Madaraka Nyerere, Vitali Maembe wateuliwa mabalozi wa CDEA ili kuchangisha fedha kwa kupanda Mlima Kilimanjaro

Viongozi wa CDEA wakiwa na Mabalozi wa kampeni ya kupanda Mlima Kilimajaro wakat wakizungumza na waandishi wa habari, kutoka kushoto ni ... thumbnail 1 summary
Viongozi wa CDEA wakiwa na Mabalozi wa kampeni ya kupanda Mlima Kilimajaro wakat wakizungumza na waandishi wa habari, kutoka kushoto ni Afisa wa Program, Naamala Samson, Mkurugenzi Mtendaji wa CDEA, Ayeta Wangusa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CDEA na balozi wa kampeni hiyo Madaraka Nyerere, Mwanamuziki na balozi wa kampeni ya Kupanda Mlima, Vitali Maembe, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya CDEA, Rose Mwalimu na Afisa Habari wa CDEA, Mandolin Kahindi


Madaraka Nyerere, Mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, pamoja na Mwanamuziki Mzalendo Vitali Maembe wameteuliwa na shirika lisilo la kiserikali Culture and Development East Africa (CDEA) kuwa mabalozi wa kushiriki kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuhamasisha jamii kuchangia ujenzi wa jukwaa la sanaa na ubunifu jijini Dar es Salaam.

Kampeni hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro imeandaliwa na CDEA kupitia njia ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Septemba 7 hadi 13 mwaka huu ili kujenga jukwaa na sanaa na ubunifu litakalowapa fursa wasanii na vijana kukutana, kufikiri na kubuni kwa pamoja ambapo mawazo ya kisayansi yatakutana na sanaa na pia sanaa kukutana na taaluma nyinginezo nyingi.

Mkurugenzi Mtendaji wa CDEA, Ayeta Wangusa anasema “ili kufanikisha kampeni yetu ya mwaka mmoja tuliyoipa jina la ‘FUN FOR FUNDS’, tumeona ni vyema kupanda mlima Kilimanjaro kwa kumtumia Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya CDEA, Madaraka Nyerere pamoja na Vitalis Maembe ambaye ni mwanamuziki mzalendo”

Wangusa anasema fedha zitakazopatikana kwenye kampeni hii maalumu zitatumika kusaidia uzalishaji wa kazi za ubunifu za njia mbalimbali za mawasiliano-bunifu, kuwekeza katika kuanzisha maabara ya Filamu(yaani film lab) na kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Jukwaa la sanaa na ubunifu.

Kwa upande wake Madaraka Nyerere anasema, “Nimekuwa nikipanda Mlima Kilimanjaro mara kwa mara kwa lengo la kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyinginezo za maendeleo, hivyo mwaka huu nimeona nifanye jambo hili kuhamasisha uchangiaji wa jukwaa hili la sanaa na ubunifu kwa kushirikiana na CDEA”

Madaraka anawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia katika kampeni hii ili kufanikisha kufikiwa kwa lengo lake. “Wadau watakaopenda kuunga mkono zoezi hili,wanaweza kutuma michango yao kwa njia zifuatazo: M-PESA: 0765544714, TIGOPESA: 0713160668 Au Benki: CRDB BANK PLC, Jina la Akaunti: CULTURE AND DEVELOPMENT EAST AFRICA TZS ACC: 0150210421400, USD ACC:  0252210421400, SWIFTCODE: CORUTZTZ”
Vitali Maembe akitoa vionjo vya wimbo wake Vuma


Kwa upande wake Mzee wa ‘Sumu ya Teja’, Vitali Maembe anasema pamoja na kuwa hii ni mara ya kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro amefanya mazoezi ya kutosha kumuwezesha kufika kwenye kilele jambo ambalo ni ndoto yake kubwa kama mwanamapinduzi wa kimuziki.

Culture and Development East Africa (CDEA) ni shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma kwa wasanii, viongozi wa utamaduni, wajasiliamali, maafisa utamaduni na mipango miji. Pia hufanya kazi na Mashirika makubwa ya kimaendeleo, taasisi za kiraia na Elimu katika maendeleo ya utamaduni, mipango na utekelezaji kwa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.