Wataalamu wasema Jotoardhi litapunguza tatizo la umeme nchini

Mkurugeniz Mkuu anaeshughulikia masula ya Ufundi wa Kampuni ya Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi (TGDC), Bwana, Taramaeli Mnjokava akiwae... thumbnail 1 summary
Mkurugeniz Mkuu anaeshughulikia masula ya Ufundi wa Kampuni ya Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi (TGDC), Bwana, Taramaeli Mnjokava akiwaelimisha Viongozi wa Kata ya Swaya Mjini kuhusu faida za jotoardhi mapema 8 Agosti, 2015 mkoani Mbeya.
Mjiolojia Mkuu toka Wizara ya Nishati na Madini, Bwana. Jacob Mayalla akiwaeleza Viongozi wa Kata ya Swaya Mjini kuhusu historia ya nishati ya jotoardhi kuanza kufanyika hapa nchini miaka ya 1976 hadi 1978 mapema 8 Agosti, 2015 mkoania Mbeya.
Afisa Sayansi ya Jamii toka Kampuni ya Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Bi. Eva Nyantori akiwaeleza Viongozi wa Kata ya Swaya Mjini kuhusu namna gani jamii itahusishwa na mradi huo hususani katika suala la upatikanaji wa ajita kwa wakazi wa maeneo yenye mardi huo, mapema 8 Agosti, 2015 mkoania Mbeya.
Afisa Mawasiliano toka Kampuni ya Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Bi. Johari Kachwamba akiwaeleza Viongozi wa Kata ya Swaya Mjini kuhusu dhamira na majukumu ya Kampuni ya TGDC hususani masuala yote yanayohusiana na nishati ya jotoardhi mapema 8 Agosti, 2015 mkoania Mbeya.
Mhandisi Mipango toka Kampuni ya Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Bwana Chagaka Kalimbia akiwaeleza Viongozi wa Kata ya Swaya Mjini kuhusu faida za moja kwa moja za nishati ya jotoardhi, mapema 8 Agosti, 2015 mkoania Mbeya.



Na Benedict Liwenga, Maelezo-Mbeya
Kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme nchini, nishati ya jotoardhi imetajwa kuwa ni muhimu kwa kuwa itaisaidia Tanzania kuondokana na tatizo la umeme usiokuwa na uhakika pamoja na kupunguza gharama kubwa zitokanazo na matumizi ya mitambo ya uzalishaji umeme yenye kutumia mafuta. 
 Kauli hiyo imetolewa 8 Agosti, 2015 na Mjiolojia Mkuu toka Wizara ya Nishati na Madini, Bwana. Jacob Mayalla wakati wa Kampeni endelevu ya kuelimisha umma kuhusu nishati hiyo katika Kata za Swaya Mjini, Nzovwe pamoja na Igale jijini Mbeya. 
 Mayalla ameeleza kuwa, kwa kawaida utafiti wa nishati ya jotoardhi unahusisha hatua kuu tatu zikiwemo ya utafiti wa maeneo yenye upatikanaji wa nishati hiyo, uchimbaji pamoja na uzalishaji ambapo kwa mkoa wa Mbeya, tayari hatua ya utafiti ilishakwishafanyika katika miaka ya nyuma ingawa bado zoezi hilo ni endelevu ili kujidhihirisha na sehemu ya uchimbaji na kwasasa hatua zinazofata ni uchimbaji pamoja na uzalishaji ili kuongeza nguvu ya uzalishaji wa umeme ikiwemi kuwezesha matumizi ya moja kwa moja ya nyumbani. 
 “Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kubainika kuwepo na kiwango cha juu cha jotoardhi nchini ni pamoja na Ziwa Manyara, Ziwa Natron, Ngorongoro Crater, pia katika Mkoa wa Mbeya, na maeneo mengine ya Ziwa Eyasi na Mara (Maji Moto) yalibainika kuwa na kiwango cha chini cha joto”, alisema Mayalla. 
Naye Afisa Mawasiliano toka Kampuni ya Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Bi. Johari Kachwamba ameeleza juu ya hali ya uzalishaji wa umeme ilivyo hapa nchini hususani katika mkoa lengwa wa Mbeya kuwa inatumia Megawati 40 jambao ambalo umeme umekuwa usio wa uhakika, hivyo TGDC ina mkakati wa kuongeza uzalishaji huo hadi kufikia Megawati 200 jambao ambalo litaweza kusaidia na mikoa mingine ya pembezoni. 
 “Kampuni ya TGDC ni Kampuni tanzu iliyopo chini ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na tuna majukumu mengi ikiwemo kuharakisha uzalishaji wa nishati hii ya jotoaardhi ili iwe nishati mbadala na kupunguza mgao wa umeme kwani nishati hii pindi ikianza kutumiwa haitarajiwi kuisha, ni nishati endelevu”, alisema Kachwamba. 
 Kwa upande wake Afisa Sayansi ya Jamii toka TGDC, Bi. Eva Nyantori amezitaja baadhi ya fursa mbalimbali ambazo jamii itashirikishwa na mradi huo zikiwemo fursa za ajira ili kuwaongezea vipato wakazi wa maeneo ambayo nishati hiyo itapatikana, elimu juu ya afya hususani elimu dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwani pindi mradi utakapoanza kuna uwezekano wa kuwa na mahusiano baina ya wageni na wenyeji. 
 Kuhusu athari za mazingira ambazo zinaweza kujitokeza pindi mradi huo utakapoanza, Afisa Mazingira toka TGDC, Bi. Esther Range amefafanua kuwa kabla ya mradi kuanza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) litafanya ukaguzi wa maeneo husika ili kujiridhisha juu ya athari zinazoweza kutokea katika eneo husika. 
 “Nishati hii ya jotoardhi hatutegemei kuwa italeta atahri katika mazingira yetu kwani kampuni itachukua hatua madhubuti ili kuepusha athari zozote zinazoweza kujitokeza ikiwemo kuwahusisha watu wa NEMC kwani wao ndo watatupatia kibali cha kuweza kuendelea na mchakato wa uchimbaji wa nishati hii, hivyo niwatoe wasiwasi wananchi kuhusu athari”, alisema Range. 
 Naye Mhandisi Mazingira toka Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Bwana. Fikirini Mtandika amesema kuwa TGDC iko mbioni kuandaa Sheria zinazohusu nishati ya jotoardhi ili Kampuni iweze kufanya kazi zake kwa umakini na kwa kuzingatia Sheria, akaeleza pia kutakuwa na masuala ya fidia kwa wahanga ambao mradi huo ikitokea umeangukia katika maeneo yao na hapo aksema kuwa ikitokea hivyo Sheria Na. 4 na N. 5 ya mwaka 1999 zitatumika katika masuala ya fidia lakini kabla ya fidia jamii husika itapewa elimu ya kutosha kuhusu fidia ili kuijengea uelewa wa kutosha. 
 “Hii Sheria itambuliwe kuwa sisi kama Kampuni hatutohusika katika kufanya tathmini ya mali ya Mhanga isipokuwa kutakuwa na Mtathmini kutoka Serikalini ambaye yeye ndiyo atafanya kazi hiyo na sisi kazi yetu itakuwa kufanya malipo tu kwani itakuwa sio vema sisi kufanya tathmini kwani tunaweza kumpunja mhanga, na fidia hii itafanywa kwa kipindi kisichozidi miezi Sita, hviyo jamii iondoe wasiwasi kuhusu suala la fidia” alisema Mtandika.