Tukiyajua madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika maisha yetu, tutakuwa wa kwanza kutunza mazingira

Mabadiliko ya tabia nchi ni mabadiliko ya mtiririko wa mfumo wa hali ya hewa yanayochukua muda mrefu au mfupi na kusababisha hali mbaya za ... thumbnail 1 summary
Mabadiliko ya tabia nchi ni mabadiliko ya mtiririko wa mfumo wa hali ya hewa yanayochukua muda mrefu au mfupi na kusababisha hali mbaya za hewa ama uchache wa hali inayohitajika au wingi wa hali isiyohitajika na kusababsisha madhara. 

Kwa mfano mvua za Elnino au mafuriko ni matokeo ya mabadiliko ya hali ya tabia nchi na sote tunajua kuwa inasababisha madhara kwa binadamu, mazingira na mali. Je ukame? Pia ni matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa ambapo pia madhara yake ni makubwa.

Kwa kiasi kubwa, mabadiliko ya hali ya hewa yanasababishwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo shughuli za viwanda. Takwimu zinaonyesha kuwa tani billion 9 za hewa ya ukaa zinatolewa angani kila siku kutokana na shughuli za viwanda. 

Bila shaka, Tanzania si nchi ya viwanda vikubwa lakini hii haina maana hatuchangii katika kubadilisha mtiririko wa tabia nchi kwa kuwa tunafanya kwa njia yetu ya kukata miti mingi bila kuwa na mpango madhubuti wa kupanda miti inayokatwa kwa ajili ya matumizi ya nishati au ujenzi. Miti ni muhimu sana katika mazingira kama shokzoba katika gari kwani husaidia kutengeneza hali ya hewa nzuri na kuzuia maji ya mvua kubaki juu ya ardhi mvua zinaponyesha.

Takwimu zinaoneysha kuwa robo tatu ya uoto wa asili umekatwa tayari kwa hiyo imebaki robo ambayo nayo inaendelea kukatwa bila kuwa na mpango wa kupanda miti upya. Watafiti kutoka Ujerumani wanasema ndani ya miaka 20 ijayo ukanda wa Africa ya kati, mashariki kusini Tanzania ikiwemo zitakuwa jangwa kabisa kutokana na uharibifu wa mazingira.
Miaka 20 ijayo si mbali, tafakari hali itakuwaje kukiwa jangwa? Mana yake ukame utatamalaki, pia mafuriko wakati wa mvua kwa sababu kutakuwa hakuna miti yaa kunyonya mvua chini. Tunasikia jangwa la sahara watu wanakufa kwa njaa, Tanzania huenda ikafika huko ndani ya miaka 20 ikiwa hatutachukua hatua madhubuti kukabiliana na tishio hili.

Mwaka huu mwanzoni mvua kubwa zilinyesha na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya nchi ikiwemo Tanga, Morogoro, Dar es Salaam na kwingineko ambapo madhara makubwa yalitokea kuanzia upotefu wa mali, ardhi na maisha ya watu. Huko Kilindi, Tanga vijiji sita vilizama ndani ya maji na kukosesha wananchi chakula na nyumba za kuishi, hapa Dar es Salaam pia nyumba nyingi zilizama na watu kufariki.

Kwa hiyo mabadiliko ya tabia nchi yanatugusa sisi wananchi kibinafsi na maisha yetu. Lakini tunaweza kufanya mambo ambayo yatasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa mfano kwakupanda miti maeneo ya wazi, shuleni, msikitini, kanisani au shambani. 

Namna tunavyotunza takataka pale nyumbani pia zinachangia kiasi fulani katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi, je unatupa plastiki hovyo? Kwa sababu plastiki ikitupwa hovyo na kupigwa na jua inaongeza hali ya joto kwa ujumla. Nyumba zetu je tunajengaje? Ukijenga juu ya mtaro unasababisha uharibifu wa mazingira, maisha na mali kwa sababu mvua ikinyesha maji yatashindwa kwenda njia yake na kusababisha uharibifu.

Mabadiliko ya tabia yanchi yanatuhusu na yaanathiri maisha yetu kwa hiyo ni wajibu wetu kushiriki kurekebisha madhara yake. Ninajua ni jukumu la serikali kutengeneza miundo mbinu ya upatikanaji wa nishati safi kama matumizi ya umeme wa jua na matumizi ya gesi kupikia. 

Lakini ni wajibu wetu kuwahimiza kwakuwa ni rahisi kutumia na jua lipo kwa wingi nchini vivyo hivyo gesi basi tulazimishe serikali kuwezesha upatikanaji wake kwetu wananchi na itakuwa bei rahisi kwa kuwa umeme, gesi na maji vinapatikana bure.

Imeandikwa na Ashura Kayupayupa