WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA DINI KWENYE VITA DHIDI YA UJANGILI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu wa pili kulia), Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Dkt.Reginald Mengi ( wa kwanza kulia)... thumbnail 1 summary
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu wa pili kulia), Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Dkt.Reginald Mengi ( wa kwanza kulia) wakiwa katika sala kabla ya kuanza Mkutano aa Viongozi wa dini zote nchini kushirikiana kwa pamoja kupambana na ujangili wa Wanyamapori na usafirishaji haramu wa Wanyamapori hai, Wengine ni Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa ( wa kushoto) akifuatiwa na Waziri kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa

Waziri wa Maliasili na Utalii imeanza kushirikiana na viongozi wa dini nchini katika kuhakikisha kuwa ujangili wa Wanyamapori , biashara ya meno ya tembo na usafirishaji haramu wa wanyamapori hai unakoma kwa kuwaelimisha Viongozi wa dini zote nchini ili waweze kuwahuburia waumini wao kuacha kujihusisha na vitendo hivyo kwani ni chukizo mbele ya Mwenyezi Mungu.
Akizungumza kwenye mkutano wa Viongozi wa dini zote nchini uliofanyika jana jijini Dar es Salaam Mhe, Nyalandu alisema vita dhidi ya Ujangili vinahitaji ushirikiano wa pamoja hasa kwa viongozi wa kiroho kwani wao wana kundi kubwa la watu wanaloliongoza katika jamii kwa kuwahudumia kiroho na kimwili.
Mkutano huu ni moja ya maazimio yaliyofikiwa mwezi wa tano huu kwenye mkutano mwanzo uliofanyika jijini Dare s Salaam wa kujadili mikakati ya kutokomeza ujangili wa wanyamapori na biashara ya meno ya tembo uliohusisha Wizara ya Maliasili na Utalii, Wadau wa Kimataifa wa Maendeleo na Jumuiya za kimataifa ikiwepo UNDP NA ICCF.
Mhe. Nyalandu alisema Viongozi wa dini ni watu muhimu sana katika kuhakikisha Maliasili za taifa ikiwemo wanyamapori na misitu inalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa hata vitabu vitakatifu na kurani vinasisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi viumbe vya Mwenyezi Mungu.
‘’Viongozi wa dini lazima muwahubuirie waumini wenu kuwa kujihusisha na ujangili ni dhambi hivyo lazima waaachanae na vitendo hivyo viovu’’ Mhe. Nyalandu alisema
Alisema watu wanaojihusisha na mauaji ya tembo na usafirishaji haramu wa wanyamapori hai ni waumini wa dini ya kikiristo na dini ya kiislaamu hivyo kama Viongozi wa dini wakikemea vitendo hivyo viovu makanisani na misikitini kwa kuwakanya waumini wao hivyo wataweza kuachana na vitendo vya ujangili.
Aidha, alisema kuwa kupitia mkutano huo, Serikali pamoja na viongozi wa dini watakuwa na sauti moja yenye nguvu ambayo waumini wa dini zote wataweza kuisikia na kuitekeleza katika mapambano ya kuhakikisha mauaji ya tembo na usafirishaji haramu wa wanyamapori hai unakoma kwa kuwa Viongozi wa dini ni watu wenye sauti yenye kugusa mioyo ya watu.
Aliongeza kuwa, Viongozi wa dini kupitia mkutano huo sio tu watashiriki kwenye vita dhidi ya Ujangili pia watakuwa mstari wa mbele kwenye masuala ya uhifadhi na uendelezwaji wa Maliasilli za taifa.
‘’Sauti za viongozi wa dini ni kubwa kuliko bunduki na ni kubwa kuliko magereza hivyo tunaamini Maliasili za taifa zitaendelea kulindwa na kuhifadhiwa kwa kushirikiano nao.’’ Mhe Nyalandu alisitiza
.
Naye , Shekhe wa Dar es Salaam ,Alhadi Musa Salumu alisema wamenyamaza kiasi cha kutosha huku vitendo viovu vikiendelea kutafuna Maliasili za Taifa hivyo ni lazima wasimamie uadilifu na hisani sio kwa binadamu tu hata kwa viumbe wengine wakiwemo Wanyama pamoja na ndege nao wanahitaji hisani ya kuishi katika mazingira yao kwa kutendewa wanavyostahili.
‘’Mwenyezi Mungu anasema kila kitu kitendewe wema hata mnyama anayestahili kuuawa sio lazima umpige risasi kumi na moja wakati kulikuwa na uwezekano wa kutumia risasi moja tu’’ Shekhe Salum alisema.
Alibainisha kuwa Wanyama wana haki ya kufurahia mazingira yao kama Mtume anavyowataka waislamu wawetendee uadilifu na hisani wanyama wote wanaoliwa na wasioliwa na sio uharamu wanaofanyiwa sasa baadhi ya Wanyamapori kwa kuwaua na kuwang’o pembe na meno yao.
Naye,Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alisema Mungu kampa Binadamu uwezo wa kuvitawala viumbe vyote vinavyopatikana katika uso wa dunia na sio kuvipukutisha kama wanavyofanya sasa kwani hayo sio mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Amesema tani za magogo pamoja na biashara ya meno ya tembo zinazoendelea kusafirishwa kila kukicha ni ishara tosha kuwa baadhi ya watu hawana hofu ya Mungu hivyo wao kama viongozi wa kiroho wataendelea kuwaelimisha waumini wao na ikiwezekana kuwakemea kwani kuna binadamu wenye macho lakini hawaoni na kuna binadamu wenye masikio lakini hawasikii.
Alisema Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa dini ni lazi wahakikishe Chama cha Haki za wanyama kinafufuliwa kwani kwa sasa Wanyama wanoishi majumbani na wanyamapori wamekuwa wakimbuna na ukatili usiovumilika hivyo lazima watetewe.
Aidha, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi alisema kuwa mkutano huo ni muhimu sana kwani Watumishi wa Mungu ni watu wanaoaminika katika jamii na wanajukumu kubwa sana katika kuhakikisha viumbe vyote vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu vinaendelea kuwepo kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema Viongozi wa dini ni lazima wawe thabiti katika vita dhidi ya Ujangili wa wanyamapori, Biashara ya meno ya tembo na usafirishaji haramu ya Wanayamapori hai kwani kwa sasa hali inatisha na wahusika ni wanaojishughulisha na vitendo hivyo ni Waumini wa dini zote za kikiristo na kiislamu.
‘’ Watumishi wa Mungu na sisi wafuasi wenu lazima tutambue Maliasili ni mali za Mwenyezi Mungu na ametupa mamlaka ya kuzitumia na si kuzimaliza kama tunavyofanya sasa hatuna haki hiyo sisi tumezikuta basi tusizitumie kwa fujo’’
Alisema Watumishi wa Mungu wana kazi kubwa ya kuwaonesha na kuwafundisha Waumini wao kuwa Mapenzi ya Mungu yanawataka watunze viumbe alivyoumba Mwenyezi Mungu na sio kuviharibu kwani hizo ni zawadi walizopewa na Mwenyezi Mungu’’
Amesema kama viongozi wa dini wakiweza kufikisha ujumbe kwa waumini wao vita hivi vitafanikiwa kwa sababu wanaaminika kwenye jamii na wana nguvu kubwa sana kwa jamii hivyo chochote wanachosema wanaaminika kwa jamii kwa sababu Waumini wa dini zote wanazungumza na Mungu kupitia wao.
‘’ Viongozi wa dini tuonesheni njia katika hili , tukeemeeni pale mnapoona hatuendi sawa kama mnaamini tunayofanya sio mapenzi ya Mwenyezi Mungu ’’ Dkt. Mengi alisisitiza
Naye Waziri kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa amesema kuwa ifike hatua sasa viongozi wa dini wakatae michango ya pesa ya watu wanaotaka kujenga makanisa kwa pesa walizozipata kupitia ujangili wa Wanyamapori kwani kufanya hivyo ni kuhalalisha ujangili kwenye nyumba za ibada.
Akiwa na kofia mbili ya uchungaji na pia ni mwanasiasa amewataka viongozi wa dini kutowanyamzia wanasiasa wanapokengeuka kwa kuhamasisha wananchi kuharibu maliasili za taifa kwa mtaji wa kura hivyo ni lazima wa wakemee kwa nguvu zao zote bila kujali cheo na hadhi ya wanasiasa hao pindi wanapofanya hivyo.
Pia amesema suala la kupambana na ujangili halina chama wala itikadi hivyo amewataka viongozi wa dini kulikemea kwenye nyumba za ibada kwani viongozi wa dini watu wenye nguvu na wanaoheshimika katika jamii.