Uchambuzi: Mambo makuu matatu adui wa mazingira Tanzania

Picha na the Habari Dotto Kahindi Kilimo na ufugaji usioendelevu, uchimbaji wa madini na ukataji wa miti kwa matumizi ya ku... thumbnail 1 summary
Picha na the Habari

Dotto Kahindi
Kilimo na ufugaji usioendelevu, uchimbaji wa madini na ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni, mkaa na ujenzi ni mambo makuu matatu adui wa mazingira ambayo yanakwamisha jitihada za serikali na asasi mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira

Mambo hayo yameainishwa hivi majuzi na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira dunia, jambo ambalo linatoa fursa kwa serikali na wadau kwa ujumla kuweka nguvu zao katika kukabiliana na mambo hayo adui wa mazingira.

Kumjua adui yako ni hatua moja katika kujihakikishia ushindi wa vita, jambo la pili na muhimu ni kujua silaha za huyo adui yako ili iwe rahisi kwako kuandaa silaha zenye maangamizi kumshinda yeye wakati jambo la tatu ni kuweka mikakati madhubiti ya namna ya kutoa mashambulizi

Samia anataja njia kadhaa za kukabiliana na maadui hao ikiwemo kuundwa kwa kamati za mazingira kuanzia ngazi za vijiji, vitongoji, mitaa, kata na wilaya zitakazosimamia vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao.

Bila shaka Mama Samia anataarifa za kutosha kwamba mbinu na silaha hizi zitafanikisha kupunguza kama si kukomesha kabisa uharibifu wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji kama kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mazingira ya mwaka huu ambayo inahimiza uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu.

Tanzania iliamua kuwa na kauli mbiu tofauti na ile ya kimataifa ambayo inasema `Go Wild For Life' ujumbe ambao unahamasisha kuchukua hatua za kulinda maisha ya wanyamapori kwa kuwa wanaunda sehemu muhimu ya mazingira.

Hii ni kutokana na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji hapa nchini ambao umesababisha kupungua kwa mtiririko wa maji katika mito ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, baadhi ya mito imebadilika na kuwa ya msimu, kuchafuliwa na hata mingine kukauka.

Samia akasema uchafuzi wa mazingira wa vyanzo vya maji kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha ukiendelea, huenda itakauka ndani ya miaka 15 ijayo na hivyo kuhimiza upandaji wa miti kwenye maeneo yanayozunguka vyanzo hivyo na kupiga marufuku shughuli zinazoviharibu.

Vizuri tumewajua maadui japo kwa kuchelewa, lakini tunahitaji kushirikisha wadu na mamlaka mbalimbali kupima uwezo wao, ili tuweze kuandaa silaha na mikakati madhubuti ya kupamnana nao na hatimaye kunusuru vyanzo vyetu vya maji.