Mabadiliko ya tabianchi yataathiri mipango ya maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki

Dotto Kahindi, Paris, Ufaransa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Balozi Dr. Richard Sezibira Mipango ya kim... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi, Paris, Ufaransa

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Balozi Dr. Richard Sezibira
Mipango ya kimaendeleo katika nchi za Umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inaweza kushindwa kufanikiwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoweza kuathiri utekelezaji wa mipango hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja huo Balozi Dr. Richard Sezibira anasema kuwa kukosekana kwa sera ya pamoja ya mabadiliko ya tabianchi itakayoainisha maeneo ya vipaumbele na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na ukuzwaji wa viwanda ni changamoto kubwa katika maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza na mtandao wa tabianchi (http://tabianchi.blogspot.fr/) wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21, unaoendelea Paris, Ufaransa, Dr. Sezibira anasema ili kuboresha uchumi wa Afrika Mashariki ni muhimu kuwepo kwa sera ya mabadiliko ya tabianchi itakayokwenda sambamba na uanzishwaji wa mfuko wa mabadiliko ya tabianchi kwa nchi z Afrika Mashariki.

Sera hiyo itatoa vidokezo muhimu vya namna changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza kutumia kama fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo katika ukanda huo hasa katika sekta ya kilimo na viwanda.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inajumuisha nchi za Jamhuri ya Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimefanikiwa kuwasilisha mchango wake wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined Contributions – INDCs). Kila nchi iliyowakilishwa katika COP21 wamewasilisha mchango wao  na kujifaragua kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Pamoja na michango hiyo kuwashirikisha wadau kutoka sekta binafsi, mashirika ya serikali ngazi za kitaifa na wanaharakati wa mazingira, lakini hakukuwa na ushirikishwaji wa pamoja baina ya nchi na nchi ndani ya jumuiya hiyo.

Kukosekana kwa ushirikiano huo wa kuandaa INDC’s kunaweza kuathiri utekelezaji wa shughuli au miradi mtambuka ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inahitaji ushiriki wa pamoja wa nchi wanacham wa jumuiya ili kufikia lengo.
Hata hivyo Richard Sezibira anasema ili kuhakikisha nchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki zinashirikiana pamoja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wameanza taratibu za kuunda Sera na Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi itakayowezesha kupata mswaada wa mabadadiliko ya tabianchi.

“Kwa sasa  tuko kwenye majadiliano na baadae mswaada utawasilishwa kwenye bunge la Afrika Mashariki mara baada ya kupitishwa na mawaziri wa nchi husika” anasema Dr. Sezibira.

Kulingana na Dr. Sezibera jambo la pili wanalolishughulikia ni kuanzishwa kwa mfuko wa mabadiliko ya tabianchi wa Afrika Mashariki ambapo majadiliano yanaendeleo ili kujua mfumo wa mfuko huo utakuwaje.

“Majadiliano yanaendelea ili kujua kama mfuko huu ujitegemee au uwe ndani ya mfuko mwingine ambao upo tayari, na mfuko huu unalenga kusaidia shuguli za kubabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza athari zake” anasema.

Dr Sezibera anakiri kuwa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inaweza kuathiri pia shughuli za kimaendeleo katika nchi za Afrika Mashariki, hasa maendeleo ya viwanda kwakuwa dunia ya sasa inahitaji kuwa na viwanda rafiki wa mazingira.

“Ili mipango yetu ya maendeleo iendane sambamba na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, tumeanzisha kituo cha nishati mbadala cha Afrika Mashariki, tunahitaji kushirikiana pamoja ili kufikia mipango hii kwa manufaa ya jumuiya yetu” anasema.

Kwa Upande wake Mwakilishi wa Shirika la Environment Compliance Institute (ECI) nchini Kenya, Gerry Opondo (pichani) anasema kuandaliwa kwa INDCs hakujazingatia umoja wa nchi za Afrika Mashariki jambo linaloweza kuathiri juhudi za umoja huo za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Kuna mipango mizuri EAC ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini mipango hiyo inaweza kupata kigugumizi katika utekelezaji wake kwa kuwa INDC’s zilizowasilishwa  zinalenga nchi moja moja, ambazo zinaweza kupingana katika utekelezaji wake” anasema Opondo.

Opondo anadadisi kuwa baada ya makubalino ya Paris kufanyika, INDC’s hazitakuwa michango bali zitageuka kuwa matakwa ya lazima ya kila nchi kuyatekeleza na ingekuwa ni jambo jema kama mataifa yote ya EAC yatatekeleza ili kunufaisha nchi zote za jumuia hiyo.