Makubaliano ya mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi 'Paris Agreement' kuanza kusainiwa leo

Na Mwandishi Maalum, New York Zaidi ya nchi 162 zinatarajiwa  kutia saini leo ( Ijumaa) Makubaliano kuhusu mabadiliko ya Tabia  Nc... thumbnail 1 summary
Na Mwandishi Maalum, New York

Zaidi ya nchi 162 zinatarajiwa  kutia saini leo ( Ijumaa) Makubaliano kuhusu mabadiliko ya Tabia  Nchi  ambayo yalifikiwa  jijini Paris -Ufaransa  mwezi Desemba Mwaka jana.

Miongoni mwa nchi ambao zimethibitisha kushiriki  hatua  hiyo muhimu   na ambayo ni hatua ya mwanzo  kuelekeza utekelezaji wa  makubaliano hayo maarufu kama Paris Agreement ni  pamoja  na  Mataifa makubwa kiuchumi  duniani  na  ambayo  yanachangia  kwa asilimia kubwa  katika utoaji wa  hewa ya ukaa.

 Baada ya utiaji  saini wa makubaliano  hayo katika mkutano ambao umeandaliwa na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa  Ban Ki Moon,  nchi wanachama wa Paris Agreement  watatakiwa ama kupitisha  makubaliano hayo  au  kuridhia ( ratification).

Ili  hatua ya utekelezaji  ianze Nchi 55  zinatakiwa kuridhia  makubaliano hayo  ndani ya  siku  thelathini,  na nchi hizo 55 zinatakiwa ziwe ni zile ambazo  kwa ujumla wake zinachangia asilimia 55 ya hewa ukaa.

Taarifa kutoka  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa  zimeeleza  kuwa mataifa makubwa kama  Marekani na  China yameonyesha nia ya kutia saini  makubaliano hayo  huku nchi ndogo  na zinazoendelea zipatazo 13  zinatarajiwa  kusaini na kuridhia makubaliano hayo.