Dotto Kahindi
RoadToParis with Media21project and Tabianchi blog
Ukosefu wa taarifa, elimu na
maarifa ya kufanya kilimo bora na kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi ni vyanzo vikubwa vya wakulima kutopata mavuno ya kutosha kulingana
na nguvu wanayotumia kuwekeza katika kilimo chao.
Mtandao wa Tabianchi umebaini hayo
baada ya kuwatembelea wakulima wa mahindi, ndizi, nyanya na mbogamboga katika Wilaya
ya Moshi vijini ambao mavuno ya kutosha kwao imekuwa ni changamoto kubwa kwa
sasa.
Ukosefu huo wa mavuno hasa katika zao
la mahindi kwa mwaka huu 2015 unatishia kuwepo wimbi la njaa kali katika maeneo
mbalimbali ya Wilaya hiyo hasa katika vijiji vya Kata ya Kirua Vunjo Magharibi.
“Kutokana na ufinyu wa elimu
hatujafanya lolote maana kama ni migomba ni ile ile, mahindi ni yale yale sasa
hatujui mabadiliko yako kwenye hali ya hewa au kwenye mazao yenyewe” anasema Methew
Nguma Mkulima wa mahindi katika kijiji cha Kirua.
Anasema “Hali ni mbaya sana, migomba
imenyauka na kahawa imegoma kabisa. zamani ndizi zilikuwa zinazaa sana lakini
sasa sielewi nini kimetokea, hakuna taarifa za kitaalamu za kutujuza tatizo hili
linasababishwa na nini”
Wilaya ya Moshi Vijijini pamoja na
maeneo mengine ya mkoa wa Kilimanjaro yalisifika sana kwa kilimo cha
umwagiliaji hapo zamani kutokana na kuwa na miundombinu ya kutiririsha maji
kutoka milimani jambo ambalo kwa sasa halipo tena.
Hali hiyo imewaacha wananchi katika
hali ya sitofahamu wakihaha huku na kule kutafuta mbinu mpya za kufanya kilimo
cha kawaida ili kujipatia mavuno na mapato ya kukuza uchumi katika familia zao.
Hali ya sasa ya magonjwa ya mimea
na ukame vimewaathiri wananchi wa maeneo hayo kiuchumi na hivyo kukwamisha maendeleo
ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
“Mimeo inazongwa na magonjwa mengi
tu, kuna magonjwa ya kahawa. Zamani tulikuwa tunapata misaada ya dawa kwenye
kahawa kutoka serikalini lakini sasa hivi haipo misaada hiyo, tunathirika
kiuchumi na kisaikolojia” anasema Nguma
Akitoa mchanganuo wa gharama za
kulima mahindi alizotumia mwaka jana, Nguma anasema alianza kwa kununua mbegu
za kisasa ambazo zinauzwa TZshs10,000 kwa kilo na hivyo alinunua kilo kumi
kiasi ambacho kinafaa kupandwa katika shamba la heka moja.
Mbali na gharama za mbegu pia
alikodi trekta kwa shilingi Tzshs40,000, akalipa vibarua kupanda mbegu TZshs40,000,
vibarua parizi TZshs50,000, mbolea TZshs50,000, vibarua wa kuweka mbolea TZShs30,000
lakini matokeo yake mahindi yalipotoa tu mbelewele yote yalikauka na hivyo
kupata hasara kubwa.
Bernard Pantaleo, Afisa Kilimo Kata
ya Kirua Vunjo Magharibi anakiri kuwepo hali mbaya ya mfumo wa kilimo katika
kata yake inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa elimu ya
kutosha kwa wakulima wa eneo hilo.
Bernard Pantaleo, Afisa Kilimo Kata
ya Kirua Vunjo Magharibi
Anasema chemichemi za asili
zimekufa na kwamba zinaathiri mwenendo wa kiuchumi na kiafya. Ingawaje kuna
mabwawa ambayo yangeweza kutumiwa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini hata hivyo
mabwawa hayo yanamilikiwa na watu binafsi likiwemo bwawa la Muhorohoro, Choro
na Kanje ambapo vijiji havina mamlaka nayo tena.
Kwa kuzitambua changamoto
zinazowakumba wakulima zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, wao kama
serkali ya kata wanatoa elimu ya kupanda miti na kutoikata hovyo, kutojenga
kwenye vyanzo vya maji, kufanya kilimo hifadhi na kupanda mazao yanayostahimili
ukame.
“Hali ya kilimo katika miaka ya
hivi karibuni ni mbaya sana hapa kwetu, hali ya ukosefu wa chakula hasa mahindi
inawakabili wakazi wa kata ya Kirua vunjo Magharibi, mwaka huu kuna hatari ya kuwa
na njaa” anasema Pantaleo
Bwawa la Muhorohoro
Akizungumzia mchango wa taasisi ya ICIPE
kupitia mradi wake wa CHIESA katika Wilaya ya Moshi Vijijini, Pantaleo anasema
mradi huo ulikuja kwa lengo la kupima hali ya hewa na kuwashirikisha wananchi
katika kutambua changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na njia
za kukabiliana nayo.
Anasema mradi huo uliweka vifaa vya
kupima hali ya hewa ili kutoa taarifa hizo katika vituo vya redio na
televisheni ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa hizo.
“Mwanzoni walipokuja walitoa mafunzo
kwa wananchi wote wa vijiji vya kata hii, lakini baada ya hapo sijaona tena
wakifanya kitu zaidi ya kupita tu hapa wakielekea kwenye vituo hivyo vya kupima
hali ya hewa.” anasema Pantaleo na kuongeza kuwa.
“Taarifa za hali ya hewa pia
zilipangwa kubandikwa kwenye mbao za matangazo kwenye kata ili wananchi waweze
kuwa na maandalizi stahiki ya kufanya kilimo lakini hawajawahi kufanya hivyo”
Chemichemi ya Miwaleni
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa
Kijiji cha Kisangesangeni, Alphonce Mgalla chemichemi ya Miwaleni ni muhimu
sana kwa mahitaji ya maji ya kunywa, kilimo na ufugaji na inategemewa na watu wengi
wa vijini vinavyoizunguka.
Afisa Mtendaji wa
Kijiji cha Kisangesangeni, Alphonce Mgalla
Chemichemi hiyo imezungukwa na
vijiji vya Kisangesangeni, Miwaleni, Uchira, Koresa, Mwangalea, Ngasimu A na B,
Moria, Mawala, Kiwanda cha sukari TPC, kiwanda cha Ngano na maeneo mengi ya Kata
nzima ya Kahe.
Hata hivyo chemichemi hii
inakabiliwa na changamoto za shughuli za binadamu zikiwemo kulima kwenye vyanzo
vya maji, kukata miti na kufanya ujenzi wa makazi ndani ya chemichemi hiyo.
Mfereji wa maji unaotokana na chemichemi ya Miwaleni
Kwa kuona umuhimu wa chemichemi
hiyo kwa wananchi sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,
CHIESA kwa kushirkiana na Mamlaka ya Bonde la Mto Pangani na wananchi wa vijiji
vya Sangesangeni na Miwaleni wameanzisha vuguvugu la utunzaji wa chemichemi hiyo.
“Kuna timu imeundwa ambayo inalenga
kuhamasisha kuhifadhi chemichemi hii ambayo imeshirikisha watu wenye ushawishi
vijijini na wadau mbalimbali ngazi ya kijiji na wilaya.” anasema Mgalla
Mradi wa CHIESA kwa kipindi cha
miaka mitatu umekuwa ukifanya utafiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa
kuweka kituo cha hali ya hewa katika kijiji cha Kisangesangeni na
kuwashirikisha wananchi ili kupata maoni yao juu ya njia gani zitumike
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“CHIESA walikuwa wanashirikisha
wananchi kutafuta dawa, nafikiri watakuja na dawa baada ya utafiti wao
kukamilika” anasema Mgalla
Mradi wa CHIESA
Akizungumza kwa niaba ya Msimamizi wa mradi wa CHIESA
Kilimanjaro, Prof. Shadrack Mwakalila, Mtaalam wa Mambo ya maji kutoka Bonde la
Mto Pangani, Philipo Patrick anasema kuwa Mradi wa CHIESA unasimamia matumizi
ya rasilimali ya maji, kuangalia uharibifu wa vyanzo vya maji na kuangalia hali
ya hewa kwa kuweka vifaa maalumu vya kupima hali ya hewa, katika meneo ya Moshi
vijijini.
Kituo cha kupima hali ya hewa kwenye kijiji cha Kisangesangeni
Anasema mradi huo
umewashirikisha wananchi katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Moshi Vijijini
katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mabadiliko ya tabianchi jambo ambalo
limefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu ya awamu ya kwanza ya mradi huo.
Vile vile anaashiria kwamba baada ya kukamilika kwa awamu ya
kwanza, wanajiandaa kufanya utekelezaji wa awamu ya pili itakayohusisha usambazaji
wa taarifa zilizopatikana kwenye awamu ya kwanza ya mradi jambo ambalo
litawawezesha wananchi kuchukua hatua stahiki za kuboresha kilimo chao na
kupata maendeleo.
Utafiti huu pia ulilenga kupata taarifa zaidi za namna gani
Bonde la mto Pangani na vyuo washiriki ambao ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine wataweza kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi kwa kushirikiana na Halimashauri za Wilaya.
“Katika kushirikiana na wananchi kuibua njia za kukabiliana
na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, tumeona ni muhimu kuwepo kwa mashamba
darasa mengi ili wakulima wengi washiriki kujifunza na kulinda chemichemi kama
njia moja wapo ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji” anasema Philipo
Makala hii imekujia kwa ufadhili wa CFI.