Hakuna kitu kinachowaharibu vijana wa Tanzania kama madawa ya kulevya na viroba.
Lakini wakati vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya ikionekana
kuendelea kuwa ngumu, serikali inakaribia kupata ushindi kwenye vita
dhidi ya viroba. Serikali imetangaza kupiga marufuku utengenezaji,
usambazaji na uingizaji wa plastiki nchini hadi kufikia mwaka 2017.
Hiyo inamaanisha kuwa viroba vitakuwa vimechimbiwa kaburi lake moja
kwa moja. Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba wakati akizungumza na
waandishi wa habari Jumapili.
Alidai kuwa mifuko hiyo ambayo mingi hutolewa bure imekuwa mstari wa
mbele katika uchafuzi wa mazingira nchini. Alisema uamuzi huo utaanza
kutekelezwa ili kuwapa muda wafanyabiashara wanaoingiza mkate wa kila
siku kupitia biashara hiyo kutafuta nyingine mapema kabla mambo hayajawa
magumu kwao.
Pamoja na kuharibu nguvu kazi ya taifa, viroba ambavyo hutumiwa na
vijana wengi katika muda ambao walipaswa wafanye kazi, mifuko yake
imekuwa ikichafua mazingira ikiwa ni pamoja na kuziba mifereji
mbalimbali ya kupitisha maji.
Hata hivyo kuzuiwa kwa mifuko ya plastiki kutawafanya watengenezaji
wa vilevi vya bei chee kufikiria njia mbadala ya kufungasha zaidi ya
chupa zilizoeleka.
Chanzo: Bongo5