Utafiti: Kiwango cha maji Ziwa Victoria kuongezeka, kufurika na kuharibu miundombinu ya maendeleo

Dotto Kahindi RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21 Wakazi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria huenda wakaku... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi
RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21
Wakazi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria huenda wakakumbwa na hatari ya kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha katika maeneo hayo na ziwa hilo kufurika maji, imefahamika.
Ziwa Victoria
Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa katika miaka 10 ijayo kutakuwa na ongezeko kubwa la mvua katika maeneo yote yanayozunguka Ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.

Utafiti uliofanywa na Idara ya Sayansi ya Majini, Nchi kavu na Anga katika Chuo cha North Carolina State cha nchini Marekani, unatoa tahadhari kwa wananchi na mamlaka mbalimbali za serikali na binafsi kuzingatia utafiti huo wakati wa kuandaa mipango yao ya kimaendeleo na kiuchumi kwani utaleta madhara makubwa.

Mkurugenzi wa Idara hiyo Dr. Fredrick Semazzi anasema miongoni mwa madhara yatakayojitokeza kutokana na ongezeko la mvua hizo ni pamoja uharabifu wa miundombinu ya barabara, reli, makazi, vitega uchumi na miundombinu ya uzalishaji wa umeme.

Wakati hali ikitarajiwa kuwa hivyo kwenye ziwa victoria maeneo ya kaskazini mwa Tanzania, kwenye mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro itakumbwa na ukame mkali.
Dr. Semazzi
Akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa tano wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Afrika (CCDA-V) uliofanyika Victoria Falls Zimbabwe, Semazzi anasema ili kukabiliana na janga hilo ni vyema mamlaka za mipango miji kuweka mipango ya kukabiliana na jambo hilo ambalo linatajwa kutokea kati ya miaka 10 hadi 15 kuanzia sasa.

“Ongezeko la mvua kwenye ukanda wa ziwa Victoria linatarajiwa kuwa kubwa baada ya miaka kumi kuanzia sasa, ukiiangalia unaiona ni miaka mingi lakini kimipango na maendelea ni michache sana, hivyo malmaka husika zinapaswa kulizingatia hilo katika kuweka mipango yao” anasema Semazzi

Utafiti huo pia umeonyesha kuwa kufurika kwa maji kwenye ziwa victoria kutasababisha uharibifu kwenye uzalishaji kupitia kilimo, ufugaji na uvuvi.

Pengine utafiti huu umetolewa wakati muafaka ambapo kumekuwa na kasi ya uwekezaji katika jiji la Mwanza na maeneo yanayolizunguka ikiwemo ujenzi wa hoteli, majengo makubwa ya biashara (malls) na viwanda ambavyo bila tahadhali vinaweza kukumbwa na janga hilo.

Kwa takribani miaka 30 sasa kiwango cha mvua kwenye ukanda wa ziwa victoria kimeendelea kupungua hali ambayo inatajwa kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi lakini hali hiyo inatarajiwa kuwa tofauti katika miaka kumi ijayo kwa kiwango hicho kuongezeka kwa haraka katika ukanda huo.

Ziwa Victoria
Ziwa Victoria lililopo Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya maendeleo ya Tanzania, na hata nchi nyingine kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Misri inayopata huduma ya maji ya Mto Nile unaoanzia kwenye ziwa hili la kwanza kwa ukubwa barani Afrika na la pili kwa ukubwa duniani.

Kutokana na kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira katika ziwa hilo lenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 68,100, utafiti wa kitaalamu unathibitisha kwamba samaki wamepungua kutoka kati ya tani 400,000 na 500,000 hadi tani 243,564 kwa mwaka 2010, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.

Ziwa Victoria lenye kina cha wastani wa mita 40 (futi 130), na mwambao wa urefu wa mita 4,828 (maili 3,000) linapata maji yake mengi kutokana na mvua (80%) na kutoka vijito vingi vidogo. Mto mkubwa unaoingia Victoria ni Mto unaotiririka kutoka upande wa magharibi.

Eneo la maji ya ziwa imegawanywa kwa 6% (4,100 km2) nchini Kenya, 45% (31,000 km2) nchini Uganda, na 49% (33,700 km2) nchini Tanzania ambapo miji mikubwa kandokando ya ziwa hilo ni Jinja na Entebe kwa Uganda, Kisumu kwa Kenya na Mwanza kwa Tanzania.

Eneo la kijiografia lilipo Jiji la Mwanza kunalifanya kuwa jiji pekee kubwa katika Ukanda wa Ziwa Victoria linalofikika kirahisi kutoka nchi zote tano zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), za Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Tanzania. 

Vitega uchumi vya kimkakati kama ilivyo Rocky City Mall, vinalipa Jiji la Mwanza fursa kubwa zaidi kuweza kuiishi ndoto yake ya kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa Makuu. 
Rock City Mall. Picha na Milardayo.com
Lakini wataalamu wa mambo ya hali ya hewa na mipango miji wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa ya madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kufurika kwa ziwa Victoria kama utafiti huu unavyoonyesha.

Hatua madhubuti
Dr. Semazzi anashauri ushirikishwaji wa wanasayansi ili wafanye utafiti kabla ya uandaaji wa mipango yeyote ya maendeleo ile ili kuweza kubaini madhara yanayoweza kujitokeza katika kipindi hicho.

“Mamlaka zinahitaji kupata mpango mzuri utakaoweza kubainisha madhara na ujio wa janga hilo mapema ili kuwe na muda wa kutosha kupanga namna ya kukabiliana nayo” anasema Semazzi

Anasema nyenzo zinazotumika kupima hali ya hewa hazitasaidia kitu kama hakutatolewa mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa, maafisa mipango miji na wanasayansi ili kuwajengea uwezo wa kubaini mambo hayo kabla ya kupanga mipango ya muda mfupi au mrefu.

“Sijui kama wanasayansi wanashirikishwa kikamilifu katika mipango ya maendeleo, lakini itakuwa vizuri kuwashirikisha vinginevyo itakuwa ni uharibifu wa fedha watu kuwekeza katika miradi ambayo itaharibika kwa muda mfupi” anasema Semazzi na kuongeza:

“Watu wanatakiwa kuwa makini na suluhu za muda mfupi kwa kuwa huongeza madhara zaidi nadhani ni muhimu kuishirikisha jamii kuanzia ngazi za chini mpaka ngazi za juu ili kupeana ufahamu wa kutosha juu ya mambo haya”.

Tayari kumekuwepo na jitihada za kupunguza athari za kimazingira kwenye ziwa Victoria ambapo Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira wa Bonde la Ziwa Victoria (LVEMP II) umekua mkombozi mkubwa wa mazingira kwa wananchi wa ukanda wa Ziwa, ikiwa pamoja na kudhibiti tatizo la magugu maji.

Akizungumza jijini Mwanza katika maonyesho ya kuadhimisha siku ya Mazingira Dunia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira Mhe. Binilith Mahenge anasema mradi huo ambao unasimamiwa na kuratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) mpaka sasa kwa upande wa Tanzania miradi midogo iloyochini ya mradi wa LVEMP II ipatayo 19 imekamilika na 197 iko katika hatua za utekelezaji.

Pengine utafiti huu utakuwa chachu kwa kamisheni hii kufikiria juu ya kukabaliana na mafuriko yatakayojitokeza hapo usoni kwa mujimu wa utafiti huo ambao ni muhimu kuzingatiwa na kufanyiwa kazi mapema.

Hotuba ya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Titus Kamani, aliyoiwakilisha bungeni wakati wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2014/2015 inaeleza jumla ya tani 38,574 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 44,260 zimeuzwa na kuiingizia Serikali mapato ya shilingi bilioni 6.1.

Pamoja na kwamba idadi hiyo ya samaki waliouzwa na kiwango cha fedha kilichopatikana sio cha samaki waliovuliwa ziwa Victoria pekee lakini inatoa mwanga wa kaisi gani sekta ya uvuvi nchini inavyochangia pato la mwananchi na taifa kwa ujuma na kwamba kufurika kwa ziwa Victoria kunaweza kuathiri uchumi huo
Habari hii imefadhiliwa na CFIMedia21 Project