Mbinu 20 za kuandika habari za mabadiliko ya tabianchi

RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21 Dotto Kahindi Nimekuandalia mbinu 20 za namna bora ya kuandika habari za maba... thumbnail 1 summary
RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21
Dotto Kahindi

Nimekuandalia mbinu 20 za namna bora ya kuandika habari za mabadiliko ya tabianchi. Mbinu hizi zimetokana na maoni yangu binafsi ambayo yamepitiwa na Mhariri wa jarida la Mtandaoni la Indian Ocean na Mchambuzi wa mambo ya mazingira katika ukanda wa bahari nchini Kenya, Wanjohi Kabukuru, naamini yatakuwa yenye msaada mkubwa kwako.

1.Ijue hadhira yako, unapoketi kuandika habari yako kuna mtu mmoja tu unayetakiwa kumfikiria, mtu huyu siyo wewe wala mhariri wako, bali ni msomaji ama msikilizaji wa habari yako. Ni muhimu sana kujua hadhira yako ni nani na pengine aina ya uelewa wao juu ya jambo unaloliandika, usitumie maneno ya kisayansi wakati unayemwandikia ni mtu wa darasa la saba. 

2.Ielewe mada, kama utakaa kuandika mada ya mazingira ambayo huna uelewa nayo, usitegemee msomaji wako ataielewa. Fanya utafiti wa kutosha kuweza kujipatia ufahamu wa kutosha wa mada yako, iwe kwa kusoma majarida au kuzungumza na wadau wenye uzoefu wa eneo hilo. Lakini bila hivyo ni sawa na kupaka rangi upepo, utakuwa unaandika madudu ambayo yatakufanya uonekana hauna maana mbele za watu. Ni sawasawa na kupika chakula, usipike chakula kibaya ambacho hata wewe mwenyewe huwezi kukila.

3.Jiielimishe, soma majarida mbalimbali ya sayansi na mazingira, ili kujijengea uwanda mpana na uelewa kwa manufaa yako. Kuandika habari za mabadiliko ya tabianchi ni muhumu kuelewa masuala ya kijamii, kisiasa na kisayansi, usibaki kuandika habari za mabadiliko ya tabianchi ni hatari, hakuna mtu anapenda kutishwa bila kuonyeshwa ukweli wa mambo. Jichanganye na watu mbalimbali, kama wanasayansi, wanasiasa na jamii ili kujua mambo mengi zaidi nje ya hapo. Waandishi wengi wa habari za mazingira wanadhani kujitenga na jamii na wanasiasa ni jambo jema, la hasha ni lazima kujua hakuna mabadiliko ya tabianchi bila siasa wala jamii.

4.Chagua mada, pamoja na kwamba hali ya uandishi wa habari kwenye nchi nyingi bado hairuhusu mtu kuchagua mchepua Fulani tu wa habari, lakini bado unanafasi ya kuamua kufanya mada Fulani au aina Fulani ya habari. Lakini uamuzi huu usukumwe na motisha yako, elimu yako na hata mazingira unayofanyia kazi, usilazimishe kufanya habari ambazo huna mapenzi nazo

5.Simama kwenye lengo, baadhi ya waandishi hupenda kuonekana wanajua mambo mengi sana hivyo kuandika habari ambazo zimejaa maelezo mengiiii wakidhani huo ndio uhodari. Hapana, hata waswahili husema miluzi mingi humpoteza mbwa, jaribu kuchukua mada moja na ieleze kwa unagaubaga kiasi kwamba msomaji anaweza kuielewa vyema, usichanganye mada, nisawa na kuchanganya mlenda na pilau, unaweza kutengeneza sumu

6.Misamiati, hakikisha unatoa ufafanuzi wa kila msamiati au neno gumu, ikiwezekana achana nayo kabisa maana yataweza kumchanganya msomaji. Maneno kama REDD, INDCs, UNFCCC, COP ni vyema ukayawekea ufafanuzi wake ili msomaji aweze kuelewa. Utaratibu huu uanzie kwa mtu unayemfanyia mahojiano yaani chanzo cha habari yako, hakikisha unakuwa na ufafanuzi wa kila neno gumu ili uwe na uwanda mpana wa kujimwaga kuandika habari yako

7.Kwa ufupi, waluguru wanasema Keep it Short and Simple, yaani usiandike lihabari lireeeeefu mpaka msomaji anaanza kutokwa na jasho, tumia maneno mafupi, mepesi na yanayoeleweka, nakwambia hakuna mtu atakuja kulalamika eti kwamba habari zako zinaeleweka sana kwa watu.

8.Ungana na wenzako, siku zote kidole kimoja hakivunji chawa. Jitahidi kuungana na vyama vya waandishi wa habari za mazingira, kwa Tanzania kuna Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), pia kuna Mtandao wa Bloggers wa Mabadiliko ya Tabianchi (BNCC) ambao umeanzishwa hivi karibuni, ungana nao. Huko utapata taarifa, uzoefu na utaweza kushiriki pia katika warsha mbalimbali zitakazokuongezea uelewa wa mambo. 

Jiunge na mitandao ya kimataifa pia, kuna tovuti nyingi tu za mabadiliko ya tabianchi, tumia mitandao kama google kutafuta na ujiunge nao ili uweze kupokea taarifa mbalimbali kwa email zinazoweza kukusaidia kuwa na ufahamu ya mambo mengi

9.Nenda kibiashara, moja ya sababu kubwa ya waandishi wengi kukwepa kuandika habari za mabadiliko ya tabianchi ni kipato. Kumbuka ili wazo lako la habari likubalike kwa mhariri lazima liwe na mwelekeo wa utofauti ambao utasaidia gazeti kuuza. Tumie mada kama za uchumi, kilimo, biashara nk kama sehemu moja ya wazo lako la habari, usiishie tu kusema nakwenda kutafuta habari ya mabadiliko ya tabianchi, hapana, ila italeta maana kama utasema natafuta habari ya mabadiliko ya tabianchi yanavyochangia kupanda kwa bei ya samaki. Hii italeta uzito kidogo 

10.Vaa miwani ya mabadiliko ya tabianchi, kila tukio linapotokea, liangalie kwa kutumia miwani hiyo, iwe ni uchaguzi, elimu, njaa, mafuriko, harusi nk fikiria ni kwa namna gani mambo hayo yanaweza kuathiri au kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo usiangalie mambo hasi tu, angalia pia na mambo chanya
Kumbuka neno mabadiliko ya tabianchi sio lazima yawe kwenye stori yako, Habari ya mabadiliko ya tabianchi itajulikana tu hata kama hutataja neno mabadiliko ya tabianchi kwenye habari yako, kwa mfano ukiandika habari kama hii, ‘Ng’ombe 20 wamekufa kutokana na ukame’, inafahamika ukame unasababishwa na nini na ni rahisi watu kuelewa uhuasiano wa tukio kama hilo na mabadiliko ya tabianchi

11.Tumia lugha ya picha, habari nyingi za mabadiliko ya tabianchi ni ngumu kuzielezea, ukikutana na hali hii, inashauriwa kutumia picha kama njia moja wapo ya kuonyesha hali halisi na kumfanya mtu aelewe zaidi. Wanasema picha husema maneno zaidi ya elfu moja

12.Weka utu na ubinadamu mbele, watu wengi hujali zaidi mambo yanayogusa maisha yao, familia zao, afya zao na mali zao. Mabadiliko ya tabianchi yanagusa maeneo hayo yote pia kwahiyo wakati unaandika habari yako jaribu kufikiria watu na vitu wanavyovijali. Gusa imani zao, maisha yao, tamaduni zao na hata mazingira yao na utaweza kukubalika katika jamii hiyo

13. Jiandae vyema kwa mahojiano, Kadri unavyojua mengi kuhusu mada na mtu unayekwenda kufanya nae mahojiano ndivyo utakavyokuwa na nafasi nzuri ya kupata maelezo stahiki. Usifike kwenye mahojiano halafu unaanza kumangamanga hata hujui wapi pa kuanzia, kuna watu wanakwenda kufanya mahojiano hawajua hata majina ya wanaokwenda kuwahoji, hili liepuke na ujiandae mapema kwa mahojiano yenye mafanikio. Pia eleza mahojiano hayo unakwenda kuyatumia wapi, nani ni hadhira yako, hii itampa nafasi unayemhoji kutoa maelezo ambayo yanaeleweka pia kwa aina ya hadhira yako.

14.Tafuta mbadala, wakati mwingine tunapofanya mahojiano na vyanzo vetu vya habari tunaweza kujikuta katika hali ya njia panda, unaweza kupata taarifa ambayo sio sahihi na kwakuwa umepewa au imetolewa na mtu mwenye nafasi au mwanasayansi basi ukadhani iko sahihi na ukaiandika kama ilivyo. Hapana, hii sio njia sahihi, jitahidi kuzungumza na mtu mwingine mwenye hadhi kama hiyo ili kupata picha nyingine. Mtu wa kwanza anaweza kuwa amekupatia taarifa yenye upendeleo ama isiyokuwa na ukweli, basi zungumza na watu wengine zaidi kwa uhakika na weledi.

15.Ukweli, baada ya kusema hapo juu haimaanishi sasa kila unapofanya mahojiano unachoambiwa ni uongo, la hasha, bali sikiliza maneno ya chanzo chako na ili kuhakikisha kinachosemwa ni kweli basi omba uthibitisho, kama anazungumzia takwimu, mwambie akupatie, kama anazungumzia idadi mwambie akupatia, na kama anazungumzie eneo mwambie akupatia uthibitisho huo. Kwa kufanya hivyo utaweza kubaini na kujiridhisha juu ya anachokizungumza. Siku zote njia ya mwongo ni fupi kama atakuwa anapika takwimu itakuwa rahisi sana kumbamba.

16.Nukuu, katika kufanya ripoti yako jitahidi kuweka nukuu za kila aina, washirikishe watu wa jinsia zote, marika yote ili kunena na kuongeza nguvu ya taarifa yako, lakini ni vyema kuzingatia nani ni muhimu kusema kitu ambacho kitaongeza uzito kwenye habari yako, kuna makundi muhimu ambayo ni vizuri kuyaangalia, hii ni pamoja na watoto, wanawake, walemavu, wazee na hata vijana. Hawa ukizungumza nao watakupa majibu yatakayokuongezea nyama kwenye habari yako, zungumza na watu wengi kadri uwezavyo kuweza kujipatia uelewa wa kutosha

17.Ukaribu na uhalisia, habari nyingi kutoka kwenye mikutano ya kimataifa, ya wanasayansi inaongelea zaidi mambo ya mabadiliko ya tabianchi kimataifa zaidi, tumia taarifa hizo kwa kuzihusisha na matukio ya nyumbani, kwa kutumia mifano iliyopo nyumbani ili kuweka uhalisia na ukaribu wa tukio lenyewe. Angalia ni jambo gani linahusiasa na mada Fulani iliyowasilishwa ambalo watu wa nyumbani wakilisikia wanaweza kuguswa na habari yako

18.Usilemazwe na taarifa za habari (press release), mara nyingi waandishi wa habari wanapenda ku-copy na ku-paste taarifa za habari na kuweka majina yao tu kisha kuwasilisha stori zao wakijiona ni wajanja kwelikweli, sawa utalipwa kwa habari yako kutoka, lakini itakuwa ni habari yenye ukakasi isiyovutia msomaji. Ukweli ni kwamba press release sio habari, ni mfupa tu ambao unahitaji ubunifu wa mwandishi kuuongezea nyama. Kwahiyo unatakiwa kuifanyia kazi zaidi ili kuwagusa wasomaji wako.

19.Kuwa mfuatiliaji na mdadisi, fuatilia kazi za waandishi wengine ili kujifunza wanavyoandika, unaweza kubaini mazuri na hata mabaya kutoka kwenye kazi zao, unaweza kupata habari nyingi za namna hiyo kwenye magazeti, blogs hasa kwenye blog hii ya tabianchi. Huwezi kujua kuandika vizuri kama hauna tabia ya kusoma kazi za wengine.

20.Fuata pesa zilipo, Kama hukujua, mabadiliko ya tabianchi ni stori zenye mamilioni ya pesa, kuna pesa nyingi kwenye eneo hili, pesa za kuzuia na kupambana na mabadiliko ya tabianchi zipo kwa wingi, lakini ni lazima ujue zilipo, nani anazipokea nani anazitumia, nani anahakikisha zinatumika ipasavyo, nani anatoa ufadhili kwa NGOs na hata wanasiasa. Fuatilia mambo haya utakuta umepata habari nzuri na nyingi zitakazokulipa hata wewe pia. Ukifuata nyuki utapata asali.

Ni hayo machache nimefanikiwa kukuletea, kama kuna mbinu nyingine sijaziweka, unakaribishwa kuchangia ili kuboresha zaidi kilichopo.