Dotto Khaindi
RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21
Wanakijiji
katika Wilaya ya Kishapu wanakumbwa na ukame wa hali ya juu unaotokana na
athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini badala ya kukaa na kuilalamikia
serikali na kuomba msaada wa chakula wanakijiji hawa wameamua kutumia maarifa
yao kubuni njia mbalimbali za kukabiliana na athari hizo.
Kwa usaidizi
wa karibu wa shirika la kikristu linalotoa huduma kwa wakimbizi Tanganyika
(TCRS), wananchi katika vijiji mbalimbali vya Kata ya Ngofila wilayani Kishapu
wamefanikiwa kubuni miradi ya upandaji miti na ufugaji nyuki kama njia ya
kujipatia kipato na kutunza mazingira.
Drop Irrigation |
Peter
Jibungu, mkazi wa kijiji cha Busongo ni miongoni mwa wanakijiji hao ambapo yeye
amepanda miti ya aina tofauti kwenye shamba la ukubwa wa hekari tatu baada ya
kupata elimu ya namna ya upandaji na utunzaji wa miti kwa njia ya umwagiliaji
wa matone (Drop Irrigation).
Anasema
elimu hiyo ameipata kutoka TCRS ambao pia walimpatia miti na chupa za matone “Baada ya kunielekeza namna ya kupanda na kuitunza miti,
nilianza kutumia njia hizo kwa upandaji na umwagiliaji." Jibungu anasema.
Anasema toka
apande miti hiyo pamoja na ukame wa hali ya juu katika kijiji hicho miti yake
haijakumbwa na tatizo lolote lile kwakuwa amekuwa mwangalifu katika kumwagilia
na kuisimamia.
“Miti inakua vizuri, mwaka jana pia
nimepanda miti mingine na kufikisha idadi ya miti 3660 iliyohai na hali yake ni
nzuri sana, kuna michache ilikufa kutokana na ukame lakini mingi imestawi na
inanipa matumaini ya kuendelea kupanda mingine.” anasema
Jibungu.
Kulingana na
maoni yake Jibungu, upandaji miti umebadilisha maisha yake na kuwa yenye
matumaini “Sasa hivi maisha yangu yako vizuri
niko kwenye maandhari nzuri inayozungukwa na miti Napata upepo mwanana lakini
zamani nilikuwa peupe sana upepo ulitusumbua mara kwa mara, sasa hivi kwangu ni
kama masika, miti ni ya kijani kabisa”
Anasema kuwa
pamoja na kwamba miti yake haijafikia katika umri wa kuuza lakini miaka
michache ijayo ataanza kuuza na kujipatia kipato kikubwa. Jibungu anasema kwa
sasa anatumia miti kupata kuni za matumizi ya nyumbani, kivuli, hewa safi na
kinga dhidi ya upepo na vimbunga ambayo vilikuwa ni tishio kwake kipindi cha
nyuma.
“Sijaanza kuuza miti, ila nafikiria
kuweka mizinga ya nyuki ili niwe napata asali. Na kwenye pori hilo nyuki
wanafaa kabisa. Wananikijiji wanashangaa kuona nyumba yangu imezungukwa na pori
la miti tofauti na zamani hapakuwa hata na mti wa kivuli." Jibunga anasema
na kuongeza kuwa.
“Wanakiji wamehamasika sana kuhusu
kupanda miti, maana ni njia pekee ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi isiyokuwa na gharama kubwa, nao wameanza kupanda miti katika mashamba
yao”
Namna ya uandaaji wa chupa za
umwagiliaji
Njia ya
umwagiliaji wa matone ni njia ya kienyeji ambayo haihitaji uwekezaji mkubwa ili
kuitumia kama ilivyo katika aina nyingine za kilimo cha umwagiliaji ambacho
huhitaji uwekezaji wenye gharama kubwa kufanikisha.
Mzee Jibungu
anasema ili kufanikisha kilimo cha miti kwa umwagiliaji wa aina hii mkulima
anapaswa kuwa na eneo la kupanda hiyo miti, kuandaa shamba, kupata miche ya
miti, kuandaa chupa za maji zilizokwishatumika (chupa za maji ya Uhai,
Kilimanjaro, Dasani na kadhalika) kisha zoezi la kupanda miti.
Anasema
makopo hayo hutobolewa tundu dogo kwenye mfuniko wa chupa kwa kutumia spoku ya
baiskeli na kisha hujazwa maji na kuegeshwa kwa kuinamishwa kwenye kila mche
uliopandwa ambapo chupa moja yenye ujazo wa lita moja ya maji hukaa kwa muda wa
siku nne.
Anasema njia
hii imemsaidia sana kukuza miti yake kwakuwa hutumia maji kiasi kidogo sana na
hivyo kuepukana na adhari ya ukame. “Mwaka huu
(2015) hakukuwa na mvua kabisa huku Kishapu lakini utaratibu huu umenisaidia
kukuza miti” anasema Jibungu
Jibungu
amepanda miti mchanganyiko katika shamba lake ambapo kuna miti ya asili na ile
ya kisasa, mingi ikiwa ni kwaajili ya mbao na nguzo ambayo anatarajia kuanza
kuiuza baaada ya miaka mitano hadi kumi kuanzia sasa.
“Miti hii inachukua kama miaka kumi
kukomaa kufikia kukata mbao, kwa hiyo baada ya miaka mitano mpaka kumi ijayo
nitaweza kuvuna miti kwa mbao”anasema Jibungu.
Wakati huu
ambao kilimo chake cha miti kikiendelea kustawi na akisubiri kufikia wakati wa
kuuza mwanakijiji huyo anafanya kilimo cha mazao ya vyakula kama vile mtama,
mahindi, uwele, alizeti na kunde, ambavyo humsaidia kwa chakula na kuuza na pia
kwa mahitaji ya familia.
Ufugaji nyuki
Andrew
Shigela mbaye ni mwanakijiji wa Inolelo, Kata Ngofila, Kishapu, Shinyanga ni
mmoja kati ya viongozi wa kundi la Mshikamano linalojihusisha na ufugaji wa
nyuki kwa muda wa miaka miwili sasa.
Kundi la
Mshikamano linaamini kuwa ufugaji nyuki ni njia muhimu katika kukabiliana na
athari za ukame zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kwakuwa njia hii
inawapatia kipato na kuwawezesha kuendesha familia zao.
“Mwaka jana (2014) tulianza na mizinga
7 lakini kufikia muda huu tuna mizinga 48. Tumeshaanza kuvuna asali tayari,
tunavuna kila baada ya miezi mitatu, tulivuna mwezi wa sita, tukavuna tena wa
tisa na tunategemea kuvuna tena mwezi wa 12” anasema
Shigela.
Kulingana na
Shigela zamani walikuwa wakivuna asali kwa njia za kienyeji lakini sasa
wamenunua vifaa maalumu vya kuvuna asali japo uvunaji bado uko chini
ikilinganishwa na idadi ya mizinga waliyonayo.
Mavuno ya
asali kwa awamu mmoja ni kati ya lita 60 hadi 100 kiasi ambacho ni kidogo sana
na huchangiwa na uchelewaji wa kuanza zoezi la uvunaji asali “Hawa nyuki wa kienyeji wajanja sana, mkichelewa kidogo tu
mnakuta wameshakula asali yote, hii ni changamoto kwetu lakini tutaikabili
kwakuwa iko ndani ya uwezo wetu” anasema Shigela.
Kikundi hicho
cha wafugaji asali kina wanachama.25, wanaonufaika na asali na fedha wanazopata
kutokana na ufugaji huo. Pesa hizo za asali huhifadhiwa kwenye akaunti ya benki
ya kikundi kwaajili ya kuendeleza mradi wao huku kiasi kidogo cha pesa
wakigawana kwaajili ya mahitaji muhimu ikiwamo kusomesha watoto, kusaidia
watoto yatima na wasiojiweza.
Lita moja ya
asali jijini Dar es Salaam, huuzwa kati ya 80,000TZS mpaka 10,000TZS wakati
kwenye maeneo ya mikoani ikiwemo Shinyanga huuzwa kati ya 40,000TZS na
80,000TZS.
Mkulima
mwingine Joseph Kadala, kutoka kijiji cha Ngofila, kata ya Ngofila Wilaya ya
Kishapu, Shinyanga analia na hali ya ukame jinsi inavyokwamisha na kurudisha
nyuma mipango na maendeleo ya wakulima Kishapu.
Anasema kwa
sasa hawategemei kilimo cha mvua hasa katika kijiji cha Ngofila zaidi ya
kutumia kilimo cha umwagiliaji wakitegemea zaidi maji kutoka kwenye mto mdogo
wa Manonga ambao hauko mbali na kijiji chao.
“Mto wenyewe hauna maji mengi, kwahiyo
tunachofanya ni kuanza kulima mwezi wa nne na kufikia mwezi wa saba tunakuwa
tumeshavuna. Changamoto ya kilimo cha umwagiliaji huwezi kutumia shamba kubwa
hivyo tunalima heka moja kwa mazao ya chakula na tunapata hata gunia tano
(gunia moja lina kilo 100)” anasema Kadala.
Kijiji cha
Ngofila kina kaya 430, ambazo zina wakaazi 3466 hata hivyo hali ya ukame
imesababisha umaskini kuongezeka ambapo hakuna uwezekano wa familia kupata milo
mitatu kwa siku.
Wakati
kijiji cha Inolelo, kina mwamko wa hali ya juu katika kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi kwani kuna shamba lenye msitu wa kupandwa ekari 15 za miti ya
milonge na miarobaini na ndani ya msitu huo kuna mradi wa ufugaji nyuki.
Faida za kilimo cha miti
Kilimo cha miti
kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya
mazingira ambapo kwa hapa Tanzania mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa maarufu
inayoongoza kwa misitu mikubwa ya kupandwa.
Miti
inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea pamoja na utengenezeji wa
karatasi lakini ukiacha mahitaji haya hivi sasa kumeibuka fursa nyingine mpya
ambapo mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua hewa ukaa (carbon
dioxide).
Kwa maana
hiyo mkulima anaweza kupanda shamba la miti halafu akawa anakusanya dola kwa
kuuza hewa ukaa wakati akisubiri miti ikomae avune mbao, nguzo ama miti ghafi
ya kutengenezea karatasi.
Mwezeshaji wa TCRS, Genes Tarimo, anasema kazi yao ilikuwa ni kuwawezesha wakulima hao ujuzi na maarifa ya kupanda miti na ufugaji wa nyuki na kuwapatia nyenzo za kuanzia kama mbegu (miche) za miti na mizinga ya nyuki.
Mwezeshaji wa TCRS, Genes Tarimo, anasema kazi yao ilikuwa ni kuwawezesha wakulima hao ujuzi na maarifa ya kupanda miti na ufugaji wa nyuki na kuwapatia nyenzo za kuanzia kama mbegu (miche) za miti na mizinga ya nyuki.
Tarimo asema
miti waliyotoa kwa wakulima ilipatikana kwa ushirikiano mkubwa na ofisi ya
misitu ya Kishapu ambapo miti zaidi ya 20,000 imepandwa katika Wilaya ya
Kishapu katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2015.
“Nashauri
uoteshaji wa miti ufanyike katika maeneo ya vijijini ili wananchi waweze kupata
miti kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Kutoa miti mbali kwanza ni changamoto
kwakuwa wakati mwingine haiendani na eneo hilo na inatumia gharama kubwa pia” anasema Tarimo.
Habari hii imefadhiliwa na CFIMedia21 Project