuri ambazo zimekuwa zikifanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Serikali yake za kuvutia wawekezaji nchini pamoja na watalii ambao wataweza kuongeza pato la taifa.

Katika siku za hivi karibuni Tanzania imetajwa kuongoza kwa kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na vivutio bora Afrika ikiyaacha mbali mataifa mengine kama vile Afrika ya Kusini; Botswana na Kenya.

Taarifa hii inatokana na utafiti ulioendeshwa na mtandao wa safaribookings.com wa nchini Uholanzi ambao ni maarufu kwa uchambuzi wa maeneo bora ya utalii duniani.Katika matokeo ya uchambuzi huo Tanzania iliweza kuwa na vivutio kumi (10) kati ya hamsini (50) vilivyo bora kabisa barani Afrika ambapo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilikuwa ya kwanza kabisa miongoni mwa vivutio hivyo. Hivyo hii imetoa fursa ya pekee kwa wawekezaji kuwekeza kwenye maeneo haya hasa, Ruaha, Mahale, Katavi na Hifadhi zote kwa ujumla.

Vivutio vingine vilivyoifanya Tanzania kuongoza ni pamoja na Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mahale, Gombe, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Arusha. Vingine ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Selous.

Ni dhahiri kuwa katika siku za karibuni Tanzania itaweza kuongeza idadi ya watalii kutokana na taarifa hizi na hivyo kuzifanya taasisi kama TANAPA kuanzanza mikakati ya kuongeza idadi ya vitanda katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kukidhi ongezeko hili.

Imetolewa na Mkurugenzi Mkuu
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P.3134
ARUSHA

12.11.2013