Wakamatwa na vipande viwili vya meno ya tembo, tai 9 zenye nembo ya Tanapa

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa kupatikana na vipande viwili vya meno ya tembo maeneo ya Mbez... thumbnail 1 summary
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa kupatikana na vipande viwili vya meno ya tembo maeneo ya Mbezi Msigani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 22 mwaka huu, saa 6:30 mchana.

“Katika harakati za kupambana na ujangili pamoja na wizi wa nyara za serikali tumekamata vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya mamilioni ya fedha,” alisema.

Kamishna Kova alisema watuhumiwa hao ni Regina Peter (29) na Upendo Peter (33), wote wakazi wa Mbezi Msigani, kwamba baada ya kuhojiwa walikiri kununua meno hayo vipande viwili kwa watu wawili, Mama Joseph na Anna kwa sh 200,000.

Alisema watuhumiwa wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano na polisi.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limekamata gari aina ya Noah linalotumiwa na majambazi katika uporaji wa mikoba ya wanawake.

Kova alisema askari walilikamata gari hilo lenye namba za usajili T 437 CCJ rangi nyeusi maeneo ya Kijitonyama ambapo ndani yake lilikutwa na mikoba mitatu ya kike, begi jeusi lenye nguo mbalimbali za kiume na fedha sh 700,000.
Alisema kuwa begi hilo liliibiwa kutoka kwenye gari aina ya Harrier baada ya kuvunjwa kioo.

“Begi hilo lilitambuliwa na Pius Philipo, hata hivyo baada ya muda walijitokeza vijana wawili ambao ni Mbarouk Said (30) na Sultani Masoud (28) wote wakazi wa Ilala wakidai kuwa gari ni mali yao na kuwa walimkodisha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Udenda,” alisema.

Alisema kuwa baada ya ufuatiliaji muda mfupi walifanikiwa kumkamata Abdulraufu Hussein (18) mkazi wa Buguruni Malapa na alipopekuliwa alikutwa na simu mbili za mkononi aina ya Samsung Garax, mifuko tisa ya kuhifadhia laptop, hati mbili za kusafiria na tai tisa zenye nembo ya Tanapa.

Vilevile alikutwa na kadi mbili za benki, noti mbalimbali za Kichina, power window za gari nne, Usb tatu pamoja na nyaraka za watu mbalimbali.

Chanzo: Tanzania Daima