Maofisa wa Klabu ya Arsenal kutua Tanzania wiki hii kuangalia fursa za ushirikiano na wafanyabiashara nchini

Klabu ya Arsenal imepanga kutuma maofisa biashara wake jijini Dar es Salaam, Tanzania kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano na wafany... thumbnail 1 summary
Balozi Peter Kallaghe, akiwa na maafisa wa masoko wa Arsenal.Klabu ya Arsenal imepanga kutuma maofisa biashara wake jijini Dar es Salaam, Tanzania kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano na wafanyabiashara kadhaa wakubwa nchini Tanzania.

Huu utakuwa ujumbe wa kwanza kabisa wa Arsenal nchini Tanzania, ambapo klabu hii kubwa ya England inataka kujenga ushirika mkubwa kabisa katika maeneo ya masoko na chapa zake, ili kutanua mafanikio yaliyofikiwa kwenye nchi nyingine za Afrika kama Kenya, Uganda na Nigeria.

Washika Bunduki hao wa London wanataka kutoa fursa kwa benki za Tanzania pamoja na kampuni za simu na taasisi nyingine kuweza kupata rasilimali zihusianazo na Arsenal, kama vile bidhaa zilizosainiwa kwa majina ya wachezaji, tiketi za mechi.

Safari hii kwa kiasi kikubwa imefanikishwa na Ubalozi wa Tanzania katika Uingereza, Kupitia kwa Mhe Balozi Peter Kallaghe, ambaye binafsi ameshiriki kuwaarifu maafisa hao, mazingira ya nyumbani, na ukuaji wa sekta za binafsi katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Arsenal wanasema kwamba wanaweza kuwapatia washirika wao hao uwanja mpana wa masoko kwa ajili ya kuwasaidia kutimiza malengo mbalimbali ya kibiashara.

Ofisa Biashara Mkuu wa Arsenal, Vinai Venkatesham amesema kwamba wameichagua Tanzania kwa sababu wana washabiki wengi, na kwa kushirikiana na taasisi za Tanzania, watakuwa karibu zaidi na washabiki wao kuliko ilivyokuwa awali.

“Katika bara lenye nchi zaidi ya 50, tumechagua kuzuru Tanzania kimkakati kwa sababu tunaiamini nchi hiyo. Arsenal ina mamilioni ya Watanzania ambao ni washabiki waaminifu na wenye mapenzi makubwa nayo.

“Kwa kushirikiana na taasisi za huko, tutaweza kuisogeza klabu karibu zaidi na washabiki hao kuliko ilivyokuwa awali, huku tukizipatia taasisi husika fursa pekee za kuifikia klabu yetu,” akasema Venkatesham.

Wajumbe hao wa jopo la Maendeleo ya Ushirikiano ya Arsenal wanatarajia kuwasili nchini Tanzania Januari 18 mwaka huu, ambapo watakaa kwa wiki moja jijini Dar es Salaam, kuitisha mikutano kadhaa ya awali ya kibiaashara na kuzindua rasmi mchakato wa kutafuta washirika wa kwanza kabisa nchini Tanzania.

Chanzo: Tanzaniasports