UWANJA WA NDEGE MPANDA WAASWA KUTUNZA MIUNDOMBINU

Na Saidi Mkabakuli, Mpanda Kufuatia kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, mkoani Katavi, Serikali imewaasa... thumbnail 1 summary
Na Saidi Mkabakuli, Mpanda

Kufuatia kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, mkoani Katavi, Serikali imewaasa watumiaji wa uwanja huo kutunza miundombino ya uwanja huo ili kuweza kuhudumia wakazi na wageni wapitao uwanjani hapo kwa muda mrefu.

Wito huo umetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, mkoani Katavi.

Bibi Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imekamilisha kazi ya kuufanya uwanja huo uwe wa kiwango kizuri tayari kwa kutumika kwa ndege za binafsi na biashara, hivyo uongozi wa uwanja huo hawana budi ya kuhakikisha miundombinu ya uwanja huo inatunzwa ipasavyo.

“Kama munavyofahamu Serikali imekuwa ikiwekeza sana katika uendelezaji wa miundombinu ya usafiri nchini hasa kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi na kuendelea na kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo ya kimkakati, hivyo kuna haja ya kuunga mkono jitihada hizi za Serikali,” aliasa Bibi Mwanri.

Akitoa taarifa ya uendelezaji uwanja huo kwa msafara wa timu ya ukaguzi, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu alisema uwanja huo umeboreshwa na hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege za kiwango cha kati na hata zile ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.

“Uwanja huu umekarabatiwa na barabara ya kuruka na kutua ndege imerefushwa kwa kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 1,820 na upana wa mita 30,” alisema Bw. Lyatuu.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, kukamilika kwa uwanja huo kumevutia idadi ya abiria wanaoutumia uwanja huo kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390 mwaka 2013/14.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),  Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na usafiri wa anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.

Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi. 

Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.

Lengo la Dira ni  kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo uwanjani hapo.
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akizungumza na Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mpanda, Mkoani Katavi Bw. Seneti Lyatuu (Kulia). Anayefuatilia mazungumzo ni Bw. Omary Abdallah ambaye Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango).