RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21
Tanzania imesema itawasilisha mchango wake wa kila nchi
katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended
Nationally Determined Contributions – INDCs) katika wiki ya pili ya mwezi Septemba
mwaka huu.
Msimamizi wa mchakato huo nchini Tanzania ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dk Richard Muyungi
amesema mchakato huo ambao ulianza tangu mwezi Januari mwaka huu uko katika
hatua nzuri.
Moja ya mabasi ya mwendo kasi ambayo yanatajwa kuchangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa |
Ili kufanikisha mchakato huo Tanzania kama ilivyo kwa nchi
nyingine zinazoendelea imepata msaada wa wataalamu wa kufanya uchambuzi
yakinifu kutoka Serikali ya Ufaransa, na fedha kutoka GEF na UNDP kwa ajili ya
kuwezesha shughuli nzima ikiwemo mijadala na wananchi na wadau mbalimbali wa
mabadiliko ya tabianchi kutoka katika sekta tofauti.
Muyungi anasema “mchakato wa kuandaa INDCs ni lazima uwe wa
kitaifa ili kupata maoni ya jamii hasa wale wanaohusika, kwa hiyo ni muhimu
ukafanywa kwa uangalifu pasipo
kukurupuka na kujikuta tukiwasilisha mchango ambao utaturudisha nyuma
kimaendeleo”
Anasema pamoja na kwamba INDCs kuwa ni jambo la hiari kwa
nchi lakini maeneo ambayo yatatajwa kama muhimu itawalazimu kuyafanyia kazi, hivyo
anaona ni muhimu kujua kama watakayoyawasilisha watakuwa na uwezo wa
kuyasimamia na kuyatekeleza.
Maeneo muhimu kwa
Tanzania
Muyingi anasema maeneo ambayo yanaweza kusaidia kukabiliana
na kusaidia dunia katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na sekta ya
kilimo, mifugo, maji, afya, nishati, uchukuzi, misitu na sekta ya masuala ya
bahari.
“Tukipunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta
hizo, tunaamini tutakuwa tumechangia kuisadia dunia kuhimili mabadiliko ya tabianchi
na wananchi watakuwa na maisha bora”
Muyungi anaamini kuwa INDCs zitachangia kupunguza matatizo ya
migogoro ya ardhi ya wakulima na wafugaji inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na
uhaba wa mvua na ufugaji usiokuwa na tija.
Anasema kupitia miradi ya gesi asilia, uchimbaji wa visima,
uanzishwaji wa usafiri wa mabasi ya mwendo kasi na upatikanaji wa umeme vijini
utapunguza matumizi ya kuni na mkaa na matumizi ya magari binafsi jijini Dar na
hivyo kupunguza uazalishaji wa hewa ukaa.
“Mradi wa gesi asilia umeshakamilika, na mradi wa umeme
vijini nao unakwenda vizuri hii itapunguza matumizi ya mkaa na kuni, lakini
hata mradi wa mabasi ya mwendo kasi utapunguza msongamano wa magari barabarani,
hiyo ni mipango ya kimaendeleo isiyo na madhara kimazingira” anasema Muyungi
Ushirikishwaji wadau
Pamoja na kwamba mchakato wa kuandaa INDCs umeshaanza lakini
zoezi la kupata maoni kutoka kwa bado halijafanyika jambo ambalo linatia shaka
kama kweli Tanzania itakuwa tayari kuwasilisha mchango wake ndani ya wakati.
“Sisi hatuna taarifa yeyote ya kuanza kwa mchakato wa kuandaa
INDCs kwa Tanzania, kwa kifupi habari hii ndio kwanza nalisikia kutoka kwako na
hatujashirikishwa hata kidogo” anasema Mwenyekiti wa Umoja wa Azaki za Kiraia
za Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA) Ally Juma
Katika kutetea hoja hii Muyungi anakiri kuwa zoezi la
kuwashirikisha wadau limechelewa kutokana na kuchelewa kwa pesa kutoka kwa
wahisani na kwamba wadau wote wa Zanzibar na Tanzania bara watashirikishwa ili
kupata maoni yao.
“Ukimuuliza Mkurugenzi wa mazingira Zanzibar anajua maana
tumeshampatia taarifa na ni huyo ndiye anayetakiwa kuainisha wadau tutakaofanya
nao kazi tutakapofikia hatua hiyo. Sasa hivi tunasubiri UNDP watupatie pesa ili
tuanze na hatua ya kupata maoni ya wadau wote nchi nzima, ikiwemo Zanzibar”
anasema Muyungi.