Tanapa:Tumejipanga kupambana na ujangili

Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Allan Kijazi, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), katika... thumbnail 1 summary
Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Allan Kijazi, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Meneja Uhusiano wa

Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limesema  limejipanga nje na ndani ya nchi ikiwamo kuwashirikisha wanakijiji wanaozizunguka hifadhi hizo kupambana na ujangili.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya serikali kusitisha operesheni ya kutokomeza ujangili kutokana na kuwapo kwa madai ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya raia.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wameanzisha vikosi kazi kwa ajili ya kutoa elimu na misaada mbalimbali kwa wanakijiji ili kutatua matatizo yatakayojitokeza wakati wa utekelezaji wa  majukumu ya kutokomeza uhalifu.

“Tunatarajia kuwapatia mafunzo na vitendea kazi vya kisasa askari wa wanyamapori kwa kushirikisha polisi wa kimataifa (Interpol) ili kuimarisha mtandao wa kutokomeza ujangili nchini,” alisema.

Wakati zoezi la tokomeza ujangili linaendelea, Tanapa imetenga maeneo 34  ya uwekezaji kwa lengo la  kuinua utalii Kusini na Magharibi mwa Tanzania kwa kupanua wigo wa huduma ya malazi.

Alisema maeneo  yaliyotengwa yatakuwa kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na kambi za kudumu kwa wageni zitakazopatikana katika Hifadhi ya Kilimanjaro, Katavi, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Saadani, Tarangire, Rubondo na Kitulo.

Kijazi alisema uamuzi wa kutenga maeneo hayo umezingatia ukuaji wa sekta ya utalii nchini. Asilimia 75 ya wageni wanaofika nchini hutembelea Hifadhi za Taifa.

Aidha, alisema shirika hilo limejipanga kuandaa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege ili kurahisisha zoezi la uwekezaji kwenye maeneo yaliyoanishwa.
 
CHANZO: NIPASHE