Nchi za kiafrika zimeaswa kuungana katika mapambano ya kukabiliana
na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu wao ni wahanga na waathirika wa kwanza wa
mabadiliko ya tabianchi duniani .
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira
Dkt. Benelith Mahenge wakati akifungua mkutano wa vyama vya kiraia
vinavyopambana na mabadiliko ya tabia nchi ukanda wa Afrika Mashariki(East
Africa Civil Society Conference on Climate Change Adaptation) ulioitishwa na
wenyeji Forum CC kwa kushirikiana na PACJA kutoka Kenya na AFCN Kunduchi jijini Dar es salaam .
Akiongea katika mkutano huo Dtk. Mahenge amesema hatua za haraka za makabiliano
ya tabianchi lazima zichukuliwe kutoka
ngazi ya chini ya nchi hadi kimataifa ili kuzuia na kulinda usalama wa dunia
kwa vizazi vijavyo.
“ni kweli nchi za
Afrika Mashariki tayari tumechukua hatua nzuri ya kuwa na mipango ya mabadiliko
ya tabianchi lakini haitoshi kuwa na mipiango bila utekelezaji”amesema Mahenge
Kuna changamoto nyingi zinazotukabili kama Afrika juu ya
mabadiliko ya tabianchi kama ukosefu wa fedha katika kukabiliana huko. Nchi
wachafuzi wa Ulaya ambao asilimia 97 ndio waharibifu kutokana na kuwa na viwanda vikubwa
vinavyotoa hali joto duniani. Bado hazijakubali kufadhili na kutoa pesa kwa
nchi zilizoathirika hasa Afrika na nchi za bara la Asia.
“Bado hatujafanya tafiti za kutosha kubaini ukubwa wa tatizo
la mabadiliko ya tabia nchi hasa kwetu ukanda huu wa Afrika Mashariki, hi yote
inatokana na kutokuwa na bajeti ya kutosha katika nchi zetu za Afrika. ”Anasema
Mahenge
Mwisho Waziri huyo wa mazingira amesema elimu ni muhimu
katika mabadiliko ya tabianchi bado nchi
za Afrika Mashariki hazijatoa elimu ya kutosha kwa wananchi wake. Watu wetu wanaendelea kukata miti hovyo,
wanalima hadi katika vyanzo vya maji, ukame umeongezeka , hamna chakula cha
kutosha, tunabakisha majangwa bila kuwa na juhudi za upandaji miti.
Amewaomba washiriki wa kongamano hili kuzichukulia
changamoto za mabadiliko ya tabianchi kama njia
ama chanzo cha kupigana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuwa na
suluhisho mbadala bila kusubiri wafadhili na wahisani wa nchi za Ulaya.
Mkutano huo uliodumu kwa siku mbili ulishuhudia vyama kutoka
ukanda wa Afrika Mashariki vikizindua umoja wao wa kushirikiana katika
mapambano ya mabadiliko ya tabianchi ikishirikisha washiriki kutoka Kenya,
Uganda, Rwanda, Burundi ,na wenyeji Tanzania.