Dotto Kahindi
Pamoja na kuwepo
kwa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 ambayo inaweka makatazo mahsusi kwa nia
ya kuepusha uharibifu wa mazingira lakini Taarifa ya Hali ya Mazingira Nchini
inaonyesha uharibifu wa mazingira ni wa kutisha.
Mito mingi nchini
inakauka, Vyanzo vingi vya maji vinakufa, Miti na misitu ya asili inapungua kwa
kasi kubwa kila mwaka na taifa linapoteza zaidi ya ekari milioni moja za misitu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira January Makamba (MB) anasema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba Sheria hii inatekelezwa kwa ukamilifu wake ili kupunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Anasema mwanzoni
mwa mwaka ujao (2016) Serikali italeta mpango kabambe wa kupambana na uharibifu
wa mazingira, ambao utatoa wajibu kwa kila mwananchi na kila taasisi ya umma na
binafsi.
Makamba anakiri
kuwa uharibifu wa mazingira unaathiri sekta zote muhimu ikiwamo kilimo, mifugo,
uvuvi, utalii, uzalishaji umeme, makazi, miundombinu na hivyo kupunguza uwezo
wa nchi kupata maendeleo endelevu.
“Tukiendelea na
mwenendo wa sasa wa uchafuzi wa mazingira, ndani ya kipindi kifupi, mifugo na
wanyamapori watakosa malisho, tumeshaanza kuona viboko wanakufa kwenye Mto Ruaha
kutokana na kukauka kwa mto, watu watakosa maji ya kutumia, kilimo
kitashindikana” anasema Makamba
Tayari Serikali ya
awamu ya Tano imeanza kutekeleza mipango yake ya kuyalinda mazingira kwa
kuanzisha operesheni ya kuwaondoa watu wanaoishi na kufanya shughuli kwenye
maeneo ya kingo za mito na maziwa, fukwe za bahari, maeneo oevu (swampy) na
maeneo ya wazi (Open spaces).
Kwa Dar es Salaam,
zoezi la kuwaondoa wananchi waliojenga au kufanya shughuli kwenye maeneo haya
kinyume cha sheria na taratibu lilianza rasmi tarehe 17/12/2015 likiratibiwa na
kusimamiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kushirikiana na mamlaka za
Serikali za Mitaa.
Makamba anasema
kuwa ongezeko la watu jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya miji, uvamizi
wa maeneo ya kingo za mito, mikondo ya bahari, maeneo oevu umeongezeka kwa watu
kufanya ujenzi wa nyumba, kilimo, ufugaji, utupiaji taka na uchimbaji mchanga.
“Shughuli hizi
katika maeneo hayo husababisha uharibifu na madhara makubwa ya mazingira hasa
kipindi cha mvua ambapo maji hukosa uelekeo kutokana na njia zake za asili
kuzibwa na hivyo kutawanyika hovyo na kusababisha mafuriko, uharibifu mkubwa wa
miundombinu hasa madaraja ambayo huvunjika, kukatika kwa barabara na vifo”
anasema Makamba.
Anataja athari
nyingine za kuvamia maeneo hayo kuwa ni kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko
yasiyoisha hasa kipindupindu kutokana na maeneo hayo ya mikondo ya mito kutokua
na mfumo wa utoaji wa maji taka.