RoadToParis2015
with Tabianchiblog&CFIMedias21
Serikali ya
Tanzania kupitia ofisi ya makamu wa Rais imesema kuwa haitakuwa tayari kuona
nchi zinazoendelea zikiingilia na kukwamisha mipango ya maendeleo ya uchimbaji
wa gesi na mafuta kwa kigezo cha uchafuzi wa mazingira.
Msimamizi wa
mchakato wa kuandaa mchango wa kila nchi katika juhudi za dunia za kukabiliana
na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined Contributions –
INDCs), nchini Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya
Makamu wa Rais Dk Richard Muyungi anasema hategemei mataifa yaliyoendelea
kuitumia INDCs kukwaza maendeleo kwa nchi zinazoendelea
“Siamini wala
sitegemei wahisani wa maendeleo watatumia INDCs kama kigezo cha kutupa au
kutunyima misaada katika maeneo ambayo yatakuwa hayamo kwenye mchango wetu”
anasema Dk Muyungi.
Nchi zinazoendelea
zimekuwa na wasiwasi kuwa, INDCs ni mtego utakaotumika kama kikwazo cha
maendeleo ya kiuchumi kwa nchi hizo jambo ambalo Tanzania haitakuwa tayari
kukubaliana na hoja hiyo.
Anasema kama
mataifa yaliyoendelea na nchi wahisani hawatasaidia nchi katika maeneo ambayo
hayakutajwa kwenye INDCS, hilo halitakuwa jambo la kiungwana kwa sabababu maeneo
ya uchangiaji ni maeneo ya hiyari na sio ya lazima.
Mapema mwezi
uliopita Makamu wa Rais Benki ya Dunia (WB) na Mjumbe Maalumu wa Mabadiliko ya
Tabianchi Rachel Kyte alisema benki ya dunia itatumia INDCs kama kigezo kimoja
wapo wakati wa kutoa misaada ya kimaendeleo kwa nchi wanachama.
“Sisi benki
ya dunia tunavutiwa na INDCs kwa sababu kwazo tunaweza kuona mahitaji ya nchi
husika na hapo tunaweza kusaidia maeneo hayo, kwahiyo kupitia hizi INDCs
tunahitaji kujua maeneo gani nchi imeyapa kipaumbele yenye fursa za maendeleo
ya kiuchumi”
Akizungumzia
uchimbaji wa gesi na mafuta kwa Tanzania kama unaweza kuwa kikwazo cha
utekelezaji wa INDCs Muyungi anasema kuwa matumizi ya rasilimali hizo
hayaepukiki kwakuwa ni muhimu katika maendeleo ya nchi.
“Kwasababu mafuta
na gesi tumeshavipata ni lazima tuvitumie, ni lazima tuchimbe, matumizi ya
nishati mbadala ni muhimu lakini kama nchi tatizo tulilonalo ni uhaba wa fedha
za kuweza kuitumia njia hiyo ambayo ni ghali sana” anasema Muyungi.
Anasema Tanzania
itawasilisha INDCs ambayo itachangia kupunguza uzalishaji hewa joto kwenye
sekta za kilimo, mifugo, maji, bahari, misitu na uchukuzi huku ikisisitiza
katika kutumia mafuta na gesi ili kupata maendeleo kiuchumi.
“Mchakato huu ni wa kitaifa, hatukubali usimamiwe na
mgeni au mtu asiyejua mahitaji halisia ya nchi, hatutaki kukurupuka, tunataka
kuandaa kitu ambacho hakitaturudisha nyuma kimaendeleo”.
Afisa Miradi
shirika linalojihusisha na masuala ya mabadiliko ya Tabianchi ForumCC Tanzania
Fazal Issa anasema nchi zote zilizoendelea kipindi wanavumbua mafuta walitumia
njia za zamani za makaa ya mawe, gesi na mafuta na wakajipatia maendeleo
waliyonayo.
Lakini leo
hii nchi zote zinazoendelea hazitakiwi kutumia vyanzo hivyo vya nishati na
badala yake zinatakiwa kutumia nishati mbadala ambayo ina gharama kubwa na
Tanzania haina uwezo wa kuwekeza katika nishati hiyo.
“Ni bora tutumie
hizi njia rahisi za makaa ya mawe, gesi na mafuta tukiwa na lengo la kuwekeza kwenye
nishati mbadala hapo baadae, lakini tukisema tuingie moja kwa moja tuhamie kwenye
gesi asilia itakuwa ni uongo, hatutaweza kwa sababu uwekezaji wake ni mkubwa
mno” anasema Fazal
Anasema nchi
zinazoendelea zingeweza tu kuhamia moja kwa moja kwenye uwekezaji wa nishati
mbadala endapo nchi zilizoendelea zingeweka fedha za kusaidia uwekezaji huo jambo
ambalo halifanyiki kwa sasa.
Historia ya gesi nchini
Shughuli za
utafutaji mafuta na gesi asilia nchini Tanzania zilianza miaka ya 1950 kupitia
Kampuni ya Agip kutoka Italia na ugunduzi wa kwanza katika Kisiwa cha Songo Songo (Lindi)
mwaka 1974 ambao ulifuatiwa na ugunduzi mwingine katika eneo la Mnazi Bay
(Mtwara) mwaka 1982.
Hata hivyo,
gesi asilia hiyo haikuendelezwa kwa kuwa ilionekana haina manufaa ya kiuchumi
(uneconomical) kwa wakati huo. Baada ya ugunduzi huo, TPDC iliendelea kufanya
utafiti ikiwa ni pamoja na kuchimba Visima mbalimbali kwa ajili ya kuthibitisha
kiasi cha gesi asilia kilichopo katika maeneo ambako gesi asilia iliyogunduliwa.
Utafiti wa
mwisho ulikamilika mwaka 1991 ambapo mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafisha
gesi asilia Kisiwani Songo Songo pamoja na Bomba la kusafirisha gesi asilia
hiyo mpaka Dar es Salaam ulibuniwa na hadi Novemba, 2014 kiasi cha gesi asilia
kilichogunduliwa nchini ni futi za
ujazo trilioni 53.28 (53.28TCF)
Kamishna wa
Nishati na Masuala ya Petroli wa Wizara ya Nishati na Madini Injinia Hoseah
Mbise mwaka 2013 alisema Serikali inakusudia kujenga kiwanda cha gesi kwa ajili
ya mauzo ya nje (LNG=liquefied natural gas), ambapo kitaliwezesha taifa kuvuna
mapato ya dola za Marekani milioni 200 (sh. bilioni 320) kwa mwaka.
Pamoja na kuwepo kwa fununua za nchi nyingi za jirani kutaka
kununua gesi asilia ya Tanzania ni nchi ya Zambia ndio pekee iliyoomba kuuziwa
gesi hiyo kwa madhumuni ya
kuzalisha umeme na kupanua wigo wa uzalishaji wa viwandani.
Ombi hilo lilitolewa Jumatano,
Februari 25, 2015 na Rais wa Zambia Edgar Chagwa Lungu kwa Rais wa Tanzania
Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo mbili.
Msemaji wa
Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud January 2015 akaweka bayana kuwa
mradi mkubwa wa umeme wa gesi kupitia bomba kubwa kutoka Mtwara na Lindi hadi
Kinyerezi jijini Dar es Salaam umekamilika na kwamba wananchi wameanza
kunufaika.
“Mradi huu utasaidia kuokoa sh.1.6 trilioni,
zinazotumika kununulia mafuta ya kuzalishia umeme kwa sasa,” amesema.
Kwa mujibu
wa Badra, umeme wa gesi una faida kubwa kwa wananchi wa hali ya chini kwa vile
unapatikana kwa bei nafuu na hautegemei maji wala mabadiliko ya hali ya hewa
kama umeme wa kawaida.
“Kukamilika kwa mradi huu pia kutachochea
matumizi ya gesi asilia majumbani, na katika shughuri za usafirishaji, hivyo
kupunguza uchafuzi wa mazingira, matumizi ya mkaa na kuni nchini” anasema