Dotto
Kahindi
Kama wote tunavyojua kuwa serikali imekusudia
kuzima simu feki nchini ifikapo Juni 17, 2016 ambapo maelfu ya simu yatatupwa
na watu takribani milioni 1.2 wataathiriwa
na hatua hiyo
Pamoja na kulalamikiwa na watu wengi hasa
wananchi wenye kipato cha chini kuwa mpango huu utakuwa mateso kwa wanachi hao
lakini mamlaka husika zimesisitiza kuwa
ni muhimu kuzima simu feki zote ili kupunguza tatizo la wizi kwa kutumia
mitandao ya simu inayofanywa zaidi za simu za aina hiyo.
Nakubaliana na serikali kuwa faida za kuzima
simu simu feki ni kubwa kuliko kuacha matumizi ya simu hizo yakiendelea lakini
swali langu la msingi ambalo pengine wengi hawajaliangalia ni wapi mabaki ya
simu feki zitakazozimwa tutaenda kuyatupa
Taka hizi za kielectroniki (e-waste) zina
madhara makubwa kwa mwanadamu na mazingira endapo hazitahifadhiwa kiutaalamu na
kuzingatia athari zake katika mazingira.
Taka hizi nyingi hubeba madini ya Mercury na
kemikali nyingine hatarishi ambazo madhara yake ni makubwa mno katika maisha ya
wanadamu, viumbe hai na hata mimea.
Kwa wasiofahamu merchury ya mfumo wowote ule
ni sumu na huathiri mfuo wa fahamu, chakula na figo. Sumu ya mercury inaweza
kupeneza na kuingia mwilini kwa njia ya mfumo wa kuvuta mvuke katika hewa yenye
mercury, kula, kuchoma sindano au kufyonzwa kwa njia ya ngozi
Kwa njia hizo za namna sumu hiyo inavyoweza
kusambaa, kipi tunaweza kufanya, kuzikusanya na kuzitupa kwenye majalala? Kuzichoma?
Najua kuna wengine kwakuwa walizipenda sana simu zao watataka walau waziweke
kwenye kabati kama kumbukumbu, sijui nao watakuwa salama
Hatari ya taka hizi ni kubwa mno, mvua
ikinyesha hubeba vipande vya mabaki ya vifaa vya kielectroniki ambavyo huwa na sumu
hizo mpaka kwenye maji, ambayo maji haya baadae hutumika kwa kuoga, kufua, na
kunywa wakati mwingine. Unaweza kupata picha ya madhara yake yanaweza kutufikia
kirahisi kwa namna gani.
Ukisema uchome moto hizi taka, nayo ni hatari
kubwa, maana moshi wake umejaa sumu kali ambayo inaweza kukupata kwa kuvuta
moshi wake. Madhara ni mengi sana lakini turejee katika swali la msingi.
Je serikali yetu kupitia wataalamu wa
mazingira wamelitafakari hili kwa makini? Je kuna njia ya kitaalamu ambayo
wataitumia kuhifadhi na kuziteketeza taka hizi? Je kuna utaalamu wa kutosha
hapa nchini wa kubadili matumizi ya taka hizo (recycling, reuse)?
Nategemea kuona hatua madhubuti zinachukuliwa
na mamlaka husika, kwa kutueleza baada ya simu zetu kuzimwa, mabaki yake
tukayatupe wapi.