Na Asteria Muhozya
WAZIRI
wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ameiaigiza Kampuni ya
Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC Ltd) kuwa ifikapo June 2016, iwe
imeanza kuchoronga mashimo 3 katika eneo la Ziwa Ngozi ikiwa ni hatua ya
mwisho inayohitajika kabla ya kuanza kujenga mitambo ya kuzalisha
jotoardhi.
"Utafiti
muhimu umekamilika. Joto la maji ni kubwa, 230-250C linalokidhi
uzalishaji wa umeme. Hiki kitakuwa ni chanzo kipya muhimu cha umeme
jadidifu" ,alisema Prof. Muhongo.
Ameongeza
kuwa, jambo hilo haliwezi kuendelea kusubiri kutokana na mahitaji ya
nishati hiyo nchini ikizingatiwa kuwa, Tanzania inapitiwa na Bonde la
Ufa kwa kiasi kikubwa.
"Tayari
wenzetu Kenya na Ethiopia wamepiga hatua kubwa katika nishati hii lakni
kwa upande wetu hatuna megawati hata moja kwa hili lazima tuchukue
hatua tutoke hapa tulipo. Hakuna kusubiri anzeni na Ziwa Ngozi" amesema
Muhongo.
Prof.
Muhongo aliitaka Kampuni hiyo kuongeza nguvu katika eneo lenye
viashiria vya jotoardhi la Ziwa Ngozi kutokana na kuwepo maendeleo
makubwa ya kitafiti ikilinganishwa na maeneo mengine yenye viashiria
kama hivyo ikiwemo eneo la Mbaka lililopo Wilaya ya Rungwe.
"TGDC
tunataka umeme wa jotoardhi, wananchi wanataka umeme, hawatakuwa
kusikia maneno, ifikapo Mwezi juni na mimi nitakwenda Ngozi kuangalia
mmefikia wapi na kama hakuna maendeleo tutabadilisha timu ya wataalamu",
alisisitiza Prof. Muhongo.
Akizungumzia
kuhusu fedha za miradi, Prof. Muhongo alieleza kuwa, nchi nyingi
duniani hazitegemei fedha za Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya
nishati na ndiyo sababu hata Tanzania inatafuta fedha katika taasisi
mbalimbali ikiwemo kukaribisha wawekezaji ili kutekeleza miradi hiyo.
"Serikali
kwa upande wake itasaidia kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza
miradi na ninyi kazi yenu ni kuhakikisha umeme wa jotoardhi unaanza
kutumika Tanzania kwa kuanza na Ziwa Ngozi".
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema kuwa amefarijika na
maelekezo aliyoyatoa Prof. Muhongo na kuahidi kuweka nguvu kubwa katika
kufuatilia suala hilo. " Ujio wako umetupa ari mpya katika kusimamia
miradi hii kwa sababu rasilimali zipo lakini zimekaa tu nakuahidi kasi
ya ufuatiliaji itaongezwa",alisema Kandoro
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rugwe ,Mwalimu Zainabu Mbusi alieleza
kuwa maagizo ya Prof. Muhongo yamekuwa faraja na kuongeza kuwa,
kukamilika kwa mradi huo itaongeza kasi ya ukuaji uchumi na kuifanya
Tanzania kufikia lengo lake la kuwa miongoni mwa nchi za uchumi wa Kati
ifikapo 2025.
Kwa
pande wake Mbunge wa Jimbo la Busokelo, Fred Atupele alieleza kuwa,
kukamilika kwa mradi huo kutachochea kasi ya uendelezaji wa viwanda
vikubwa na vidogo na kueleza kuwa, kwa nafasi yake watachukua jukumu la
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa vyanzo hivyo.
Awali
akieleza akieleza Mikakati ya Taasisi hiyo, Mkurugenzi wa TGDC ,
Mhandisi Boniface Njombe alisema eneo la Mbaka ni miongoni mwa maeneo ya
maji moto yenye viashiria vya nishati ya jotoardhi.
Vilevile,
alieleza hivi sasa wataalam kadhaa wamesambaa wakifanya tafiti za
mwisho katika eneo la Mbaka ili kuanisha mipasuko na maeneo ya kuchimba
nishati hiyo na kuongeza kuwa, TGDC imelenga kwa kuanza kuzalisha
umeme wa jotoradhi wa kiasi cha megawati 200 huku lengo ikiwa ni
kufikia megawati 5000.
Aidha,
alieleza kuwa, mbali na kuzalisha umeme , maji moto yanaweza kutumika
viwandani na majumbani katika kukausha mazao ikiwemo kuwa kivutio cha
utalii kuoga kwa kuwa inaelezwa kuwa maji hayo yanatajwa kuwa tiba ya
magonjwa ya ngozi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopitiwa na Bonde la Ufa eneo ambalo linatajwa kuwa na viashiria vya nishati ya jotoardhi.