Miradi ya Mkuhumi inavyosaidia kuhifadhi mazingira nchini

Sekta ya ardhi nchini ni ya kipekee katika uthibiti wa mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa ndiyo sekta pekee ambapo ndipo uzalishaji na ... thumbnail 1 summary
Sekta ya ardhi nchini ni ya kipekee katika uthibiti wa mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa ndiyo sekta pekee ambapo ndipo uzalishaji na uondoaji wa kaboni hutokea.

Mfumo wa matumizi mapana ya ardhi ambao siyo endelevu unapaswa ubadilishwe ili nafasi yake ichukuliwe na matumizi ambayo ni sahihi na endelevu zaidi tofauti na hali ilivyokuwa mwanzo. Hatua hiyo ni pamoja na kutumia vyema ardhi iliyopo kwa kupunguza uzalishaji wa gesi joto unaotokana na ardhi.

Mnamo mwaka 2009, Ubalozi wa Ufalme wa Norway nchini Tanzania ulianza kuwa chachu ya ufadhili wa miradi saba ya majaribio ya Mkakati wa Kupunguza Ukataji Hovyo  na Uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) kwa kutoa dola za Kimarekani zipatazo milioni 100 kufadhili mradi huo.

Fedha hizo zilipelekwa kwenye taasisi za elimu ya juu nchini ambazo zinajukumu la kuandaa wataalamu mbalimbali.
Taasisi zilizopata fedha hizo ni pamoja na Chuo Kukuu Cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa lengo la kuendesha mafunzo na utafiti.

Fedha nyingine zilipelekwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kitivo cha Tathmini ya Rasilimali ambako huko pia waliingia mkataba na Asasi zisizo za Kiserikali (NGO’s) za hapa nchini ili kutekeleza mkakati wa MKUHUMI vijijini.

Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt Julius Ningu hivi karibuni alibainisha kuwa MKUHUMI ni moja ya maeneo ya utekelezaji wa mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi ambao unalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto katika sekta ya misitu, mkataba huo uliosainiwa katika mkutano uliofanyika nchini Indonesia mwaka 2008.

“Gesi joto ni mchanganyiko wa gesi mbali mbali zinazozalishwa kutokana na shughuli anazofanya binadamu kama vile viwanda, kilimo, sekta ya usafirishaji, magari, na mitambo inayotoa gesi mbalimbali ambayo hupanda hadi kufikia umbali wa kilometa moja hadi moja na nusu kutoka uso wa dunia na huko hutengeneza utando mzito (tabaka la gesi joto)”, alisema Dkt Ningu.

Ongezeko la hewa ukaa unasababishwa na uharibifu wa misitu kutokana na shughuli za kilimo cha kuhama hama na upanuzi wa makazi ya watu na miji ambapo maeneo ya misitu yanabadilishwa na kuwa makazi ya watu,  ufugaji huria usio endelevu, uchomaji moto wa misitu unaofanywa kwa makusudi kutokana na mila na desturi pamoja na shughuli za viwanda zinazofanyika katika nchi zinazoendelea.

Madhumuni ya mkakati MKUHUMI ni kushughulikia masuala ya ardhi, misitu na usimamizi wa kaboni wenye tija kwa namna mbalimbali ikiwamo ushirikishwaji mpana wa wadau katika ngazi mbalimbali.

Aidha, mkakati huo unalenga kupunguza uzalishaji wa kaboni itokanayo na matumizi ya ardhi kwa kiwango kinachoweza kuhakikiwa na kuzisaidia kaya masikini kuainisha vyanzo mbadala vya kujipatia mapato ambavyo havitegemei  uvunaji wa misitu usio endelevu.

Ili kuwa na maendeleo endelevu ya nchi, mradi wa MKUKUMI umeainisha malengo mengine ambayo ni kujenga utayari wa wananchi katika shughuli zake nchini, kufanya majaribio ya kisera kupata matokeo bora ya MKUHUMI na kuwezesha wadau mazingira kuwa na ushirikiano wenye tija.          
         
Katika kuimarisha juhudi hizo za kuboresha mazingira na kupunguza hewa ya kaboni, zipo pia Asasi zisizo za kiserikali (NGO’S) zinazotekeleza mradi wa MKUHUMI hapa nchini.

Asasi hizo ni pamoja na shirika la kimataifa la CARE, Taasisi ya Jane Goodall, mradi  wa kaboni wa shirika la The African Wildlife Foundation, shirika la World Wildlife Foundation na shirika la World Wildlife Fund.

Asasi nyingine zinazojishughulisha na kupunguza hewa ya kaboni ni Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania, Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika la Uhifadhi wa Mpingo na maendeleo na Taasisi ya Wildlife Conservation Society.

Asasi hizo zinafanya kazi hiyo kupunguza hewa ya kaboni katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Tanzania, Kigoma na Uvinza, wilaya za Lindi, Kigoma, Mpwapwa, Kondoa na Zanzibar.

Maeneo mengine ambayo miradi ya MKUHUMI inatekelezwa hapa nchini ni zile sehemu yenye aina nyingi za misitu kama vile nyanda za juu milimani, misitu ya miombo kwenye maeneo yenye ukame na maeneo ya maji maji, misitu ya ukanda wa Pwani, mapori ya acacia, na maeneo yenye misitu ya mikoko.

Akizungumzia suala hilo hivi karibuni jijini Dar-es-Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Sazi Salula alipokuwa katika mkutano wa wadau wa mazingira uliohusu utekelezaji wa miradi ya majaribio ya MKUHUMI, alisema kuwa Watanzania hawana budi kuzingatia namna bora ya kuhifadhi mazingira, upangaji wa matumizi  bora ya ardhi na utekelezaji wa mipango ili kuleta tija na maendeleo endelevu nchini.

Naye kiongozi wa miradi ya majaribio ya MKUHUMI ndugu Merja Makela alisema kuwa taasisi yake imesifika kutokana na kutekeleza na kusimamia miradi hiyo kwa makini katika maeneo husika nchini.

Athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu ni pamoja na hali ya hewa kutofautiana kwa hali mbalimbali ikiwemo urefu wa msimu wa kiangazi au masika ambayo huchangia uharibifu wa uzalishaji mazao, uwepo wa njaa na upotevu wa amani ambapo baadhi ya makabila huingia kwenye mapigano ya kugombea ardhi.

Mbali na hayo, athari nyingine inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ni pamoja na kuwepo kwa mvua nyingi mfano El nino ambazo husababisha mafuriko, uharibifu wa mali, upotevu wa maisha ya watu na mali zao pia ongezeko la fukuto la joto katika uso wa dunia linasababisha ongezeko la ukame unaoathiri mazingira ambayo ni mahali pao pa makazi.

MKUHUMI katika kutekeleza majukumu yake imekuwa na faida nyingi zinazopatikana kutokana na miradi hiyo ikiwa ni pamoja na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania kwa kushirikiana na MJUMITA kuweza kutoa kiwango cha kaboni kilichohakikiwa kwa ajili ya mauzo.

Aidha, miradi MKUHUMI imeleta manufaa muhimu yasiyo ya kaboni yakijumuisha ongezeko la usalama wa jamii wa kufanya maamuzi juu ya usimamizi wa maliasili zao pamoja na msitu wa Masito Ugalla ulioko mkoani Kigoma wenye ekeri 93,000 uliokuwa umesambaratika ulifanikiwa kurudishwa na wanyamapori walirudi na shughuli za ufugaji ya nyuki ulianzishwa.

Kiasi cha uzalishaji wa kaboni  kimepunguzwa kwa nchini kutoka tani 39,896  kwa mwaka mmoja kuanzia 2012 katika eneo la Lindi, na tani 27,600 zimepunguzwa kwa mwaka mmoja Kusini Mashariki mwa Tanzania katika misitu 10.

Manufaa mengine ya mradi huo ni kuwa watu zaidi ya 50,000 nchini wamefikiwa na elimu ya mazingira katika eneo la Kusini Magharibi  mwa Tanzania kupitia mradi wa Taasisi ya Wildlife Conservation Society.

Aidha, miradi hiyo imewanufaisha wananchi maskini kwa kuhakikisha zinaongeza ufikaji na ufanisi wa shughuli za mazingira zinawafikia kwa usawa  pia kuwepo kwa mgawanyo sawa wa faida za kifedha katika ngazi mbali mbali.

Miradi hiyo imekuwa na manufaa makubwa ya ziada ya kaboni ikiwemo ulinzi zaidi wa haki za miliki za ardhi na misitu, uboreshaji wa usimamizi wa maliasili, vyanzo vya maji na kupunguza upotevu wa bioanuwai.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, shirika la mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kupitia mkutano wa kimataifa wa 21 uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam ilikubalika kuwa Afrika iwe na kauli moja  ya kuwahamasisha vijana wa jinsia zote  washiriki kutoa maoni na kuchangia  masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.

Katika mkutano huo, Makamu wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilali alisema kuwa  kuna kila dalili ya maeneo ya ukame kuongezeka kwa asilimia 5 hadi 8  barani  Afrika ifikapo mwaka 2080 kutokana na matumizi ya nishati ambayo husababisha joto la dunia kuongezeka kwa asilimia zaidi ya 0.74.

Miradi ya MKUHUMI inakabiliwa na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na kiwango cha chini cha uzoefu na uelewa wa taasisi zinazotekeleza au kushughulikia masuala ya mazingira na fikra dhaifu miongoni mwa wananchi, zinazohusisha usimamizi endelevu wa uvunaji wa misitu na ufuatiliaji dhaifu wa matokeo.

Imetayarishwa na Jovina Bujulu-MAELEZO