Watu 30,000 hufa kwa uchafu kila mwaka nchini

WATU 30,000 ikiwemo idadi kubwa ya watoto hufa nchini kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotokana na uchafu. Hayo yalielezwa jana na mrat... thumbnail 1 summary
WATU 30,000 ikiwemo idadi kubwa ya watoto hufa nchini kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotokana na uchafu.
Hayo yalielezwa jana na mratibu wa kampeni ya kitaifa ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima, alipokuwa akitoa taarifa ya kilele cha kampeni ya unawaji mikono duniani itakayofanyika kitaifa Novemba 19 mwaka huu katika viwanja vya Peoples Club mjini hapa.
Alisema kutokana na watu wengi kutokuwa na uelewa wa umuhimu wa unawaji mikono kwa sabuni pamoja na matumizi bora ya vyoo, wizara imeamua kila mwaka kufanya kampeni  hiyo ili kuepusha vifo.
Mwakitalima alisema Tanzania inapoteza zaidi ya sh bilioni 13 kwa mwaka kutokana na kutibu watu wanaougua magonjwa yatokanayo na kuhara yanayosababishwa na uchafu.
Alieleza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni watekelezaji wakuu katika suala la usafi wamejipanga kutoa elimu, ili wananchi wabadilike na  waone usafi ni jambo la kuzingatia kwa umakini.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, alisema katika maadhimisho hayo watafanya Msafara wa Sabuni yenye manufaa kuanzia kwa wanafunzi wa shule za msingi kwani wao ndio walengwa zaidi.
“Napenda niwaambie ukimfundisha mtoto wakati bado akiwa mdogo akikua hataweza kukusumbua, hivyo Msafara wa Sabuni unaanzia mashuleni, ili kuwafunza baadaye wasiweze kuja kufa kwa magonjwa yatokanayo na uchafu,” alisema Kone.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajia kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Usafi ni ustaarabu unaaza na sisi, tumia choo bora, nawa mikono kwa sabuni, okoa maisha ya watoto”.

Chanzo: Tanzania Daima