Dotto
Kahindi, Le Bourget, Paris, Ufaransa
Kupitia mradi wa CFIMedia21 nimekuwa miongoni mwa
waandishi wa habari, Bloggers na Watangazaji kutoka nchi za Afrika na Asia waliohudhuria
Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21, uliofanyika Mjini Paris, Ufaransa
Disemba 2015.
Makala hii fupi inalenga kutoa ‘mtazamo wangu’ juu ya mambo kadhaa
yaliyojitokeza kwenye mkutano huu.
Wanufaika wa mradi wa CFIMedias21 kutoka Afrika na Asia katika picha ya pamoja |
Maandalizi
Maandalizi ya mkutano huu ambayo yamefanywa na
wenyeji Serikali ya Ufaransa kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mkutano wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) yamekuwa ni ya hali ya juu
kufanikisha jambo hili.
Ufaransa ilijipanga sawasawa kuhakikisha mkutano
huu unafanyika katika mazingira mazuri yatakayotoa mwanya kwa nchi wanachama wa
mkutano, wanaharakati, waandishi wa habari na wadau wengine wa mabadiliko ya
tabianchi kufanya kazi zao katika mazingira mazuri.
Mkutano huu umefanyika Le Bourget, Paris,
Ufaransa, eneo ambalo hutumika kama uwanja mdogo wa ndege lakini likabadilishwa
kwa muda ili kutosheleza mahitaji ya mkutano wenyewe.
Usafiri
Utaratibu wa alama za usafiri na namna ya kufika
eneo la mkutano ulikuwa mzuri na rahisi jambo ambalo liliwezesha kila mtu
kufika Le Bourget kila alipotaka kufanya hivyo.
Kwa wale waliotumia treni kuna alama za uelekeo wa
treni ya kuelekea kwenye mkutano, kwa kuwa kuna treni nyingi na zinakwenda
sehemu tofauti hii ilikuwa na msaada mkubwa kwa wenzangu na mimi ambao kujua ni
mpaka kuona.
Kulikuwa na mabasi ambayo yaliwachukua washiriki
kutoka kwenye kituo cha treni kwenda kwenye eneo la mkutano, ambayo yalikuwa
yakiondoka kila baada ya dakika 5.
Ukarimu
(Hospitality)
Inawezekana kulikuwa na mafunzo mazuri kwa
wasaidizi katika mkutano huo ambao muda wote hata pale walipokuwa na njaa
walitabasamu na kukaribisha washiriki kwa upendo.
Hii si tu kwa wahudumu katika mkutano huo ambao
walikuwa kila kona kuanzia kwenye vituo vya treni, kwenye mabasi, na katika
mkutano wenyewe bali hata kwenye maeneo ya hoteli tulipoishi mambo yalikuwa
murua.
Ulinzi
na Usalama
Kulikuwa na ulinzi wa hali ya juu katika mkutano
huu pengine ni kutokana na shambulio la kigaidi lililotokea mapema mwezi
Novemba 2015, hivyo walihakikisha washiriki katika mkutano huu wanashiriki
salama bila kuwa na shaka ya shambulio.
Ukaguzi wa mali za washiriki walizoingia nazo
kwenye mkutano ulikuwa mkali sana, kila ukiingia ‘wali-scan’ mizigo yako yote
na kuchunguza kibali chako cha kuhudhuria mkutano huo, jambo ambalo liliondoa
hofu ya watu wengi ya kuwa huenda kukawa na shambulio kwenye mkutano huo.
Chakula
Kwakweli kwenye chakula mambo ndo yalikuwa magumu,
yaani ni full mikate, miti (mboga za majani), burger, sandwhich nk, yaani kwa
wale tunaotoka Musoma na Kakamega kwetu ilikuwa kama mboga tu, kwa kifupi muda
wote tukiwa Paris tulikuwa tunakula mboga.
COP ijayo nitabeba unga wa muhogo na mahindi
halafu nitajipikia mwenyewe, haipendezi kabisa kukomba mboga kwa masiku yote
hayo.
Vyumba
vya habari (Newsrooms)
Kama ni kujali waandishi wa habari basi mkutano
huu ulijali sana waandishi pamoja na kuwa na idadi kubwa ya waandishi lakini
kulikuwa na vifaa vya kutosha vya kutendea kazi hasa kompyuta na makabati ya
kutunzia vifaa vingine.
Kulikuwa pia na eneo la kupumzika (Kulala) maalumu
kwa waandishi wa habari ili kupunguza uchovu wa mihangaiko ya kutafuta habari
ndani ya mkutano huo ambazo zilikuwa na changamoto kubwa pia. Pia kulikuwa na intaneti
nzuri
Afrika
Ni mataifa machache tu ya Afrika yaliyoweza kuweka
mabanda yake au vituo vya taarifa kwenye banda kubwa la Afrika (African
Pavillion), kwa bahati mbaya katika nchi hizo chache Tanzania pamoja na
kupeleka ujumbe wake kwenye mkutano huo haimo.
Kwa Tanzania pengine ni kutokana na kutokuwa na
waziri kwa wakati huu, au pengine ni kutokana na kubana matumzi yasiyo ya
lazima kama alivyoagiza Rais Magufuli lakini nilidhani ingekuwa muhimu kutumia
fursa hizi kutangaza mambo muhimu ikiwemo fursa za biashara na uwekezaji pamoja
na utalii.
Mataifa mengine yalikwenda na ushawishi wa miradi,
biashara na uwekezaji ili kuutumia mkutano huo kupata washirika watakaosaidia
kutumia changamoto za mabadiliko ya tabianchi kama fursa za kiuchumi.
Kama kuwa na banda la Tanzania pekee ni gharama
basi kungekuwa hata na banda la Afrika Mashariki lakini haikuwa hivyo,
ushirikiano wa Afrika Mashariki unahitajika pia katika mambo muhimu kama ya
mabadiliko ya tabiachi. Si Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi ama Uganda
waliokuwa na banda.
Mashirika
ya Binafsi na Wanaharakati
Afisa Miradi Forumcc, Fazal Issa akihamasisha katika moja ya maandamano waliyoyafanya wakati wa COP21 |
Mashirika binafsi na wanaharakati walikuwa na
nafasi kubwa sana ya kufanya ushawishi katika majadiliano hayo kwa manufaa ya
nchi wanazotoka ambapo Tanzania tulipata nguvu kutoka ForumCC ambao walishirikiana
na PACJA.
ForumCC kwa kushirikiana na PACJA wameleta mchango
mkubwa katika kuwezesha kupatikana kwa andiko la mkabata wa mabadiliko ya
tabianchi.
Ni taasisi hii ambayo ilikuwa mstari wa mbele
kusema, kukosoa na kutoa mapendekezo mbadala ambayo yangefaa kuwamo kwenye
mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi na mchango wao umeifanikiwa kwa kiasi
kikubwa sana
Niliwatumia pia katika kupata ufafanuzi wa kina wa
vipengele vya mkataba huo ili kuuelewa vizuri kabla ya kuupasha umma wa
watanzania na wapeni wa mtandao wangu kwa ujumla
Place-to-B
Miongoni mwa shughuli za ubunifu zenye lengo la
kuwaunganisha watu wa mataifa mbalimbali katika kupambana na mabadiliko ya
tabianchi bila kujali wanatoka katika fani gani, Place-to-B ilionekana sehemu
muhimu sana.
Mpango huu ambao unaendeshwa na Anne-Sophie Novel
kwa lengo la kupata mawazo ya kibunifu kutoka pande tofauti za dunia.
Kwa kutambua kuwa mpango huu ungewakutanisha watu
wengi, Place-to-B iliamuliwa ifanyike kwenye hoteli ya St. Christophers Inn iliyopo
Gare du Nord, ambayo ina uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 600 kwa usiku mmoja.
Kulikuwa na shughuli mbalimbali zilizoendelea
katika Place-to-B na moja wapo ilikuwa ni majadiliano, uandaaji wa vipindi vya
radio, televisheni na kulikuwa na kipindi cha televisheni ambacho kilirushwa
moja kwa moja kutokea hapo.
Ni eneo hili ambalo nilipata nafasi ya kukutana na
viongozi, wanaharakati, wanahabari kutoka mataifa mbalimbali na kubadilishana
mawazo.
Uwakilishi
wa Tanzania
Pamoja na Tanzania kutokuwa na Waziri wa Mazingira
katika majadiliano ya mkutano huu wa Paris, kazi kubwa iliyofanywa na balozi wa
Tanzania nchini Ufaransa, Begum Taj ambaye kwa kushirkiana kwa ukaribu na
mwakilishi wa Tanzania kwenye mkutano huo Dr. Richard Muyungi wamecheza karata
yao vizuri.
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe Begum Taj akiwa na Dr. Richard Muyungi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania |
Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huu ulikuwa na
jumla ya watu 12, idadi ambayo
ilimjumuisha balozi huyo na walikuwa na kazi kubwa ya kusimamia maslahi
ya nchi katika kufikia makubaliano ya mkataba huo mpya wa mabadiliko ya
tabianchi.
Ujumbe
huu ulieleza kuwa Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Kimarekani 65 bilioni
sawa na bilioni 140 kwa mwaka kwa ajili ya kutekeleza mchango wake wa kila nchi
katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended
Nationally Determined Contributions – INDCs).
Magufuli
Jambo ambalo sikutegemea kulipata Paris ni namna
watu wanavyomkubali Rais mpya wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli, kutokana na
utendaji aliouonyesha kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli |
Pengine kutokana na kupenda kwangu kuvaa skafu
yenye rangi ya bendera ya Tanzania ilikuwa rahisi kwa watu wengi kutambua
utaifa wangu na jambo la kwanza walilouliza baada ya salamu ilikuwa ni
Magufuli.
Wanaamini chini ya uongozi wa Magufuli mikataba ya
kibwenyenye haitapata nafasi na hivyo utekelezaji wa mambo yote yatakayoamuliwa
kwenye mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi utasimamiwa mguu kwa mguu kama
sio jicho kwa jicho.
Sifa hii pia inaongeza matumaini kwa nchi wahisani
kuwa na imani ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika miradi ya maendeleo na
madailiko ya tabianchi kwakuwa usimamizi na uwajibikaji utakuwa umeongezeka
ndani na nje ya serikali ya Tanzania
Mkataba
wa mabadiliko ya tabianchi
Baada ya majadiliano makali baina ya nchi
wanachama wa mkutano huo mnamo siku ya Jumamosi, Disemba 12, 2015 makubaliano
ya mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi yakafikiwa.
Pamoja na mkataba wenyewe kuwa na mapungufu kadhaa
lakini nchi ziliufurahia ikiwa kama ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye
makubaliano mapana yenye manufaa kwa wote.
Miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye mkataba huo ni
pamoja na Kiwango cha nyuzi joto, Upunguzaji wa gesi Joto, Kukabiliana na
mabadiliko ya tabainchi, Uharibifu na upotevu, Fedha za mabadiliko ya tabianchi
na Mfumo wa taasisi.
Hatua inayofuata baada ya majadiliano ya Paris
kumalizika, ni Katibu Mkuu wa COP kuwaalika wanachama wote Aprili 22, 2016 ili
kutia sahihi mkataba huu na utakuwa wazi kuridhia mpaka 2017.
Idadi ya nchi wanachama wanaotakiwa kuasini ili
kuupa nguvu ya kuanza kutumika mkabata huo ni 55, idadi ambayo ni karibu na
theluthi moja ya nchi wanachama wa mkutano huo ambayo ni 196.
Makala ifuatayo itaeleza na kuchambua kwa kina
vipengele vyote vya mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi, endelea kutembelea
mtandao huu